September 12, 2017


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam; Mkuu wa Wilaya Temeke jijini pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa namna walivyoshirikiana na Shirikisho katika kusimamia mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania uliokutanisha timu za Azam FC na Simba.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Septemba 9, mwaka huu, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ameshukuru vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia utaratibu wa weledi katika kudhibiti kila aina ya vurugu kabla, wakati na baada ya mchezo huo.

“Watu wote walifika uwanjani kwa utulivu, walikaa vema uwanjani, baadaye waliondoka bila ya vurugu yoyote. Hakuna tukio lililolipotiwa kwangu kwamba kuna vurugu eti kwa sababu ya mechi… hakuna,” amesema Kidao.

Ameongeza: “Mchezo ulikuwa mzuri, nadhani kila aliyekuja uwanjani anaweza kuwa shahidi. Hii inatupa nguvu kwamba siku nyingine tunaweza kuandaa mchezo mwingine mkubwa katika uwanja ule.”

Amesema kwamba nguvu ya kuandaa mchezo mwingine mkubwa katika Uwanja wa Azam ni nguvu ya ushirikiano aliyoipata kutoka Serikali ya Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.


Mbali ya viongozi hao, Kidao pia aliwashukuru viongozi wa Simba na Azam pamoja na mashabiki wao kwa kudumisha amani katika mchezo huo ambao awali ilidhaniwa kuwa ungekuwa na vurugu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic