September 6, 2017



Uongozi wa klabu ya Azam umelishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya rais wake, Wallace Karia kwa kitendo cha shirikisho hilo kuzitaka timu za Simba na Yanga kwenda kucheza kwenye Uwanja wa Azam Complex, kwenye michezo yake ya ugenini wakiwa wanapambana na timu hiyo.

Hatua hiyo ya TFF kuziamrisha Simba na Yanga kucheza na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex imekuja hivi karibuni baada ya kufanyia marekebisho ratiba ya Ligi Kuu Bara jambo ambalo halikuwa linatokea awali kutokana na kucheza katika Uwanja wa Taifa au Uhuru kwenye mechi zote za ugenini na nyumbani.

Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd amesema kuwa wanaishukuru TFF kutokana na kuwaidhinisha kucheza kwenye uwanja wao wa nyumbani mbele ya klabu hizo kongwe tofauti na kipindi cha zamani ambapo walikuwa wanalazimika kutumia Uwanja wa Taifa, bila ya kujali wanacheza ugenini au nyumbani.

“Sisi kama Azam tunawashukuru sana TFF kwa kuturuhusu kutumika kwa uwanja wetu katika mechi zetu za Simba na Yanga kitu ambacho ni tofauti na ilivyokuwa inafanyika huko nyuma ambapo tulikuwa tunalazimika kucheza Taifa, bila ya kujali kwamba tupo ugenini au nyumbani.

“Tulikuwa tunashangazwa na kutotumika uwanja wetu mbele ya timu hizo wakati hpa tayari timu mbalimbali za Afrika zimeshacheza, lakini pia timu ya taifa, Taifa Stars, imecheza hapa na hakukuwa na lolote lililotokea.

“Kuhusiana na idadi ya mashabiki kila mmoja anafahamu uwezo wa uwanja wetu namba ya mashabiki ambao inaingia na kuhusu suala la usalama hilo tunawaachia TFF na idara zinaohusika na tunaamini hakutakuwa na jambo lolote litakalotokea,”alisema Jaffar.


Katika hatua nyingine Jaffar aliongeza kuwa kikosi chao chini ya kocha wake, Aristica Cioaba kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo huo wakiwa na nia ya kuibuka na pointi tatu huku wakitarajia kuwakosa washambuliaji wao wawili, Shaban Idd Chilunda na Joseph Kimwaga ambao wapo nchini Afrika Kusini wakiendelea na matibabu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic