Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, ameibuka na kusema kuwa, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, msimu huu wanacheza kwa kubahatisha kwani hawana kiwango chochote.
Bwire ametoa kauli hiyo baada ya wikiendi iliyopita timu yake kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Bwire amesema katika mchezo huo wao ndiyo waliokuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi, lakini kutokana na Yanga kupata bahati, wakaondoka na ushindi.
“Yanga hii si timu ya kutisha kabisa, tumecheza nayo na imepata ushindi wa kubahatisha, lakini wanajisifia kwamba wana timu nzuri.
“Niseme tu kwamba kufungwa kwetu na Yanga haimaanishi kwamba tutatetereka, bali tunajipanga kuhakikisha tunalipiza kisasi mzunguko wa pili ukianza.
“Katika kulipiza kisasi huko, tutaanza na Simba ambayo ilitufunga mabao saba katika mzunguko wa kwanza kipigo ambacho mpaka leo hii kinatuumiza, hatutakuwa tayari kuona tunaumia mara ya pili kiasi hicho,” alisema Bwire.
Ruvu Shooting kwa sasa inaburuza mkia wa ligi hiyo ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi 14 na kushinda mbili, ikitoka sare tano na kufungwa saba. Imefunga mabao saba, huku ikiruhusu kufungwa mabao 19.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment