November 24, 2017




NA SALEH ALLY
HARAKA kabisa nianze na kukuuliza kwamba hata kama ni shabiki maarufu sana wa Yanga, unaamini beki Vincent Bossou ndiye bora zaidi ambaye Yanga inamuhitaji?

Nikuulize tena, unafikiri kama Yanga inatafuta suluhisho katika ulinzi wake, Bossou anaweza kuwa suluhisho sahihi kabisa na Yanga itakuwa imemaliza matatizo yake yote?

Swali la mwisho kabla sijaendelea? Hivi ni kweli hapa nyumbani Tanzania, hakuna beki mwenye kiwango si sawa, nauliza zaidi ya huyo Bossou?

Uongozi wa Yanga umekuwa ukificha kuhusiana na suala la kurejea nchini kwa beki huyo, Vincent Bossou ambaye alikuwa hapa Tanzania lakini mwisho aliondoka baada ya kutaka aongezewe dau na Yanga wakaona hawakuwa na kiwango hicho, akaondoka.

Tokea ameondoka, Yanga imecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara, imefungwa mabao manne sawa na Mtibwa Sugar na Singida United. Hii inaifanya Yanga kuwa ya pili kwa ubora katika kuruhusu nyavu zake kutikiswa baada ya Azam FC ambayo imefungwa mabao mawili tu.

Hapa unaweza kujiuliza kwamba Bossou anahitajika kwa ajili ya nini? Kama ni jibu la kimataifa, kweli Yanga haina walinzi wa kucheza mechi za kimataifa hadi Bossou?

Binafsi naona kama kuna mchezo ambao sio sahihi wa kutaka kuwasajili wachezaji wanaojulikana kwa ajili ya kupata kiasi fulani na huu unaweza ukawa unafanywa na mawakala ambao wanaizunguka Yanga.

Wako watu wengi ambao wamekuwa wakitumia maneno kama “Yanga yetu” na kadhalika wakitaka kuonyesha wana mapenzi makubwa sana na klabu hizo hasa zile kubwa kumbe wamekuwa wakifaidika binafsi.

Wakati wa usajili kumekuwa na migogoro mingi sana ndani ya klabu ingawa mambo yamekuwa yakiisha chinichini lakini ukweli ni kwamba mgawo umekuwa chanzo cha matatizo hayo na hasa kwa mawakala ambao wanakuwa tayari kutoa au kuchukua kiasi fulani.

Yanga inapaswa kujipima na kuangalia kuwa kuna nafasi ya kuwapata walinzi bora zaidi ambao wanaweza kuwa na kiwango bora na kuisaidia timu hiyo.

Bado Yanga wanaweza pia kumpa moyo nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alionekana kuvunjwa nguvu baada ya kulazimishwa “uzee” hasa baada ya mfarakano na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ambaye sasa ni katibu mkuu wa Yanga.

Hivi karibuni nilizungumzia kuhusiana na ubora wa beki kama Yusuf Mlipili wa Simba dhidi ya Juuko Murshid ambaye kwangu namuona ana uwezo lakini kiwango anachoonyesha kinaweza kufanana na mabeki wengi wa hapa nchini kama huyo Mlipili.

Tanzania ina vipaji vya kutosha, kuna shida ya kuaminika wazawa na tatizo kubwa la kuamini kila mgeni lazima atakuwa na uwezo mkubwa sana.

Cannavaro amecheza mechi nyingi za kimataifa kuliko Bossou, lakini niwakumbushe kwamba Yanga inahitaji beki bora na kijana na si mwenye umri wa Bossou kwa kuwa tayari ina Cannavaro na Kelvin Yondani.

Lakini najiuliza hofu ya kupindukia kwa Andrew Vincent ‘Dante’, kwamba ana makosa mengi. Kama difensi yake inaonekana kuwa imara na yeye ndiye amekuwa akicheza karibu mechi zote akiwa na Yondani au Cannavaro na Yanga imefungwa mabao machache, shida nini.

Kama Dante ataanza kukaa benchi ni kumdidimiza na kumrudisha nyuma tena. Wakati sasa ni wakati mzuri wa kurekebisha makosa hayo machache ili azidi kuwa bora zaidi na kuendelea kufanya vizuri hadi atakapokuwa zaidi ya tegemeo.

Siamini kama ujio wa Bossou utakuwa ni wa kiufundi pekee, badala yake naweka walakini kutokana na kiwango chake na uchezaji wake kwa kuwa kuna wengi ambao nawaona wana uwezo wa kufanya vizuri hata kuzidi yeye. Kama kweli kinachoelezwa,  iko haja ya Yanga kuongeza umakini na kuacha kusajili kwa kufuata ushabiki au kuangalia mambo fulani.

3 COMMENTS:

  1. Niajabu kumchukua huyu mtu, hata kama mzuri, lakini alitukimbia wakati wa dhiki yetu. Mtu gani wakutaka raha tu. Hakumbuki timu ilipomvumilia akikaa benchi kuinua kiwango chake. Tofauti ya Tshishimbi ambaye amefika na moja kwa moja kuingia first 11. Bossou anaweza kuisumbua, kwanza kilichomrudisha ni nini?

    ReplyDelete
  2. A friend in need is a friend indeed! Bossou YOU ARE NOT! Yanga "Always Forward"

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic