October 30, 2017




Na Saleh Ally
ZILE kelele za watani wa jadi Yanga na Simba zimemalizika na sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. 

Simba au Yanga, kawaida zingependa ushindi kila zinapokutana lakini unaweza kushangazwa na sare huufurahisha upande mmoja, hiyo lazima. Kama unakumbuka sare ya 3-3 baada ya Yanga kuongoza 3-0 hadi mapumziko.

Sare ya jana, imeifurahisha Yanga. Inaweza kukawa na mambo mengi lakini suala la timu yao kuonyesha kiwango safi huku ilikuwa ikionekana kama “haina kitu”, limewafurahisha na wana haki ya kufurahi.

Usisahau pia kabla ya mechi, gumzo walikuwa Ibrahim Ajibu na Emmanuel Okwi ambao walipotea kabisa na hakuna aliyeonyesha ni hatari.

Pamoja na kwamba Simba wako kileleni tena mwa Ligi Kuu Bara, lakini sare inaonekana kutowafurahisha na jambo baya zaidi, gumzo limekuwa katika fedha, Sh bilioni 1.3 zilizoelezwa kutumika katika usajili.

Hakuna anayeweza kusema kila kikosi ghali kilishinda au wingi wa fedha ndiyo ubora wa kikosi. Uchambuzi huo wa kishabiki ni sehemu ya furaha ya mashabiki unaweza kuuacha.



Mimi ninaangalia mchezo huo kwa mtazamo tofauti kabisa kwa kuwa niliamua kutulia kuona kila nilichotaka kuona katika mechi hiyo ya watani baada ya kelele nyingi.

Wako walioziangusha timu zao na wako waliofanya vizuri kwa faida kutokana na ubora na ungeweza kusikia mashabiki wakiendelea kuwalaumu bila ya kuwa na tathmini ya kutosha.

Ajibu:
Ibrahim Ajibu, amekuwa na faida nayo ni moja tu. Yeye ndiye alianzisha shambulizi la bao la kusawazisha, akapeleka pembeni ambako ilipigwa krosi iliyozaa bao lililofungwa na Obrey Chirwa baada ya beki Juuko Murshid kubaki amezubaa.


Ukiachana na hivyo, Ajibu hakuwa na faida kubwa kwa Yanga. Zaidi alionyesha “utoto”, alitaka kupiga chenga na huenda kuwaonyesha Simba. Mashabiki hawawezi kulaumu kwa kuwa ni kipenzi chao kwa sasa, lakini anapaswa kujirekebisha.


Kotei:
Ukiwasikia mashabiki wa Simba, wengi wanalaumu kwa nini alianza lakini ndiye alifanya kazi nzuri ya kuzuia na kupiga mipira mirefu lakini huyu ndiye alichangia Ajibu afanye shoo zaidi. Kwani alimbana kwa kila namna, naye akataka kuonyesha badala ya kuingia katika malengo ya jumla la kikosi ambayo ni ushindi. Utaona mabadiliko ya Mkude yalionekana ni mazuri.

Yondani:
Kelvin Yondani ni beki asiyechuja ingawa watu hawataki kulikubali hilo. Yondani aliamua kumuacha mgongoni kwake Andrew Vicent akafanya kazi ya kuhakikisha Emmanuel Okwi anapumua kwa shida katika dakika 90 na kweli alifanikiwa kuhakikisha hapigi hata shuti moja lililolenga lango.

Tshishimbi:
Raia wa DR Congo, Papy Tshishimbi ndiye alikuwa dereva wa kusukuma mashambulizi na mkata umeme wa mashambulizi ya Simba.

Alishambulia na unaweza kuona tofauti yake ya kutaka ushindi. Alikuwa ‘siriaz’ hasa, kwa kuwa alikimbia kusukuma mashambulizi kwa kasi na ndiye alikuwa “hub” au kianzishi cha ‘counter attack’ zote walizofanya Yanga.

Kocha George Lwandamina alimtumia Tshishimbi kama “jicho la timu”, wanaposhambulia au kushambuliwa na kazi hiyo aliifanya hasa kuonyesha hakuwa akitaka mzaha na alifanikiwa.
 

Buswita/Daud:
Baada ya kupata uhakika hatampata Thabani Kamusoko, Kocha George Lwandamina aliamua kuua winga moja na kutengeneza pacha ya kupambana na kiungo cha Simba akiwatumia Raphael Daud na Pius Buswita ambao pia walichangia kumpa wakati mgumu Kotei kwa kuwa walicheza upande wake katika kiungo.

Kikubwa ambacho inaonekana walifundishwa kutopoteza mipira hovyo na walipozidiwa, walitakiwa kurudisha mara moja nyuma ili kuanza upya.


Mwashiuya:
Mara tatu au nne alionyesha yuko vizuri na kujaribu mashuti makali, alipiga krosi “dongo” za maana na kitu kizuri zaidi, hakuonyesha uoga wa mechi au namna ya kumkabili beki mkongwe kama Erasto Nyoni.

Huenda mfumo pia ulimbana kwa kuwa alilazimika kucheza katikati wakati mwingine kusaidia kuzuia kiungo cha Simba lakini kama angebaki pembeni hadi mwisho huenda Simba wasingemsahau.


Manula:
Kipa Aishi Manula amekuwa nyota wa mchezo, ameonyesha ni mtu anayeweza kuyafanyia marekebisho makosa yake. Kusema ameisaidia Simba ni sahihi kwa kuwa hiyo ndiyo kazi yake kuhakikisha haifungwi lakini hakuna ambaye atamsahau katika “ana kwa ana” na Emmanuel Martin ambaye unaweza kumlaumu hakufunga lakini haukuona timing na Manula kuwa ilichangia Martin kushindwa kutimiza alichotaka.

Angalia shuti maridadi ambalo ndiyo lilikuwa hatari zaidi katika mechi hiyo, aliweza kuliona na kufuta yale makosa ya mechi zilizopita.
 
Manula kuwa nyota wa mchezo, maana yake Simba ilishambuliwa zaidi na hilo Simba wanapaswa kukubali na kujipima upya.

Mavugo:
Laudit Mavugo alipewa nafasi ya kuanza, kashindwa kuitumia mara nyingine na alionekana ana papara. Awali, Simba walipaswa kuanza na John Bocco, inawezekana Omog akaamua kubadili mawazo lakini Mrudi huyo alifeli.

Omog:
Timu yake aliipanga vizuri, ilicheza vizuri kwa maana ya kutafuta nafasi, ilifeli katika direct football, hakukuwa na malengo katika pasi nyingi na haikucheza kulazimisha kupata ushindi na badala yake ilibaki na mpira muda mwingi bila faida.
Hilo hakuliona na kulifanyia kazi, bado, timu ilipanda yote, ikapigwa counter attack, hakukumbusha kosa hilo kila mara.

Hakuwa mwepesi katika mabadiliko sahihi kama kumtoa Mavugo mapema zaidi au kumpumzisha Muzamiru Yassin mapema, maana kipindi cha pili alipotea mapema zaidi.
  

Lwandamina:
George Lwandamina ni mzuri katika kusoma mchezo. Utaona Yanga walicheza kimfumo na inaonekana walifundishwa jambo hasa wakitumia counter attack. Mashambulizi yao yalikuwa na nguvu nyingi licha ya kwamba hawakukaa na mpira sana.


Pia ilionekana sare ilimtosha kwa kuwa alitaka kushambulia kwa kushitukiza zaidi. Angalia sub yake ya kumuingiza Pato Ngonyani ili kuongeza ulinzi mwishoni, akafanikiwa na bado alishambulia kwa kasi. Alimuingiza Martin akimtoa Mwashiuya, naye akafanikiwa. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic