November 15, 2017




Na Saleh Ally
KAULI ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe kuhusiana na beki Shomari Kapombe imeonekana kuwakera watu wengi sana.


Hasa mashabiki wa Simba, wameonekana kulaumu kuhusiana na kauli hiyo ya Hans Poppe ambaye amesema bila breki wala kona, kwamba kama Kapombe ataendelea kutocheza kwa kuwa ni majeruhi, basi aende zake.


Hans Poppe amesema moja kwa moja kwamba hawawezi kuendelea kumlipa Kapombe wakati akiendelea kuwa nje na huenda anaonekana kuwa hana furaha na kinachoendelea, kwani Kapombe tangu asajiliwe akitokea Azam FC ameendelea kubaki benchi.

Awali, ilielezwa wiki mbili, ikaongezwa ikawa wiki sita nyingine na hadi sasa baada ya Simba kucheza mechi 9, Kapombe ameendelea kuwa benchi akijitibu kwa lengo la kupona ili arejee uwanjani akiwa vizuri.

Kapombe alitoa majibu yake ikiwa ni pamoja na kusema kwamba hawezi kucheza akiwa majeruhi na kama Simba wanaona wanataka wavunje mkataba wake, basi hana tatizo.

Kuna mtu mwingine kasema, Kapombe hajajibu hivyo na si kweli lakini kuna kituo cha redio kina sauti yake akijibu kuhusiana na suala hilo.

Yote yanaweza yakawa yamepita, mijadala imeanza na ninaona wengi waliokuwa wakijadili wamekwenda katika suala la ubinadamu na kauli kali ya Hans Poppe.


Kwamba hakuonyesha ubinadamu kwa kuwa Kapombe ni majeruhi na alipaswa kusubiri hadi apone badala ya kufanya au kusema alichokizungumza.

Kuhusiana na kauli; kwamba haikupaswa kuwa hadharani. Badala yake Hans Poppe, angeweza kumfuata Kapombe na kuzungumza naye wakiwa pamoja ili kujua tatizo na kwenda katika vyombo vya habari.

Yote mawili ni hoja ya msingi, lakini mimi najaribu kuangalia tofauti na wengine na huenda baada ya Hans Poppe kuzungumza vile; nimepata nafasi ya kujifunza jambo na huenda tunaweza kujifunza.

Nionavyo ni hivi; Hans Poppe ana haki kabisa ya kuona alivyoona. Kama mwajiri, mtu anayehusika na kufanya ubunifu wa kuona Simba inaingiza kiasi gani cha fedha, kuona wachezaji wanalipwa kwa wakati mishahara na posho zao kama ilivyo kwa makocha na wafanyakazi wengine, atakuwa anafikiria tofauti sana na mimi na wewe.


Hans Poppe anakuwa kama mwajiri ambaye anamlipa mfanyakazi fedha na hatumikii kinacholipwa. Bila shaka kwa waliowahi kuajiri watu watanielewa. Na kama haujawahi kuwa na kampuni, mfano mzuri ni wewe kuwa na dada wa nyumbani ambaye tokea amefika kwako ni mwezi wa tatu au nne, hajawahi kufanya kazi kwa kuwa anaumwa na sasa unamhudumia.

Nimetoa mfano huo wa dada wa kazi kwa kuwa naamini asilimia zaidi ya 70 watakuwa na wasaidizi wa kazi nyumbani maarufu kama “Dada wa Nyumbani” na itakuwa rahisi kunielewa.

Kama wewe utaona analipwa bila kazi, Hans Poppe anaweza akaona hivyo kwa Kapombe na hasa anapofikiria upatikanaji wa fedha za uendeshaji wa klabu na tukubaliane, lazima kuna ugumu wake hata kama kuna wadhamini.

Lakini utagundua kuna makosa mawili katika uwasilishaji wa jambo hilo. Moja ni kwa Hans Poppe mwenyewe na pili kwa Klabu ya Simba na hili linaweza kuzigusa klabu nyingine nyingi.

 MOJA:
Hans Poppe yuko sahihi, lakini alishindwa vipi kuzungumza na Kapombe kwa kuwa ni mchezaji wake? Kama inaonekana ameshindwa kurejea uwanjani na Simba inaona hasara, basi katika mkataba kuna vipengele vya kuvunja au kufanya njia mbalimbali kuhakikisha mambo yanakwenda sahihi.

 Kumsema mbele ya hadhara utafikiri Kapombe anafanya hivyo kwa makusudi, haikuwa sahihi na kama kuna jambo la ziada lililofichika, basi Hans Poppe angeliweka hadharani ili kukamilisha alichokisema hasa kama kuna zaidi.

PILI:
Jiulize, kama Kapombe leo ameshindwa kucheza tokea asajiliwe na kama unakumbuka akiwa Azam FC pia alikuwa majeruhi, vipi kamati ya Hans Poppe ilikubali kumsajili?


Ilikubali kumsajili kishabiki? Hapa ndilo lile somo nililosema litazihusu na klabu nyingine kwamba wakati wa usajili, suala la vipimo ni muhimu sana. Tumeona hata klabu kama ile ya AFC ilimsajili Mtanzania Thomas Ulimwengu bila ya kumfanyia vipimo, leo inahangaika na inaonekana kuwa alikuwa majeruhi kwa muda mrefu hata akiwa TP Mazembe.

Lakini nchi nyingi za Ulaya na kwingine mpira ulipopiga hatua, suala la uhakika wa vipimo vya afya ya mchezaji kabla ya kumsajili ni muhimu sana. Hivyo kamati ya Hans Poppe inapaswa kuwajibika katika hili na kujifunza kufanya mambo kisayansi zaidi.

Kapombe hakuingia Simba kwa mlango wa uani, alipita sebuleni wote wakimuona. Na kama ni tatizo la afya mapema, wanawajibika wao lakini kama wanaamini ni bahati mbaya, iko haja ya kufuata utaratibu sahihi na ikiwezekana bila ya kukwazana.



2 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic