September 6, 2017


Na Saleh Ally, Manchester

EDGAR Davids alicheza msimu mmoja tu katika kikosi cha FC Barcelona. Lakini kabla ya hapo kazi yake ilijulikana uwanjani akianzia kwao Uholanzi katika klabu iliyomkuza kisoka ya Ajax.

Sifa ya Ajax inajulikana, ni kutengeneza vijana na kuwauza lakini kabla huwatumia kujipatia mafanikio makubwa na Davids ni mmoja wao.

Yeye alikuwa akijulikana kwa sifa ya kucheza kwa juhudi kubwa, ubabe na mjeuri kweli.

Sifa yake nyingine ukiachana na ukabaji, alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti na hasa nje ya boksi la 18.

Mwaka 2004 ndiyo pekee ambao alicheza Barcelona mechi 18 tu akitokea kwa mkopo Juventus na baada ya hapo, timu hiyo ikamuuza Inter Milan, akalazimika kurejea Italia baada ya mechi hizo akiwa amefunga bao moja.



Katika mahojiano mafupi yaliyofanyika jijini Manchester, Davids anasema hata sasa bado angependa kucheza kibabe kama atapata nafasi ya kucheza. Lakini analazimika kuwa mtulivu kwa mambo mawili.

“Kwanza viungo haviruhusu vurugu kama za wakati huo. Nilikuwa nina mazoezi ya ziada kila baada ya wenzangu kumaliza. Nilitaka kuwa fiti zaidi mara mbili ili niendeshe timu pia kuisaidia kukaba.

“Sipendi kushindwa, ningependa kucheza na kushinda. Ndiyo maana unaona nilikuwa napambana sana,” anasema.



Davids amecheza katika ligi kubwa tatu, yaani England, Hispania na Italia. Lakini alifanya vema akiwa na Ajax kwa kucheza mechi 106 na kufunga mabao 20.

Huko alipata mafanikio zaidi akichukua ubingwa wa nchi hiyo mara tatu, Kombe la Shirikisho la Uholanzi mara mbili, pia Ligi ya Mabingwa Ulaya na Uefa Super Cup.

La Liga hakudumu akaondoka, England alicheza Tottenham na Crystal Palace na hakukuwa na mafanikio makubwa sana lakini Italia ndiyo sehemu anaamini ilikuwa na ushindani wa juu zaidi.

“Italia ya wakati ule ilikuwa bora kuliko Hispania na England. Kama unakumbuka Serie A wakati huo, Juventus, AC Milan na Inter Milan zilikuwa zinashikilia kila kitu. Wachezaji bora wa dunia kama wanavyotokea leo Hispania walikuwa wakitokea Italia.

“Ushindani ulikuwa juu sana na kila mchezaji bora alitamani kucheza Serie A,” anasema.

Kuhusiana na ubora wake uwanjani na ushindani, anasema kiungo waliyekua naye kisoka Ajax, Clarence Seedorf ndiye alikuwa mpinzani wake mkubwa wakikutana lakini alikuwa akipata wakati mgumu kwa Zinedine Zidane maarufu kama Zizou.

“Yule alikuwa ni mtu wa aina yake, hauwezi kuujua ubora wake hadi utakapocheza naye. Huenda unaweza kudhani ni laini lakini Zidane alikuwa na nguvu sana.

“Silaha yake kubwa ilikuwa ni unyumbulifu. Hata akiuficha mpira ni vigumu kuuchukua kwa kuwa angeweza kugeuka sehemu ambayo hukuitarajia. Mimi alikuwa ananisumbua sana.

“Kila nilipokutana naye niliwaza sana suala la kadi. Nilitaka kuepuka kadi kwa kuwa mimi sikutaka mchezo.

“Hata wakati tukiwa wote Juventus kabla hajaenda Real Madrid, nilikuwa nikimueleza atoe mpira haraka, la sivyo nitampitia. Lakini hakuwa mtu mwenye papara na wala hakuwa mwoga,” anasema.

Akiwa na mpenzi wake, Olcay Giusen ambaye ni mwanamitindo, Davids aliamua kuanzisha kampuni ya mitindo inayohusiana na soka. Kampuni hiyo inajulikana kwa jina la Monta Soccer.

Monta Soccer imekuwa ikibuni aina mbalimbali za nguo za kike na kiume na kuziuza. Katika nchi kadhaa za Italia, Uholanzi na Hispania imepata umaarufu mkubwa.

Davids ambaye si mzungumzaji na huenda mgumu kumhoji, kwa kuwa hapendi kuzungumza au anaweza kujibu kwa kifupi, mara nyingi anasema kampuni hiyo zaidi inasimamiwa na mwandani wake huyo na yeye zaidi amekuwa akihusika katika utoaji wa mawazo huku akiendelea na maisha yake mengine.

Championi: Maisha yako, yapi hayo nje ya biashara yako?
Davids: Wewe inakuhusu nini? Niache tafadhali.
Championi: Si vibaya kujua ili mashabiki wajue pia.
Davids: Sina mashabiki (anainuka na kuanza kuondoka), bye.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic