February 17, 2018







Na Saleh Ally
SIMBA sasa iko kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 42, hii ni baada ya kucheza mechi 18, maana yake kuna mechi 12 zinasubiriwa.

Mashabiki na wanachama wa Simba wana hamu kubwa ya kukata kiu yao, nayo ni kuona timu yao ikibeba ubingwa baada ya misimu minne ya kutokuwa na kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Yanga wamechukua mara tatu, Azam FC mara moja na Simba wameambulia patupu. Hili limekuwa likiwaumiza sana mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.

Safari hii huenda watakuwa na maumivu makali zaidi kama wataukosa ubingwa huo kwa kuwa wanategemea mkono mmoja tu. Mwingine tayari si mali yao kutokana na hali halisi.

Mkono mwingine wa kuwashikisha kombe na kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ni michuano ya Kombe la Shirikisho ya Azam Sports ambayo tayari wameng’olewa na kuvuliwa ubingwa na timu ya daraja la pili ya Green Worriers. Wanachotemea sasa ili washiriki michuano ya kimataifa ni kubeba ubingwa wa ligi kuu.


Simba wanapambana kutumia jiwe moja ili kuua ndege wawili na wanajua uchungu watakaokuwa nao kama hawatafanikiwa. Maana yake kama ni kazi basi kila mmoja wao anatakiwa kufanya mara mbili zaidi ya kawaida, au kufanya kwa ziada.

Kama ni wachezaji inabidi wafanye mara mbili ya kawaida, vivyo hivyo kwa makocha, viongozi na mashabiki pia wanatakiwa kushangilia mara mbili zaidi ya kawaida.

Pamoja na kwamba Simba wamekuwa wanapambana, leo nataka nifungue mjadala huru kuhusiana na faida ya kuwa na mtu au yule ambaye unaona faida yake ni ipi hasa.

Naanzia kwa mshambuliaji Laudit Mavugo ambaye Simba ilisumbuka kwa kiwango kikubwa kuhakikisha inampata. Likawa gumzo la misimu kuhakikisha anatua Simba na mwisho uongozi ukafanya kila juhudi kuhakikisha anapata nafasi na kujiunga na Simba, leo huyo hapo.

Taarifa wakati anakuja nchini, alikuwa amefunga mabao zaidi ya 16 kwa kila msimu ndani ya misimu miwili na kuwa mfungaji bora mara zote. Alielezwa kuwa mshambulizi hatari na Simba haikuchoka kumtafuta.

Nakumbuka wakati Simba ikipambana kumtafuta, mmoja wa waandishi wakongwe wa Rwanda alinieleza alikuwa akishangazwa na juhudi kuu za Simba kumpata Mavugo ambaye alionekana ni mshambulizi wa kawaida naye alikuwa akiijua kazi yake vizuri kwa kuwa aliichezea Polisi Rwanda chini ya Goran Kopunovic ambaye amewahi kuifundisha Simba.


Mwandishi huyo ambaye ni rafiki yangu, alisema Mavugo alikuwa ni mshambuliaji mzuri lakini wa kiwango cha kawaida kabisa na Simba hawakupaswa kusumbuka kumpata kwa kuwa nchi kama Tanzania wanaweza kupata washambulizi wengi. Nikamueleza, acha wakimpata tuone.

Hakika bila kuzungusha maneno Simba hawapaswi kujilaumu kwa kuwa walijaribu kutafuta kilicho bora kutokana na rekodi za Mavugo alizokuwa nazo lakini inaonekana amefeli na sasa haipaswi kupoteza muda tena.

Huenda uoga au subira ya kupita kiasi ndiyo imembakiza Mavugo Simba lakini alitakiwa kuondoka wakati wa dirisha dogo na nafasi yake ingechukuliwa na mchezaji mwingine.

Wakati mwingine unaweza kuona kwamba Simba ingeweza kumbakiza Fredric Blagnon na kumruhusu Mavugo maana tofauti ya wachezaji hao ilikuwa inaonyesha mmoja ana uchezaji wa kuburudisha lakini hafungi ambaye ni Mavugo na mwingine hana burudani lakini akipata nafasi hafanyi utani ambaye ni Blagnon.

Binafsi kiufundi namkubali Mavugo, hii ilinipa matumaini kwamba siku moja atabadilika na kuwa msaada kwa Simba na somo kwa wachezaji wa Kitanzania kwa kuwa atatoa changamoto. Sasa ana mabao mawili msimu huu na saba msimu uliopita.

Simba imempa nafasi ya kutosha, makocha waliokuwepo ukianzia na Jackson Mayanja, Joseph Omog, Masoud Djuma na sasa Pierre Lechantre wamempa nafasi ya kutosha, lakini haonyeshi kuwa ni bora na anastahili kuwa tegemeo katika ushambuliaji.

Utamtetea kwa kusema kuwa hajazoea, utachekwa. Utasema ana hofu, kazi ya kuipunguza na kuimaliza ni yake, lakini hata ukimuona anavyocheza utafikiri Simba wanamkopa au wanamlazimisha kucheza namba ambayo si yake.

Hashindani kuonyesha kweli anataka kushinda au anacheza akiwa ni msaada kwa Simba. Ukweli Mavugo anainyonya Simba, anachukua wakati yeye hakuna anachotoa kusaidia.


Vizuri apambane kuhakikisha anamaliza msimu angalau ana mabao 10, lakini awe msaada katika michuano ya kimataifa ili kuifanya Simba kuwa na uhakika kama Bocco anaumia au mgonjwa, basi yeye Simba iwe na uhakika kuwa na mshambulizi mwenye umbo kubwa na aache uvivu.

Kama ataendelea kucheza hivyo, halafu ataendelea kubaki Simba, basi nitaamini hayuko kwa faida ya Simba badala yake kuna mtu anambakiza kwa maslahi yake binafsi.

3 COMMENTS:

  1. Tatizo lako unaandika maelezo meeeeeeeengi badala ya ku-focus point kulingana na kichwa cha
    Of course unatia NUX
    Inafika time tunaishia njiani maana ni kama tunasoma kitabu cha JOKA LA MDIMU 😕😕

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kwani Jackson umelazimishwa kusoma? unataka tusome habari ya michezo kama tunasoma sms kwenye cm! Tulia mwandishi afanye kazi yake

      Delete
  2. @Elibarick kumbe na wewe ni Saleh Jembe 😜😜
    Hiyo habar ulituma ww #Nanga

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic