November 17, 2017


KARIA

NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na mjadala ambao ulianzia mitandaoni, huenda ulianzishwa na mtu aliyekuwa na jambo au aliamua kufanya hivyo kwa ajili ya kuridhisha nafsi yake.

Unapozungumzia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), unagusa maslahi ya watu wengi sana. Bado ninaamini kuna wengi hawakufurahishwa kuondoka kwa uongozi uliopita, hali inayowafanya kuanza kutengeneza mambo.

Lakini bado hatuna haja ya kumbeza sana muanzisha hoja kwa kuwa kuna mijadala aliyoanzisha ambayo inakuwa ni rahisi kama tutalenga kujadili kwa kujenga, basi kutakuwa na jambo jema.

TFF walikuwa wanataka kuuthibitishia umma kwamba wao ni wasafi, jambo ambalo naweza kuungana nao kwa kuwa hata ukisema kwa kipindi hiki wamefuja fedha tayari ni kuwaonea.

Sote tunajua, viongozi wengi wa TFF wameingia madarakani wakiwa na moto wa kuleta maendeleo. Kadiri siku zinavyosonga mbele, wamekuwa wanabadilika hadi mambo yalipokuwa mabaya na mwisho wakawa wakali na viburi na wasiotaka kukosolewa.

Kwa sasa, TFF wako katika kipindi cha mvuto. Ndiyo wanajaribu kuvuta mambo na kuyapeleka taratibu na kipindi hiki hautarajii kuona wanaharibu sana. Huenda tuna takribani miezi sita hadi mwaka wa kupima kama kweli watakwenda mwendo sahihi au nao watabadilika na kuwa kama waliopita.

WAMBURA

Wakati TFF na wadau wengine walikuwa katika mjadala wa ufujaji fedha wakiangalia viongozi wa TFF wanalipwa juu zaidi. Mimi nikaamua kutofautiana na wengi, badala ya rais na makamu wake kutolipwa mishahara na walipwe posho, naona wanastahili kulipwa.
Wallace Karia ambaye ni Rais wa TFF na Michael Wambura ambaye ni makamu wa rais wanapaswa kulipwa mishahara ili wawe watu wanaohusika kwa asilimia mia.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), ndiyo liliona utaratibu huo ni mzuri zaidi kwa marais na makamu wao au viongozi wa kuchaguliwa kulipwa posho tu na wale walioajiriwa ndiyo walipwe mishahara.
Wakati mwingine naona kama Fifa walitengeneza utaratibu ambao unaweza kufanya kazi vizuri zaidi Ulaya, Amerika na kidogo Asia na Amerika Kusini. Lakini kwa Afrika ukawa na walakini tena mkubwa.

Tunaweza kuendelea kuwabana viongozi hao wa juu pale linapotokea jambo na wao wakaona kama unawaonea kwa kuwa wanajitolea tu. Kwa hali ya kawaida utaona ni kama Karia na Wambura ndiyo wanaoisadia TFF.

Kwa mazingira ya Ulaya na kwingineko, nafasi za rais na makamu wake, zinagombewa na wafanyabiashara wakubwa ambao utawalipa kiasi gani kama utasema mishahara? Ni watu wanaotaka sifa ya mabadiliko kupitia walichojifunza katika biashara kupitia makampuni yao makubwa.

Fifa iliona hivyo kwa kuwa hata wagombea wa nafasi hizo wanakuwa ni watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha. Huku kwa Afrika mambo ni tofauti kidogo na hata kama ni wafanyabiashara basi ni wa kiwango cha kawaida kabisa.
Binafsi naangalia tofauti, kwamba kama ni mtu anayejitolea, basi hawezi kuweka nguvu zake asilimia mia na hata mambo yanapoharibika na kunakuwa na ugumu kuyakwamua naye hujisikia kama hahusiki kwa asilimia mia kwa kuwa si mwajiriwa.

Neno kujitolea, Ulaya na kwingineko lina maana kubwa sana lakini si hapa kwetu na tunakubaliana Karia na Wambura wamekulia katika utamaduni wa maisha yangu na wewe. Kujitolea kupo lakini kwa kiwango cha chini.

Tukubaliane wanaijitolea ni wachache. Kama Karia na Wambura watalipwa mishahara wataona wana deni na pale watakapodondoka wanaweza kubanwa zaidi kwa kuwa hawajitolei tena na badala yake ni wahusika wakuu wanaotakiwa kusaidia au kuleta maendeleo.

Kazi ya kujitolea na ile unayotakiwa kuifanya kwa ufasaha ukiwa mwajiriwa ni mambo mawili tofauti. Nimesikia Karia amekataa hadi posho, lakini ingekuwa ni utaratibu wa mishahara, angekubali tu.

Endeleeni kujadili kuwa wanalipwa fedha nyingi, mimi nasubiri mjadala huu pia. Kwamba walipwe ili wafanye kazi kwa moyo mmoja na wakishindwa tuwabane.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic