February 3, 2018



Huku akiusoma mchezo kwa kutafakari namna ya kupata nafasi kikosi cha kwanza, beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefungwa plasta ngumu (P.O.P) na atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja akiuguza jeraha la enka.

Ninja alipata majeraha hayo ya enka wakati timu ilipokuwa ikicheza na Mlandege FC mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi mwezi uliopita huko Zanzibar.


Beki huyo tangu amesajiliwa Yanga kutoka Taifa Jang’ombe hajaweza kupata nafasi kikosi cha kwanza mbele ya mabeki Kelvin Yondani na Andrew Vicent ‘Dante’ pia nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Ninja alisema P.O.P hilo alifungwa juzi Alhamisi kwenye Hospitali ya Muhimbili baada ya kupigwa X-Ray kwa mara ya pili na kuonekana mfupa wake una tatizo.

Ninja alisema baada ya kuwekwa P.O.P hilo alipewa magongo mawili yatakayomsaidia kutembea vizuri kwa hofu ya kuukanyagia mguu na kuutonesha.


“Nimeambiwa nitatoa P.O.P hili baada ya wiki mbili, lakini kurejea uwanjani nitarejea baada ya mwezi mmoja nikiwa nimepona kabisa.

“Nilikuwa nimeanza mazoezi mepesi ya binafsi hivi karibuni kabla ya jana (juzi) kwenda Muhimbili kufanyiwa vipimo vya mwisho na kugundulika sehemu ya mfupa kwenye enka kuwa na tatizo,” alisema Ninja.


Daktari wa Yanga, Edward Bavu alisema; “Ninja amefungwa P.O.P na amepewa magongo mawili kwa ajili ya kupata msaada wa kutembea na atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic