November 1, 2017



 Na Mwandishi Wetu
SHINDANO la Vipaji vya Sauti kwa mara nyingine limehitimishwa huku washiriki 25 wa mwisho wakichuana vikali na kupata washindi 10.

Washindi hao 10 wanapata nafasi ya kwenda nchini China ambako wataishi kwa mwaka mmoja wakifanya kazi ya kuingiza sauti wakiwa wamepewa mikataba.

Washiriki 25 walioshiriki shindano hilo ambalo huandaliwa na StarTimes wauzaji maarufu wa ving’amuzi kupitia kampuni yao kuu ya Star Media Ltd, walitoka katika maeneo matatu ya Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar.

Ushindani ulikuwa mkali hadi anapatikana mshindi na utaona wasanii wengine maarufu nchini kama Abdallah Makumbila ‘Muhogo Mchungu’ walijikuta wakiangukia pua kwa kuwa vijana walijiandaa hasa.

Ili kuwapata hao watano wa Zanzibar lilifanyika shindano lililoshirikisha zaidi ya washiriki 100 kama ilivyokuwa Mwanza. Lakini Dar es Salaam wakajitokeza takriban watu 400 kushindana ili kuwapata 15 walioingia katika fainali hiyo.

Kwa waliopata nafasi ya kuliona shindano hilo, hasa hatua ya fainali kwa kuwa lilirushwa moja kwa moja runingani, watakubaliana kwamba lilikuwa shindano lenye uwazi na kila kitu kilikwenda bila ya upendeleo au lawama.

StarTimes ambao kazi yao ni kuuza ving’amuzi, wanakuwa watu ambao wanaonyesha thamani kubwa hapa nchini, hasa kwa vijana wa Kitanzania.




Unaweza ukajiuliza, shindano lipi la sanaa ambalo limewahi kutoa zawadi ya kazi kwa washindi 10 ambao wanapelekwa kuishi nchini China? Na hii si mara ya kwanza!

Vijana wanapata ajira na sehemu ya kuishi nchini China, hili si jambo dogo na linapaswa kuungwa mkono sana na Serikali ya Tanzania inaweza kuungana nao katika jambo hili zuri kabisa.

Kitu cha pili ukiachana na ajira, utaona kuwa StarTimes wanachokipigania ni Kiswahili, hii ni lugha yetu ya taifa na unaona watu wanaoanzisha jambo fulani zuri kuipigania lugha hiyo. Ni kampuni ya Kichina ambayo huenda wangeweza kusema wana mpango wa kueneza Kichina zaidi.




Badala yake wanachofanya ni kusaidia Lugha ya Kiswahili kuenea zaidi na kuwa ya kimataifa zaidi kwa kuwa vijana hao watakaokwenda kuishi nchini China wakifanya kazi watakuwa wakifanya kazi ya kuingiza sauti katika filamu za Kichina na Kingereza ili zisikike Kiswahili.

Hili ni jambo jingine la jeshima kubwa katika lugha yetu ya Kiswahili, jambo ambalo huenda ungetegemea kuona runinga au wauza ving’amuzi ambao ni kampuni ya kizalendo wakifanya hivyo.

StarTimes wanaweza kuwa ni wafanyabiashara na tukawaangalia kwa jicho hilo. Lakini ni watu ambao wanaweza pia kuungwa mkono na kupewa kongole kwa kitu kinachoonyesha manufaa ya moja kwa moja kwa taifa letu.

Unajua kuishi China ambavyo mtu angelazimika kufanya kazi ya ziada tena akiwa na ajira ambayo inatambulika. Tunajua hata Wachina wenyewe nchini mwao, wako wasio na ajira kutokana na uhaba wa ajira.

Lakini vijana hao wa Kitanzania, wanakwenda China tayari wakiwa na ajira ya uhakika kwa mwaka mzima jambo ambalo hakika linaonyesha ushirikiano wa maendeleo ndani ya taifa letu.

Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa StarTimes ni kuhakikisha hawaishii njiani na ikiwezekana waongeze mikoa zaidi iwe zaidi ya Dar es Salaam, Mwanza na Zanzibar ili kuendelea kupata vipaji.

Serikali izidi kuwaunga mkono katika hilo ikiwezekana wazo jingine watakalokuwa nalo ambalo limelenga kusaidia vijana wetu wa Kitanzania, lipitishwe.


Lakini kwa wale walioshindwa kuingia katika 10 Bora wakati wa shindano hilo, niwape moyo, hakika wote wanaweza na walistahili kwenda lakini shindano lazima washindi wapatikane. Hivyo litakuwa jambo zuri kama wataendeleza vipaji vyao kwa njia nyingine ili wafikie ndoto au mafanikio yao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic