Na Saleh Ally aliyekuwa Ujerumani
KLABU nyingi za soka hasa zile kutoka katika nchi ambazo mchezo wa soka umepiga hatua zimekuwa zikitumia “mascot” kama sehemu ya uwakilishi wake.
Mascot kinaweza kuwa kitu chochote, mfano sanamu ambalo lina aina ya ndege, mnyama au binadamu lakini ambalo litakuwa linachukuliwa kama mwakilishi.
Mwakilishi huyo anaweza kuwa mnyama au jambo fulani linalohusiana na timu husika kama ambavyo baadhi ya timu zinawakilishwa na ndege mfano wa kuku, tai au zile zinazowakilishwa na wanyama kama Simba na wengineo.
Katika Ligi Kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga, kila timu kati ya 18 zinazoshiriki ligi hiyo zina mwakilishi wake mfano wa “mascot”, lakini timu mbili zinatumia “mascot” hai.
Timu ya kwanza na Eintracht Frankfurt wanayemtumia tai hai kama mascot wao na FC Koln wanaowakilishwa na mnyama aina ya mbuzi kama mwakilishi wao.
Lengo la mascot ni uwakilishi wa kundi la watu na katika nchi za Ulaya Mascot amekuwa akipewa heshima kubwa kwa kuwa anaonekana ni mwakilishi namba moja wa klabu au timu.
Utaona kuna baadhi ya makocha, wachezaji na wakati mwingine hata viongozi waliwahi kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Lakini mascot anaendelea kubaki mwakilishi namba moja wa klabu.
Inawezekana aliyekuwa akifanya kazi hiyo ya mascot akaondoka kutokana na jambo lolote lile. Lakini anayefuatia hutakiwa kuvaa sanamu hilo na kuendelea na shughuli ya uwakilishi wa timu.
SALEHJEMBE ilifika kwenye Uwanja wa RheinEnergie, unaomilikiwa na FC Koln katika Jiji la Koln nchini Ujerumani na kushuhudia moja ya mechi za Bundesliga wakati timu hiyo ikiwavaa wageni wake Hertha Berlin na mwisho ikapoteza kwa mabao 2-0.
Pamoja na kupoteza mechi hiyo kwa kufungwa kwa mabao hayo 2-0, bado mashabiki waliendelea kuishangilia timu yao kwa nguvu, huku mbuzi ambaye si sanamu, mnyama hai aliyekuwa pale uwanjani akishangiliwa kwa juhudi kubwa.
Mashabiki walionekana kuonyesha mapenzi makubwa na mbuzi huyo ambaye alikuwa na mwangalizi wake na nilielezwa hufika uwanjani hapo kila mechi ya FC Koln ili kushuhudia mechi au kujumuika na anaowawakilisha.
Mbuzi huyo hutokea katika kila mechi ya FC Koln na kuwekwa pembeni ya mstari wa uwanja kama mshangiliaji namba moja wa kikosi kwa kuwa hata nembo ya klabu hiyo ina mbuzi.
Mashabiki wamekuwa wakimshangilia kwa nguvu sana kila anapokuwa uwanjani hapo kuonyesha wanamuunga mkono.
Historia inaonyesha mbuzi Hennes, ilianzia mwaka 1950 wakati mmoja wa mabosi wa mji huo alipotoa zawadi ya mbuzi kwa klabu hiyo kama zawadi ya kuwatakia kila la heri. Wakati huo Kocha wa FC Koln alikuwa ni Hennes Weisweiller ambaye aliamua kumchukua mbuzi huyo na kumlea.
Aliamua kuwa anakwenda naye uwanjani kwa kuwa ni sehemu ya timu alikuwa anakwenda naye mazoezini na urafiki wa mbuzi huo na mashabiki ukaendelea kuanzia hapo.
MASCOT WA MAN UNITED |
Baada ya hapo, urafiki ulizidi kukua na baada ya hapo wakamtunga jina “Mbuzi wetu ni bingwa”. Na Mwaka 1978, FC Koln ilitwaa ubingwa na baada ya hapo wakapitisha mbuzi huyo kuwekwa katika nembo ya klabu kwa kuwa aliungana nao kushangilia katika mechi zote za ligi.
Unaweza kujiuliza, Hennes yuko tangu mwaka 1950 hadi sasa, jibu ni hapana? Anapozeeka mbuzi’ au kupoteza maisha wanachagua kati ya watoto wake na mmoja wake anaanza kutumika katika nafasi yake kinachofanyika ni kuongeza namba, mfano Hennes II, Hennes III, Hennes IV na kuendelea.
MASCOT WA ARSENAL |
Kuanzia Agosti 3, 2008, FC Koln wamekuwa wakimtumia Hennes VIII. Maisha yake nayo ni kistaa kwa kuwa anaishi katika sehemu maalum katika zoo (sehemu ya kuhifadhia wanyama) akiwa ametengenezewa sehemu nzuri ikiwemo ile ya kupumzikia. Huchanganywa na mbuzi wengine mara chache.
Kinachovutia kuonyesha kweli mbuzi huyo ni staa na nembo ya klabu, amefunguliwa hadi ukurasa wake wa Facebook na mashabiki wamekuwa wakimtumia salamu au kuwasiliana naye kupitia mtu maalum ambaye hujibu maswali yao.
MASCOT WA DORTMUND |
Wakati mwingine, kupitia ustaa wake, Hennes VIII amekuwa akipata nafasi ya kufanya matangazo ya biashara na kuiingizia klabu hiyo kibunda cha fedha.
Kwa sasa FC Koln iko katika wakati mgumu sana na wakati wowote inaweza kuteremka daraja lakini timu hiyo ni ya kitamaduni.
Jiji la Koln ni la nne kwa ukubwa nchini Ujerumani pia ni kati ya miji ya starehe sana kutokana na kuwa na vyuo vingi na wanafunzi wengi.
MASCOT WA CHELSEA |
Pamoja na hivyo kiutamaduni wakazi asilia wa Koln si watu wa kugeukageuka. Hivyo msimamo wao wa kuipenda timu yao uko kwa kiwango cha juu bila ya kujali inacheza na nani au katika daraja lipi.
Hivyo, hata inapoteremka na kucheza Ligi Daraja la Kwanza badala ya ligi kuu yaani Bundesliga, sapoti yao huendelea kuwa kubwa kwa kiwango cha juu.
0 COMMENTS:
Post a Comment