Ili kuhakikisha kama akirejea basi anakuwa fiti hasa, daktari wa Simba, Yassin Gembe amemuongezea wiki moja ya mapumziko beki wa pembeni wa timu hiyo, Shomari Kapombe kabla ya kurejea uwanjani kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake.
Kapombe aliyesajiliwa na Simba msimu huu akitokea Azam FC, hakufanikiwa kucheza mechi yoyote ya timu yake hiyo mpya baada ya kupata majeraha ya nyonga.
Beki huyo, alipata majeraha hayo ya nyonga akiwa kwenye kambi ya Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na mechi dhidi ya Rwanda katika mechi ya marudiano kufuzu Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).
Mratibu wa Simba, Abbas Ally alisema kwa mujibu wa ripoti ya daktari wao, Kapombe alitarajiwa kuanza mazoezi Jumatatu wiki hii, lakini ameongezewa wiki moja ya kupumzika.
Ally alisema, Kapombe anatarajiwa kuanza tena mazoezi ya pamoja na wenzake wiki ijayo akiwa fiti kwa ajili ya kuichezea Simba.
Alisema kurejea kwa beki huyo kutaimarisha kikosi hicho katika michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara ili kuhakikisha wanashinda.
“Kapombe amepona na yupo fiti kabisa kwa ajili ya mapambano na alitakiwa kuanza mazoezi Jumatatu ya wiki hii, lakini ameongezewa siku za mapumziko ili akirejea awe fiti zaidi,” alisema Ally.
0 COMMENTS:
Post a Comment