September 1, 2017


Na Saleh Ally
KIUNGO Pius Buswita kwa sasa anaunguruma karibu kila sehemu katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Ukisema sasa Buswita ambaye msimu uliopita aliichezea Mbao FC anasikika huenda hata kuliko Emmanuel Okwi ambaye katika mechi ya kwanza katika ligi ana mabao manne, wala hautakuwa umekosea.

Buswita ni bado kijana mdogo kabisa ambaye anajitafutia maisha na kusikika kwake wala si kwa sababu ya uwezo wake, badala yake anasikika kwa upuuzi wake alioufanya.

Hivi karibuni, ameingia kifungoni, mwaka mmoja na hii ni kutokana na kushindwa kuonyesha kutuliza kichwa chake na kujua anataka nini katika wakati gani.

Amesajili katika timu mbili, Yanga na Simba. Uamuzi wake wa kusajili timu hizo mbili umesababisha aingie matatizoni lakini cha kufurahisha, meneja wake anaamini “Shetani alimpitia”.

Shetani aliyempitia Buswita hatujaelezwa ni wa aina ipi lakini ukweli, shetani mwenyewe ni uamuzi mbovu wa Buswita kushindwa kutuliza kichwa chake na huenda ilichangiwa na tamaa.

Mambo mawili nayaona, moja ni tamaa ya fedha kutoka kwa kijana ambaye tayari alikuwa amesajili timu mmoja, alipokaa na viongozi wa timu nyingine wakaweka dau kubwa zaidi na kumshawishi asajili tena.

Pili ni kudanganywa na kwa kuwa hajitambui, akaona anachofanya ni sahihi. Tayari alisajili timu moja halafu akaambiwa upande mwingine ni bora zaidi, anachotakiwa ni kusaini tu na kuwaachia viongozi wao watalishughulikia suala la usajili wake TFF na timu nyingine itarudishiwa fedha zake.

Huenda kama alivyosema Msemaji wa Simba, Haji Manara, mambo hayo hufanyika sana na inaonekana uongozi mpya wa TFF chini ya Wallace Karia umeamua kunyoosha haki. Hivyo ugumu wa kuzungusha mambo unakuwa ni shida.

Wakati Buswita aliposaini Simba, tuliandika katika gazeti hili namba moja la michezo kwa sasa. Baada ya muda akasaini Yanga, tulipomtafuta na ninakumbuka nilizungumza naye mwenyewe, akasema ameambiwa awaachie viongozi ndiyo watalizungumzia.

Hivyo alibadilika, hakutaka kukubali amesaini Yanga au amekataa na hakutaka tena kulizungumzia suala la Simba. Hata tulipojaribu kumshawishi aliishia kusema alikutana na viongozi wote lakini asingependa kuzungumzia zaidi na anamuachia meneja wake.

Meneja wake ndiye aliyesema baadaye suala la “Kupitiwa na shetani” ambaye awali hakutaka kuzungumzia suala la Simba. Sasa anaonekana angependa Simba watoe msamaha kwa kijana huyo ingawa mwanzo aliwalaumu kama watu wabaya.

Wengi pia wanaendelea kuwasihi Simba, wamsamehe Buswita, lakini wako ambao wanaonyesha kufanya propaganda za kipuuzi ambazo zinaonyesha ushabiki wa kijinga kabisa. Lawama za moja kwa moja kwa Simba wakionekana kama wanataka kumzuia Buswita kujiendeleza kisoka.

Hakuna anayesema Buswita amefanya upuuzi, hakuna anayefungua mdomo wake kumkanya kwamba alifanya jambo baya. Hakuna anayeona kuwa wachezaji wetu wanapaswa kujielimisha, kuelimishwa na ikiwezekana kujitambua vema katika masuala muhimu.

Mfano, Buswita angekuwa na mshauri wa kisheria wakati anasaini Simba, isingekuwa rahisi kusaini tena Yanga na shetani aliyempitia asingemkuta. Au yeye angekuwa ni mtu anayejitambua, basi hakika suala hilo ambalo miaka ya 1990 kwa wale waliokuwa wanajitambua, hapa nyumbani lilikuwa ni jambo la kawaida tu watu kusaini timu mbili wakafungiwa.

Wanaoilaumu Simba bila kumueleza ukweli Buswita nikuendelea kujenga vijana wa hovyo wasiojitambua, pia ni kujihusisha na kina “shetani” wengine bila kujijua. 

Naona wanasikitisha sana kwa kuwa wanaangalia zaidi ushabiki badala ya uhalisia na kufanya mambo sahihi ili kusaidia mambo yaende vizuri sasa na baadaye na kumaliza kabisa mambo haya yaliyopitwa na wakati.

Ninatamani pia kuona Simba wanamsamehe Buswita, wala nisingependa kuona wanamfikisha mahakamani kama walivyodai. 

Najiuliza, Buswita mwenyewe anajifunza vipi kufanya jambo hilo la kipuuzi na kumsingizia shetani. Halafu wanaomzunguka, wanakubali kuwa shetani kutetea upuuzi wa shetani mkuu!

Kumueleza Buswita ukweli ni kumjenga, lakini ni kukemea ili wengine pia wasije wakarudia jambo kama hilo ambalo hakika ni la upuuzi kabisa. Kuendelea kumtetea Buswita na kuona anaonewa ni kuhalalisha jambo hili la kijinga na kutaka wengine waendelee wakiamini watatetewa kama ambavyo Buswita aliona Yanga wangeweza kulimaliza.

Ili kujiepusha kuonekana shetani wa Buswita anawahusu, viongozi wa Yanga na Simba, huenda hii ni nafasi ya kuonyesha ukomavu na ukongwe wao. Badala ya kuendelea kuzozana kwenye vyombo vya habari kama mashabiki, waende na uhalisia na kuachana na propaganda za kitoto na badala yake aliyekosea akubali, aliyekosewa akubali baada ya mazungumzo, walimalize hili.

Tunamhitaji Buswita bila ya upuuzi alioufanya. Tunakihitaji kipaji chake katika njia sahihi akiwa anajitambua. Akibadilika, mpeni nafasi. Akishindwa kuonyeshwa uungwana, achinjiwe baharini tuendelee kutafuta walio makini, wanaojitambua ili kupunguza wanaoendelea kuufanya mpira ni sehemu ya kubahatisha. 


1 COMMENTS:

  1. hii ni moja kati ya mada bora kabisa hongera sana kaka!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic