September 25, 2017





Na Saleh Ally, aliyekuwa Manchester
KATI ya mechi ambayo imebaki katika kumbukumbu za mashabiki wa Arsenal ni ile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006 wakati FC Barcelona iliposhinda kwa mabao 2-1 na kubeba ubingwa.

FC Barcelona ilishinda mechi hiyo iliyochezwa Mei 17 kwenye Dimba la Stade de Fance, Saint-Denis, Ufaransa huku ikionekana Arsenal ilikuwa na nafasi kubwa ya kubwa bingwa. Tokea siku hiyo, Arsenal haijawahi kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa na haijarejea tena katika fainali.

Ingawa Arsenal ilionyesha ina nafasi ya kubeba kombe ikiongozwa na Thierry Henry lakini dakika ya 18, kipa Jens Lehmann alipigwa kadi nyekundu, Arsenal ikalazimika kumtoa Robert Pires na nafasi yake kuchukuliwa na kipa Manuel Almunia. Hii ilitibua mipango ya Arsenal.

Pamoja na kuwa pungufu, Arsenal ilikwenda mapumziko na bao la Sol Campbell katika dakika ya 37. Lakini kipindi cha pili, Barcelona ilisawazisha kupitia kwa Samuel Eto’o katika dakika ya 76 na dakika ya 80, Juliano Belletti akamaliza kazi.



Belletti raia wa Brazil mwenye asili ya Italia alifunga bao hilo katika dakika ya 80 na kuimaliza kabisa Arsenal ambayo imebaki na “stori” ya fainali hiyo hadi leo.

Championi ni gazeti lenye kupiga hatua au linalohangaika kupata vizuri kwa ajili ya wasomaji wake kwa kuwa limefanikiwa kumpata Belletti ambaye ameizungumzia fainali hiyo na kusema inabaki katika kumbukumbu yake kwa kuwa ni fainali ngumu zaidi aliyowahi kucheza katika maisha yake.

Belletti anasema, kamwe hawakuwadhulumu Arsenal kama watu wengi walivyosema na kila kitu kilikwenda sawa kwa sheria za soka ukianza na kadi ya Lehmann lakini hakukuwa na bao lolote lililolaumiwa.



“Kila kitu kilifuata utaratibu, angalia kadi ya kipa wao ilikuwa haki tupu. Tulishinda kwa haki lakini ulikuwa ushindi mgumu zaidi kwa kuwa hata wakati naingia katika dakika ya 71 kuchukua nafasi ya Oleguer, nilijua kuna kazi ngumu mbele yangu,” anasema katika mahojiano yaliyofanyika jijini Manchester, England.

“Unajua dakika ya 69, Oleguer alipewa kadi ya njano na kwa kuwa Henry alikuwa akimsumbua sana, haraka Kocha Frank Rijkaard aliniambia nisimame na kuanza kupasha misuli kwa hofu kuwa angepewa njano nyingine. Dakika moja tu nilitakiwa kujiandaa kuingia. Joto la Henry nililiona lakini kocha wetu alikuwa mjanja alisema, tuhamishie mashambulizi upande wangu na aliniambia kila mpira ufike kwa mtu, sikutakiwa kupoteza hata mpira mmoja na alinihesabia.



“Alifanya hivyo ili kupunguza kasi ya Henry na dakika 9 tokea nimeingia nilifunga bao la pili ambalo niliona Arsenal hawakulitarajia na walianza kulaumiana na baada ya hapo tuliambiwa kuumiliki sana mpira na ndipo tulifanya hivyo na kumaliza mchezo,” anasema.

Kwa misimu mitatu aliyokaa FC Barcelona, Belletti alifanikiwa kubeba makombe mawili ya La Liga, Super Cup ya Hispania na Ligi ya Mabingwa Ulaya na mwaka 2009 akaamua kujiunga na Chelsea.

Ingawa alikuwa ni beki wa kulia, lakini asili yake ni kiungo wa ukabaji pia alikuwa ana uwezo wa kucheza kama kiungo mchezeshaji.



Akiwa na Chelsea pia alipata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuchukua Ngao ya Jamii, Kombe la FA mara mbili, Ligi Kuu England mara moja na akatinga fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini wakapoteza kwa Man United kwa mikwaju ya penalti nchini Urusi. Kama unakumbuka nahodha, John Terry aliteleza na penalti yake ikaota mbawa.



Chelsea alikaa kuanzia 2007 hadi 2010 akiwa chini ya Kocha Jose Mourinho halafu Avram Grant, Luis Filipe Scolari, Guus Hiddink na mwisho Carlo Ancelotti.

“Chelsea ni klabu yenye mfumo wa peke yake kabisa. Ndiyo timu niliyokaa kwa muda mfupi na kufundishwa na makocha zaidi ya watatu. Lakini ambacho kinashangaza unaona makocha ni wengi na mafanikio yanapatikana.
“Kingine ambacho kinashangaza, makocha wengi tofauti kwa wakati mfupi lakini umoja wa wachezaji uko juu sana. Wanashirikiana kwa karibu na mabadiliko ya makocha hayawabadili wachezaji, wanazidi kuwa imara zaidi.


“Terry, Drogba na Lampard walikuwa kama ndiyo makocha. Maana wao hata aingie kocha gani iwe Mourinho au Hiddink ambao ni wakubwa na wana heshima zao, walikuwa wanalazimika kuwasikiliza. Unapokuwa nje ya Chelsea unaweza kuwaona ni watu wa kawaida lakini pale, ni watu wakubwa sana na kitu kizuri ni watu wenye upendo na heshima kwa kila mmoja wanayefanya naye kazi,” anasema.

Belletti anasema, Barcelona ni sehemu nyingine ambayo hawezi kuisahau kwa kuwa ushirikiano ulikuwa mkubwa katika kipindi ambacho watu kama Samuel Eto’o, Ronaldinho, Iniesta na Xavi Hernandez walikuwa katika kiwango cha juu kabisa na kuutikisa ulimwengu wa soka chini ya Kocha Rijkaard lakini miaka michache baadaye anaingia Pep Guardiola na ujio wa Lionel Messi ambaye kipindi hicho alikuwa kama mwanafunzi.

Mwaka 2001, Belletti aliamua kustaafu baada ya maumivu makali ambayo alishindwa kuyatibu. Anasema anaendelea kuzitumikia timu za wakongwe lakini kwa sasa anacholenga ni kuendelea na biashara inayohusiana na soka huku akisaidia wale ambao anaona wanaweza kufika mbali na kuendesha maisha yao.




1 COMMENTS:

  1. Hahahaha. Nimeipenda hiyo "Na Salleh Ally aliyekuwa Manchester" 😂😂😂😂😂. Hongera bro, tusalimie Manchester.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic