NA SALEH ALLY
KUANZIA jana mapema kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na suala la mshahara wa Kocha mpya wa Simba, Pierre Georges Lechantre.
Taarifa nilizozipata kwamba mshahara wake “ulivuja” na gazeti moja (si Championi wala Spoti Xtra), likaandika kwamba kocha huyo kila dakika analipwa Sh 42,000!
Kwa hasebu za kawaida kabisa ambazo hazitaki hata kuumiza kichwa, lazima kwa kocha huyo utaanza kumpigia kuzikuza kwenda kuutafuta mwezi.
Kocha huyo Mfaransa ni mwajiriwa wa Simba, unajua malipo yanakuwa ni ya mwezi. Hata yakiwa ya wiki, huwa yanatengenezwa kujenga mwezi.
Kuupata mwezi, lazima Sh 42,000 ya dakika uitafutie saa ambayo inakuwa ni mara 60, unapata Sh 2,520,000 (maana yake kocha huyu, kwa saa moja tu, mshahara wake unakuwa mkubwa kuliko wa wachezaji wake takribani 20. Yaani wachezaji wanaofikia mshahara wa Sh milioni 2, hawawezi kufika 15).
Baada ya kupata saa ambayo ni Sh 2,520,000 ukiipigia mara 24 ili kupata siku, inakuwa ni Sh 60,480,000. Hapa pia unaweza kuanza kushangaa mapema kwamba mshahara wake wa siku moja, unazidi mishahara ya wachezaji wa takribani timu 12 za ligi kuu kwa mwezi?
Kwa fecha hizo, utakapoamua kupata malipo ya mwezi, basi kocha Lechantre anachukua kitita cha Sh bilioni 1.8 ambazo pia zinazidi gharama ya kikosi cha Simba kizima ambacho kimesajiliwa kwa Sh bilioni 1.3.
Kama Simba itakaa naye kwa mwaka mzima, maana yake ni Sh bilioni 21 na chenji kiasi. Kama unakumbuka, mwekezaji mkubwa Simba ni Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji ambaye anawekeza kwa Sh bilioni 20 na matarajio apate hisa za asilimia 49 au 50. Sasa jiulize, uwekezaji wake wote unaweza kuishia kwa kocha pekee tena ndani ya mwaka mmoja, wa nini sasa?
Kama kweli ni hivyo, hii itakuwa Simba ya ajabu zaidi kutokea katika maisha yote. Kama kocha huyo atapata mshahara huo Tanzania, basi Simba bora wangejenga uwanja wao na wakaamua kubaki na Masoud Djuma.
Thamani ya Uwanja wa Taifa ambao ni mzuri kuliko yote Afrika Mashariki na Kati ni Sh bilioni 53 zilizochangwa na Serikali ya Tanzania na China.
Sasa kama Sh bilioni 21 zingejengewa uwanja, Simba ingekuwa na uwanja ghali na mzuri zaidi kuliko viwanja vyote vinavyomilikiwa na klabu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kuna mtu mmoja alijaribu kunifafanulia na kusema kwamba walioripoti walikuwa wanamaanisha kuwa kocha huyo analipwa kwa kila dakika katika 90 tu za mchezo.
Hii nayo ikanishangaza pia, kwamba kwani Simba imemuajiri kocha huyo kwa ajili ya mechi tu, yaani zile dakika 90 tu!
Kocha ni mwajiriwa wa Simba na si deiwaka. Anapokuwa katika benchi, kumbuka atakuwa akishiriki katika mazoezi, mikutano na viongozi wa klabu, mikutano na benchi la ufundi. Kumbuka pia hukutana na wachezaji wote au mmoja mmoja.
Sasa unawezaje kumpigia hesabu za mechi kwa mechi katika dakika 90. Wakati mwingine nilifikiri nisijadili ili kujiaminisha huenda hao walioripoti walikuwa wanatania tu!
Kama ni kweli basi haya yatakuwa maajabu ya karne kutoka katika mpira wa Afrika na huenda hata yeye Lechantre atajionea maajabu makubwa kuwa na mshahara takribani nusu ya ule anaolipwa Paul Pogba kule Manchester United.
Sikutaka kuingia ndani sana, nilitaka kuonyesha kiasi gani nimeshangazwa na hilo. Lakini nitasubiri taarifa sahihi ya Klabu ya Simba kama watakubali kutangaza lakini nitafuatilia kujua usahihi, ikiwa ni hivi kweli, nitarudi tuchambue na kushangaa zaidi.
Iliripotiwa kuwa kocha wa mazembe ndie kocha mpya wa simba ikawa ni uzushi tu. Ikaripotiwa kocha mpya wa simba anakuja na wasaidizi wanne ikawa ni uzushi tu. Sasa inaripotiwa kocha wa Simba analipwa 1.8bl kwa mwezi hapana itakuwa ni uzushi tu kama taarifa hizi hazijatolea rasmi na Simba yeneywe. Inashangaza kuona karibu nyingi ya habari zinazotolewa na vyombo vya habari siku hizi ni uzushi tu. Iwe za siasa, michezo au habari zinazohusu jamii zote ni uzushi tu. Gazeti au mtandao wa jamii kuandikwa na kusamabaza habari zisizo na chanzo cha kuaminika na uhalisia wa hizo habari ni fedheha na upotoshaji. Hata huyu kocha Mburundi wajuaji walishamzushia kila aina ya uzushi kitu amabacho inaonesha dhahiri sisi watanzania ni watu tunaoabudu uzushi na majungu ya hovyo na ndio maana hata hivi vilabu vyetu vya mpira na mpira wetu unashindwa kupiga hatua. Simba na viongozi wake sio wapumbavu hasa ukimtilia maanani Mohamedi Mo. Kama kuna watanzania kumi wanaojua faida na hasara katika biashara basi Mohamedi Mo ni miongoni mwa watanzania hao. Simba sio kama hawataki uwanja mzuri wa kisasa ila Simba kama Simba na viongozi wake nnaimani haiwezi kupita hata sekunde moja wa mshale wa saa bila kufikiria suala la uwanja. Na tatizo la uwanja sio Simba tu isipokuwa Tanzania zima kama kuna jambo la aibu katika mpira wa Tanzania basi ni viwanja vya kuichezea mpira angalau Simba ya Daresalam inaweza ikajisaidia katika viwanja vilivyopo. Kwa hiyo ni vizuri kupata ukweli wa jambo kabla ya kuelezea umma na hata kama kweli huyu kocha atakuwa analipwa kiasi hicho cha mshahara kama atakuja kufanya kazi yake kwa matarajio yanayotarajiwa na kuipaisha Simba na Tanzania katika medani za kimataifa kuna tatizo gani? Pengine kutokana na uzowefu wake wa kazi akawawezesha wachezaji kadhaa wazawa kuonekana zaidi duniani na hatimae kutoka zaidi kimataifa hatuoni kuwa ni faida au huwa tunaangalia hasara tu? Nafikiri kila mtanzania anatamani kuwaona wachezaji au vijana wetu wakicheza nchi za nje hasa ulaya sasa huyu kocha mpya wa Simba ni miongoni mwa watu au makocha wa kutupelekea vijana wetu kucheza soka ulaya ila ukitaka kula kizuri lazima udhurike.
ReplyDelete