Na Saleh Ally
SI vibaya kusema kuwa tuna hadithi nyingi sana na kitu kibaya zimekuwa hazina mwisho. Mwendelezo wake pia haueleweki na si vibaya kusema pia hatueleweki.
Kuunda Tanzania maana yake kuna Tanganyika na Zanzibar inayoundwa na Unguja na Pemba na hakuna haja ya kuficha kwamba kuna ushindani wa mambo mengi baina yetu na inawezekana hawa hujiona bora na wengine hujiona bora zaidi.
Kinachotufanya tubaki pamoja ni muungano wetu na tuna bahati ya kuwa na wazee wenye busara na viongozi wanaoendelea kusisitiza muungano huo.
Leo ni siku ya Uhuru wa Tanzania Bara, miaka 56 sasa tangu Tanganyika sasa Tanzania Bara ilipopata uhuru wake. Ninaona ni nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo ikiwa ni siku moja baada ya Zanzibar kuitwanga Tanzania Bara kwa mabao 2-1 katika michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya.
Sina sababu ya kusema Zanzibar wametibua furaha ya uhuru kama ipo, lakini ninachoangalia ni uhalisia wa mambo ambao umezua mjadala mkubwa huku kila upande ukiwa na msimamo tofauti.
Hapa unakuja katika suala la timu ya taifa, Taifa Stars ambayo hujumuisha Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ndiyo Tanzania. Kwamba imekuwa ikiundwa na wachezaji wengi zaidi kutoka Tanzania Bara.
Wakati zinapokutana timu hizo zikiwa zimegawanyika mara mbili, Tanzania Bara wamekuwa wanyonge wakitandikwa karibu kila mara.
Umeona mechi ya juzi, Zanzibar Heroes wametokea nyuma kwa bao 1-0 hadi kushinda 2-1. Hii inamaanisha mijadala takribani 50 yenye msingi na isiyo na msingi.
Nikigusa baadhi ile ambayo naona ina msingi; ni suala la ubora wa Tanzania Bara dhidi ya Zanzibar, idadi kubwa ya wachezaji wa Bara dhidi ya Zanzibar katika Taifa Stars na Zanzibar walio na ligi dhaifu halafu wakawa na timu bora.
UBORA;
Kama kweli wachezaji wa Tanzania Bara wanawazidi wale wa Zanzibar, vipi wanakuwa wanashindwa kuwafunga na sisi tunataka kutumia kigezo cha kisingizio cha katika soka lolote linatokea! Jiulize mara ngapi au hadi lini?
Uliangalia ile mechi, Bara walizidiwa, visiwani walionyesha soka bora zaidi. Kama kweli tunawazidi vipi ilikuwa hivyo na imekuwa ikiendelea? Iko haja ya kutafakari hili.
IDADI:
Wachezaji wa Bara wamekuwa wengi katika kikosi cha Taifa Stars na mafanikio yamekuwa duni. Je, umefika wakati wa kuipa Zanzibar nafasi kubwa zaidi ili kujaribu angalau kidogo?
Maana wale wa Bara ambao ni nyota hawafanyi vizuri na wale wa Zanzibar wanaotokea katika ligi dhaifu ambacho kimekuwa ni kipimo, wanafanya vizuri.
Wako baadhi ya wanaotokea Zanzibar wanaporejea katika timu yao ya taifa wanafanya vizuri kuliko wale wa Bara. Tena unajiuliza kama Ligi Kuu Bara inawafanya kuwa bora, vipi wale wa Bara wenyewe hawawafikii hao wanaotokea kwa “ndugu” zao!
Hapa pia kuna haja ya kuwaangalia wachezaji wa Zanzibar kwa jicho la pili na ikiwezekana kuwapa nafasi kuona kama kuna mabadiliko au la.
LIGI DHAIFU:
Huenda hiki ni kipimo pekee kimekuwa kikitumika dhidi ya Zanzibar kwamba wana ligi dhaifu hawawezi kushinda dhidi ya Bara yenye ligi ngumu.
Au hawawezi kufanya vizuri wakiwa na Stars kwa kuwa ligi yao ni dhaifu lakini wakiwa na Zanzibar Heroes wanawanyanyasa haohao wanaotokea katika ligi ngumu.
Kunaweza kuwa na mambo mengi sana, lakini huu ni wakati mzuri kabisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuanza kuiangalia Zanzibar tofauti na ikiwezekana pale kwenye upungufu wapafanyie kazi ili kuwaimarisha huenda kizazi chao cha soka kikawa na msaada kwa Tanzania hapo baadaye.
TFF ni ya Tanzania, maana yake Zanzibar ipo ndani. Wao Zanzibar wamekuwa wakiendelea kutaka uanachana wa Caf na ikiwezekana Fifa. Kabla hawajapata lazima tukubali wao ni Tanzania na TFF inatakiwa iwape huduma sawa na inazotoa Bara.
Zanzibar kuikomboa Tanzania si jambo baya maana Bara tumeitumia kitambo na hakuna mabadiliko au nafuu ipo isiyo na nafasi kubwa. Hivyo tunaweza kujifunza kwa kukubali kujaribu na ikiwezekana tuone siku moja Taifa Stars yenye wachezaji wengi kutoka Zanzibar kama itakuwa na msaada.
Shida moja ya Zanzibar, viongozi wao wa soka ni watu wanaolalamika sana bila ya kuwa na mipango mathubuti ya kuusaidia mpira wao. Huenda kama wataacha hivyo, kunaweza kuwa na mabadiliko makubwa sana kwa kuwa sote tunakubali Zanzibar kuna vipaji kwelikweli, tatizo ni miundombinu, udhamini na msukumo sahihi kwenda katika mafanikio. Hii ni kazi ya viongozi na Serikali ya Zanzibar kwanza.
Kingine, tujifunze. Kwamba wachezaji wa Zanzibar, huwa wakisafiri kwenda katika michuano ya Chalenji kwa mwendo wa kuungaunga, lakini wanajitahidi na kufanya vizuri hata kuliko Kilimanjaro Stars ambayo wana kila kitu.
Wanafanikiwa kwa kuwa huwa wana nia ya kushinda, wanajituma vilivyo na hauwezi kusema eti huwa wanaifunga Taifa Stars tu, angalia wameitwanga Rwanda kwa mabao 3-1 ikiwa ina matunzo bora kabisa. Hivyo, wachezaji wa Bara nanyi achene ubishoo!
KUNA KITU CHA KUJIFUNZA:..
ReplyDeleteNilisafiri na Mzanzibar mmoja kwenye basi naelekea Dodoma. Yeye aliniambia wao wana mfumo wao wa uchezaji (Falsafa). Basi hiki ndio kitu pekee ambacho tunakikosa watu wa bara. Sitaki kuwalaumu sana wachezaji ila tumekosa misingi imara ya mpira wa miguu.
Lazima tukubali endapo kuna timu ina kombineshini nzuri inaweza kuchukuliwa na kujaribu kuziba mianya inayotakiwa ili kufanikisha timu yetu. Watanzania tumekaa sana ki-Uyanga na Usimba. Nenda kwenye Vibanda Umiza ndio utajua hiyo tabia.
Nikwambie kitu....kwa mpira wa Tanzania huwezi kumchukua mchezaji anaechezea Kenya alafu umuunganishe na mchezaji anaechezea Majimaji...umuanganishe na Mchezaji anaechezea Singida..utanidanganya. Sisi hatuna Falsafa ya mpira inayoweza kumsaidia mchezaji yoyote wa Tanzania hata akienda Ulaya akirudi atajua sisi tunachezaje?. Angalia Wazanzibar...wao wana mpira wao..hata leo mchezaji akienda Ulaya lakini akirudi Zanzibar atajua anachezaje.
Wachezaji wamekosa morali ya kiuchezaji hata kama wanapata mamilioni na kulala Hotel kubwa. Nimshauri Ninje...akae achague wachezaji yeye mwenyewe na si kujaziwa wachezaji wasio na morali kwenye mapigano. Mi naamini kwa kuwa kikosi cha Olympic kimeshataja angeweza kuwaita wale waende wakapambane na si hawa ambao wamepoteza mvuto.
Pia nahisi kama tulienda kufanyia majaribio wachezaji ndio maana unaona ni wachezaji watatu tu wamecheza mwanzo mwisho mechi zote ambao ni Kennedy Juma, Aishi Manula na Erasto Nyoni. Kitathimini inaonesha hatukwenda kushindana ila tumekwenda kujaribu.
Tumetengeza neno "Poor"
i) Performance
ii) Efficiency
iii) Effectiveness
Ndio maneno rahisi ninayoweza kusema.
PENDEKEZO:
Siku zijazo tuangalie wachezaji wa kuwaita. Tusiseme kishabiki...ila alivyoumia Yondani tulikosa mbadala, Kichuya angeumia tungekosa mbadala.Labda nikwambie..makocha wapo na timu kutengeneza CV na si kuisaidia timu ndio maana wamewaita Viungo wakabaji wengi ambao wataweza kusaidia kulinda kuliko kushambulia.
JIFUNZO:
Dawa ya kuzuia ni kushambulia kwa nguvu na si kuweka viungo wengi kama walivyofanya makocha wa timu yetu. Ndicho anachofanya Mayanga na kaambukiza hadi timu aliyoenda nayo Ninje. Angalia mechi tuliyocheza sijui Gabon au Benin ya mwisho...alimfanya Himid Mao kama Fullback ya kulia, sita akamuweka huyu Abdallah Hamisi shida ilikuwa ni kulinda. Kwani hatuna Fullbacks Tanzania?
Tuanhitaji kocha mtaalamu hasa aliye na uzoefu.Simkubali Mayanga wala Kinje ambao naona hawana jipya
ReplyDeleteShida kubwa wachezaji hawana morali, ile hali ya kusafiri kila siku wao wanaona kawaida tu. Uchungu wa kufungwa wenzetu hawana kabisa na awajui kabisa ni kiasi gani mashabiki huku wanaumia namna gani
ReplyDeleteMuda umefika Zanzibar vijana wao kupewa nafasi zaidi kwenye timu ya Taifa Stars hata kwa trials zifanyike pale tumu zinapo chaguliwa maana kwa sasa kigezo ligi mbovu ya visiwani.