November 6, 2017



Na Saleh Ally
NILIWAHI kufunga safari hadi nchini Ujerumani ambako niliungana na vijana kadhaa wa Kitanzania ambao walipata mafunzo ya michezo hasa soka na elimu ya kawaida ikiwa ni pamoja na kujifunza Kijerumani.


Asilimia kubwa ya vijana waliokuwa Ujerumani katika mji mdogo ulio karibu na Mji wa Freiburg, Ujerumani sasa wanacheza Ligi Kuu Bara katika timu mbalimbali.


Mji wa Freiburg uko Kusini mwa nchi ya Ujerumani katika mipaka ya Ufaransa na Uswisi na wakati mwingine tuliendesha baiskeli kuingia nchini Ufaransa na kwenda kutalii katika miji ya karibu na mpaka ambako tulijifunza mengi.

Baadhi ya vijana waliokuwa huko ni pamoja na Frank Sekule, mara ya mwisho alikuwa Majimaji, Carlos Protus ambaye aliteremka daraja na Toto African (sasa iko daraja la kwanza), Rajab Rashid yuko Stand United, Said Ndemla ambaye yuko Simba na Mudathir Yahya ambaye sasa ndiye nahodha wa Singida United, timu inayoonekana kuwa tishio kutokana na kikosi chake kukamilika.


Tukiwa Ujerumani, Mudathir na Ndemla ndiyo walikuwa wachezaji wa kwanza kunishangaza. Wao waliomba waondoke Ujerumani na kurejea Tanzania na wakaeleza wazi kilichowakwaza ni mambo ya kuingia darasani wakati wanachotaka ni kucheza soka na si ziada.


 Kwa nyakati tofauti, alianza Ndemla ambaye alisisitiza angependa kurejea Tanzania na kuendelea kuichezea Simba ambayo alikuwa amepandishwa kikosi cha wakubwa. Halafu Mudathir naye akawa wazi kabisa kwa kusema hapendi kusoma, zaidi anafurahia kucheza soka ambako anaamini atatimiza ndoto zake. Mwisho aliondoka kurejea Tanzania kwenda kujiunga na timu ya vijana ya Azam FC.


Wahusika ambao ni Wajerumani walishangazwa sana na Ndemla na Mudathir na kuna mmoja wao alisema haamini kama wataendelea kisoka. Mimi ambaye nilishangazwa na ujasiri wao, nilimueleza Tanzania ni tofauti kama wana moyo wa kutaka kufanya vizuri, wanaweza kufanikiwa.



Nilitaka kujua kuhusiana na Ndemla na Mudathir. Kama walichofanya ni sahihi na kweli ni watu waliopania kutimiza ndoto zao. Kwa Ndemla sina hofu ila ninachoweza kusema kwa sasa hayuko katika sehemu sahihi.


Hakika anastahili kucheza na si kwa kiwango anachopata nafasi na mwenyewe mwisho ataamua apate nafasi Simba au aende kwingine akapate nafasi zaidi ya kucheza.

Upande wa Mudathir akiwa Azam FC pia hakuwa akipata nafasi ya kutosha ya kucheza. Kijana huyu anaonyesha wazi kuwa ana nia ya kufanya vizuri na amepania kufanya vizuri.

Kwa kawaida Mudathir si mzungumzaji sana, ukiwa haujamzoea unaweza kudhani ni mtu mwenye dharau lakini anaonyesha anaweza kufika mbali zaidi kwa kuwa ana hamu, amepania na anataka kutimiza ndoto yake.

Unaweza kujiuliza, kikosi cha Singida United kilichoshiba wachezaji wa kila aina kutoka nchi mbalimbali wakiwemo nyota wa nchi hizo yeye ni nahodha wao.

Aliyemuamini na kumpa unahodha ni mmoja wa makocha bora wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati au Afrika, Hans van Der Pluijm. Hili ni jambo zuri na vizuri wachezaji wengine wa umri wake au wanaochipukia wanaweza kujifunza kwake kwani si lazima kujifunza lazima mchezaji awe Yanga au Simba pekee.

Kama ulibahatika kushuhudia mechi ya Yanga dhidi ya Singida United waliokuwa wenyeji utagundua kuwa Mudathir alikuwa ndiye mchezaji aliyecheza vizuri zaidi katika kiungo.

Licha ya kupambana na kiungo mzuri kama Papy Tshishimbi lakini bado alichomoza na kuweza kung’ara zaidi akiichezesha timu inapokuwa inashambulia lakini alionekana anakaba zaidi inaposhambuliwa.

Unaweza kuona picha za Mudathir akiwakaba wachezaji mbalimbali wa Yanga kwa nyakati tofauti na hii inaonyesha alimkaba karibu kila mchezaji wa Yanga aliyekwenda kushambulia bila ya kujali ilikuwa ni upande upi wa uwanja. 

Bado Singida haifanyi vizuri sana lakini kupitia kikosi chake kinachoongozwa na kinda Mtanzania, Mudathir inaonyesha wazi kuwa ina nafasi ya kung’aa hapo baadaye na kufanya vizuri zaidi.

Lengo langu si kumvimbisha kichwa Mudathir, badala yake kuzidi kumchombeza kuendelea na mwenendo wake wa kutaka kutimiza mdoto zake kwa kuwa nimeona nguvu anayoitumia kufikia anachokitaka inaonekana na ikiwezekana anaweza kuongeza zaidi na kuifikia inavyotakiwa.

Ninaamini atarudi tena Ulaya, iwe Ujerumani au kwingine lakini safari akiwa mwanasoka na kuyashinda maneno ya yule rafiki yangu Mjerumani aliyeamini hawezi kufanikiwa baada ya kukataa kusoma na kusisitiza anachotaka ni soka na ndiko zilizo ndoto zake za mafanikio.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic