September 29, 2017




NA SALEH ALLY
NIMEAMUA kuandika tena kuhusiaa na Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa nimekuwa kati ya watu wachache wanaoona Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefanya haraka kuhusiana na kuongeza timu zaidi Ligi Kuu Bara.

Kuongeza timu Ligi Kuu Bara ni kuwafanya wachezaji kucheza mechi nyingi zaidi wakiamini watakuwa imara zaidi na kuwafanya kuwa katika hali ya ushindani zaidi.

Mimi nasisitiza, hiyo ni haraka kwa kuwa kabla ya kuongeza timu ligi kuu, vema kuanza kuiboresha Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa ni ligi pacha ya ligi kuu.

Ligi hiyo, inatoa timu nyingi zinazoshiriki Kombe la Shirikisho ambalo linazikutanisha na timu za ligi kuu. Kama zitakuwa zinakutana timu imara, basi itakuwa sehemu moja ya kuiimarisha Ligi Kuu Bara.

Hivi karibuni niliwahi kulizungumzia hilo kwa upande zaidi, leo nimeanza kwa kulikumbushia lakini zaidi nitalenga kuhusiana na waamuzi wa Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa kwangu nawaona nao wamekuwa tatizo.

Baadhi ya waamuzi wa daraja hilo wamekuwa wakishiriki kampeni nyingi chafu kwa lengo la kufanikisha mambo ambayo si sahihi, jambo ambalo wanapaswa kubadilika mara moja na ikiwezekana wamuogope Mwenyezi Mungu.
  
Hauwezi kuwa mwadilifu kama hamuogopi Mwenyezi Mungu kwa kuwa wengi wanachokifanya ni dhuluma na tunajua, kabla serikali hata imani zetu za dini zinakemea tabia ya dhuluma hata ile ya kificho. Lakini jiulize dhuluma ya mbele ya macho ya watu rundo uwanjani.

Inawezekana kabisa, kwa kuwa TFF imekuwa haitupii macho ligi hiyo kwa kuwa nguvu nyingi zimeelekezwa Ligi Kuu Bara, basi wengine wamegeuza ni kichaka cha kuficha maovu yao na kufanya wanavyotaka, hii si sawa.

Kuna mikoa imekuwa ikifanya kampeni mahsusi za kuhakikisha timu zao zinapanda. Kampeni hizo za mkoa haziwezi kufanikishwa bila ya kuhakikisha waamuzi wanakuwa sehemu yao ili “kuinyonga” timu pinzani.

Tunajua hata zile timu pinzani, ili moja ifanikiwe kuinyonga nyingine, ni lazima ihakikishe inamtumia mwamuzi na aghalabu sana kuwatumia wachezaji wa timu pinzani.

Tunajua waamuzi wanatumika kama sehemu ya kufanikisha mambo ambayo si sahihi, jambo ambalo si jema na wanajua wanafanya ambacho si sahihi kama ambavyo taaluma yao inawaagiza kusimamia mambo kwa ufasaha.

Waamuzi ni wasimamizi wa mchezo wa soka, wao ndiyo wanafanya mambo yaende kwa utaratibu sahihi hasa kama unazungumzia katikati ya uwanja sehemu ambayo hata viongozi wa shirikisho hawawezi kuingia.

Tumeshuhudia malalamiko mengi kupindukia, waamuzi wa Ligi Daraja la Kwanza wamekuwa wakiona kama wako katika kichaka ambacho wanaweza kufanya wanavyotaka na mambo yakaendelea vizuri.

Kama nilivyosema mwanzo, kuna mikoa inafanya kampeni za kupandisha timu zao na wakati mwingine kuna viongozi wa mikoa wamekuwa wakishiri kampeni hizo, zikiwemo zile haramu. Waamuzi ndiyo wanaotumika na TFF ninaamini inalijua hili.

Huu ndiyo wakati mwafaka wa kuelezana ukweli na tuenze na waamuzi, kwamba mara moja waache mambo hayo.

Ukiachana na kuwasaidia kupandisha heshima au thamani yao, itausaidia mchezo wa mpira kukua lakini hii pia itachangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha yale matukio ya wao kupigwa hovyo yanapungua.

Sote tunajua, waamuzi wamekuwa wakipigwa kama wezi. Ni jambo ninalolipinga kwa nguvu zangu zote, lakini waamuzi wasio waaminifu basi vizuri nao wakanyoosha mambo na kufanya kazi yao kwa kuzifuata na kuzilinda Sheria 17 za mchezo wa soka.

Lakini TFF, lazima ihakikishe inamaliza kwa kufumua kichaka ambacho wanajificha waamuzi wasio waaminifu wanaochafua heshima ya wengine waaminifu na kuvuruga thamani ya kile watu wanachokipigania kikue.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic