Baada ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kuchelewa kujiunga na kikosi hicho, mwenyewe ameomba msamaha na kuahidi kuifanya kazi yake kwa nguvu moja ili kuisaidia timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Okwi ambaye awali alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya enka, alienda kwao Uganda kutibiwa, lakini ilielezwa kuwa licha ya kupona, alikawia kurejea jambo ambalo limewaudhi Wanasimba wengi.
Mganda huyo kabla ya mechi ya jana Alhamisi dhidi ya Singida United, mara ya mwisho kuitumikia timu hiyo ilikuwa ni Novemba 5, mwaka jana kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi Mbeya City ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumzia juu ya suala hilo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma, alisema Okwi baada ya kurejea ameomba msamaha kwa kilichotokea, hivyo hivi sasa kilichobaki ni kuwa kitu kimoja katika kuipambania timu.
“Alikuja akaomba msamaha kwa watu wote kutokana na kuchelewa kwake, unajua binadamu hakuna aliyekamilika, nikiwa kama mwalimu wa timu, mtu akishaomba msamaha unamsamehe kisha unampa nafasi ya kujirekebisha kwa kile alichokifanya.
“Kikubwa kaahidi kwamba hawezi kurudia tena makosa, hivyo nawaomba Wanasimba wote wamuelewe na waunganishe nguvu katika kuwania kile tunachokihitaji msimu huu ambacho ni ubingwa,” alisema Djuma.
0 COMMENTS:
Post a Comment