NA SALEH ALLY
NILIMSIKILIZA Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumzia kuhusiana na suala la watu kulaani kuhusiana na wao kuwa na timu zao ambazo ziko daraja la kwanza na huenda wanazisaidia kutaka kupanda daraja hadi Ligi Kuu Bara.
Karia alikuwa akizungumzia watu kusema yeye anaisaidia Coastal Union kwa kuwa ni shabiki wa timu hiyo lakini makamu wake, Michael Wambura kwamba anaipendelea Biashara Mara kwa kuwa anataka juu chini kuona mkoani kwake kuna timu inayocheza Ligi Kuu Bara baada ya miaka rundo ya kuhangaika.
Wakati Karia anazungumzia suala hilo, alichokumbushia akiwa makamu wa rais wa TFF chini ya Jamal Malinzi aliyekuwa rais kwamba timu mbili za Tanga za Coastal Union na African Sports ambazo ziliteremka daraja na yeye hakufanya chochote kuziokoa kwa kuwa anapenda haki.
Hivyo akasisitiza, asisingiziwe kama zitapanda zote kwa madai kwamba anazipendelea. Huku akisisitiza kama Coastal na African Sports, zitapanda basi zipande tu kwa kuwa amechoka na kelele hizo.
Katika mazungumzo hayo ya Karia pia watu wanaolalamika viongozi wa juu wana timu zao, upande mmoja naungana kabisa na Karia na upande mwingine napingana naye kabisa, nitaeleza kwa nini.
Katika upande ambao ninaungana naye ni kwamba anapaswa kuwa na uhuru kama mwanadamu kuwa na timu ili mradi anafuata taratibu ambazo ni sahihi.
Sote tunajua Karia amewahi kuwa kiongozi wa Coastal Union, pia ni shabiki wa siku nyingi sana wa timu hiyo na moja ya klabu kongwe nchini. Nafikiri hakuwezi kuwa na ubaya kwa kuwa Karia naye ni mwanadamu.
Kwa Wambura, wanaosema yeye na timu ya Mara, sijawahi kusikia ni shabiki lakini ni kiongozi wa chama cha soka cha mkoani humo, hilo linajulikana na haliwezi kuwa tatizo kama ilivyo kwa Karia kama watakuwa wanafuata weledi.
Lakini ninachopingana na Karia ni kuhusiana na kuweka msisitizo huku akikumbushia kuhusu suala la yeye wakati akiwa makamu wa rais timu za Coastal Union na African Sports ziliteremka daraja na hakuzitetea, hiyo haina mashiko ya kumfanya asihojiwe wakati akiwa Rais wa TFF.
Ambacho anapaswa kukumbuka Karia kwamba sasa yeye ni rais wa shirikisho, ndiye kiongozi wa juu, hivyo ni vema kusikiliza malalamiko kama yana mashiko maana pamoja na kusikia tu, inawezekana kuna watu wanatumia jina lake vibaya au wanatumia vibaya jina la Wambura.
Kwamba wao wanaweza wakawa wanaona kama watu wanakosea, kumbe watu wanafanya ujanja kuonyesha “hii ni timu ya rais”, ikiwa ni sehemu ya propaganda.
Hivyo, badala kuzungumza ile kwa jazba kwamba kama timu zinapanda basi zipande tu, haitakuwa sawa.
Unajua kwa yeye kama kiongozi wa juu anaweza akawa hajasikia mambo mengi sana, hivyo wakati wa kuyapokea kwa mapokeo chanya na kuyachambua kwamba wanaosema kwamba anaipendelea Coastal Union walitumia kigezo kipi.
Kama watakuwa wana hoja, basi azifanyie kazi na ikiwezekana lingekuwa jambo zuri sana kama angeanza kuwaonyesha wanaotumia vibaya jina lake na kusisitiza uchezaji wenye maamuzi ya haki.
Sote tunajua daraja la kwanza “kumeoza” na kuna mambo mengi ya kuoneana na kuvunjana nguvu ambayo viongozi wa juu ndiyo wanapaswa kusimamia na kuhakikisha hayaendelei kwa kuwa wadai wamefikia sasa wamechoshwa.
Kama watu wanakosea kuhusiana na Karia waelezwe, lakini wale wanaotaka kutumia majina yao vibaya nao waonywe kuhusiana na wanachofanya badala ya kuwaacha na kusema kama inapanda ipande, hiyo ni kuzidi kuchanganya mambo na kuwapa nafasi wanaofanya hivyo kama wapo waendelee.
Lazima viongozi wa TFF wakemee kwa nguvu yanayotokea Ligi Daraja la Kwanza lakini lazima wawakikishie wadau pale kunapokuwa na swali.
0 COMMENTS:
Post a Comment