NA SALEH ALLY
UKIIANGALIA mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kati Yanga na St Louis ya Shelisheli, utagundua kile nilichowahi kukueleza kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, anatumia kikosi ambacho kwake kingekuwa ni chaguo la pili kulingana na alichokitaka.
Mipango ya usajili ya Lwandamina, ilitegemea wachezaji wengi ambao sasa katika kikosi chake hawapo na wale ambao walionekana watakua taratibu ndiyo wamegeuka kuwa tegemeo.
Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya St Louis, ushindi ambao wapenda soka wengi wanauona ni kiduchu kwa kuwa Yanga ingestahili kushinda angalau mabao 3-0 na kuendelea.
Hali halisi ya kikosi hicho, inaonyesha Yanga ilistahili kushinda bao hilo moja lakini kikubwa ni kuamini kwamba pamoja na ushindi finyu, bado Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi hata kama itakwenda kucheza ugenini.
St Louis wamefungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga ugenini, unaweza kujiuliza vipi Yanga watashindwa kufanya vizuri wakiwa ugenini Shelisheli na ikiwezekana kushinda kwa bao 1-0 tena au zaidi?
Bado haitakuwa rahisi hata kidogo kama Yanga haitajipanga na kubadilisha mawazo ya kuwa wanacheza mechi ya kimataifa tena inayokwenda kwa mfumo wa mtoano.
Ukiingalia vizuri mechi hiyo, utaona wachezaji wengi waliitumikia Yanga kama vile ilikuwa ikicheza mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo kinachohitajika zaidi ni pointi tatu.
| ST LOUIS |
Mechi hiyo ilihitaji ushindi ikiwezekana wa mabao mengi, ilihitaji ushindi ambao ungepatikana kuanzia mapema. Ilihitaji umakini maradufu katika matumizi ya nafasi zilizopatikana.
Yanga imepoteza zaidi ya nafasi saba za wazi za kufunga na inaonekana waliokosa hawakuwa wakijua au waliingia uwanjani wakiwa hawajajazwa vya kutosha kwenye bongo zao kwamba mechi hiyo ni ya kimataifa na rahisi sana kupotea hesabu wasipotuliza vichwa.
Kona:
Katika mechi hiyo ya juzi, Yanga imepata kona 13, imetumia kona moja tu kupata bao baada ya kuwa imefanya mabadiliko. 12 zote hazikuwa na faida na hili ni tatizo kubwa ambalo katika ligi kuu lingekuwa sawa, lakini kimataifa ni kujimaliza.
Faulo:
Yanga imepata mipira zaidi ya mitano ya faulo “zilizokufa”, nje ya lango la St Louis. Unaona wapigaji wote hakuna hata mmoja aliyesababisha hatari langoni kwa Washelisheli hao.
Wapigaji walipiga kwa aina unayoona si watu waliokuwa “wame-focus” kufanya jambo hasa. Walikuwa ni kama watu wanaojaribu na upigaji leo unaona ni Ibrahim Ajibu, baadaye Kessy na baadaye mwingine, Yanga vipi?
Mashuti:
Yanga walipiga mashuti 23 langoni mwa St Louis, kati ya hayo sita ndiyo yaliyolenga lango na 17 yakatoka pembeni. Unaweza kujiuliza timu gani inayocheza nyumbani inaweza kuwa na papara kiasi hicho.
Jiulize mashuti hayo yalipigwa kwa wakati sahihi, yalipigwa kwa ufundi unaotakiwa au kwa kuwa Yanga wanacheza na Shelisheli, kila mmoja aliamini anaweza kufunga?
Ilikuwa ni lazima wachezaji wahakikishe wanafanya kilicho sahihi kwa wakati mwafaka wakijua dakika 45 za kipindi cha kwanza lazima wawe wametangulia na kwa namna ilivyo St Louis, ilikuwa inawezekana angalau kupata bao moja katika kipindi cha kwanza na hasa kama umakini ungekuwa na “chumba kikubwa”.
Penalti:
Imetosha sasa, Yanga kuendelea kumpa mikwaju ya penalti mshambuliaji wake, Obrey Chirwa inakuwa ni kama vile kuna utani au kuogopana.
Ndani ya mwezi mmoja na nusu, Chirwa amekosa penalti tatu katika michuano mitatu tofauti. Ilikuwa Kombe la Mapinduzi, Yanga ikatolewa, akafunga na baadaye kukosa katika Kombe la Shirikisho, Yanga ikanusurika.
Safari hii Ligi ya Mabingwa na jiulize, Yanga inawapiga penalti bora wangapi hasa katika mechi muhimu kama hiyo, kwa nini lazima iwe Chirwa?
Alipokosa penalti hiyo, ilimtoa mchezoni kabisa na hakuonekana tena zaidi ya krosi aliyompigia Buswita akashindwa kumalizia.
Umaliziaji:
Tatizo la umaliziaji ni kati ya matatizo makubwa kwa timu za Tanzania. Yanga walionekana hawakuwa wamejiandaa kutulia na badala yake papara na ikiwezekana kila mmoja kutaka kufunga hasa safu ya ushambulizi.
Ajibu angependa kuonekana amerejea, Chirwa angependa kuonekana ni mkombozi, Buswita angefurahia kuona anaendeleza kufunga. Nani alicheza kama timu kutaka kuona hata wengine wanafunga? Wachezaji wa Yanga lazima wajifunze pia nafasi moja ikipotea hairudi na huenda wakiipata wapinzani wanaweza kuitumia. Katika soka, si kila mmoja anaweza kujaribu.
Uzoefu:
Tukubali, wachezaji wakongwe ambao ni majeruhi, yaani Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko na hata kukosekana kwa Haruna Niyonzima, ni sehemu ya ugumu mkubwa wa kazi kwa Lwandamina.
Ukiangalia, Buswita ilikuwa mechi yake ya kwanza ya kimataifa kama ilivyo kwa Hassan Kessy, Ajibu na Raphael Daud ambaye kidogo hakuwa mwepesi kumaliza mambo haraka.
Kessy alionyesha ana hamu ya ushindi, juhudi ya ushiriki kuwamaliza Washelisheli. Buswita pia alijitahidi kama ilivyo kwa Daud na Ajibu. Bado unaona utofauti wa kile ambacho sahihi walistahili kukifanya hakikufanyika.
Angalia tofauti na ilivyokuwa kwa Papy Tshishimbi ambaye pamoja na kuishikilia “roho” ya timu lakini ndiye alitoa pasi ya bao.
Hata Kelvin Yondani, alionyesha ni mkomavu na mchezaji wa mechi za kimataifa. Aliweza kupiga angalau mashuti muhimu hata kuliko Ajibu, Buswita na Chirwa.
Martin ni mgeni wa michuano ya kimataifa, lakini alionyesha kuwa alikuwa na hamu ya kufanya vema na alitaka timu ifanye vema.
Wote wanaweza kuwa walitaka timu ishinde, lakini hali ya umakini ilikuwa ndogo katika kikosi cha Yanga na hii ilitokana na wachezaji wengi kuwa na uzoefu mdogo.
St Louis, utaona walicheza soka la kufundishwa na kuwabana Yanga katika ufundi wakitumia muda mwingi kupoza mchezo
Achana na kipa ambaye ni kinda kabisa, huenda kwa kuwa alicheza michuano ya kimataifa ya vijana kwa ngazi za juu, lakini hakuwa na kashkash kubwa.
CHA KUFANYA:
Lwandamina ni mzoefu wa michuano ya kimataifa, hakika wachezaji wake lazima wabadilike na wana nafasi ya kuitumia nafasi ya ugenini kushinda.
Wamepoteza nafasi nyingi za wazi na walionyesha “utoto” wa kutojua hesabu sahihi. Mechi inayofuata ni lazima waonyeshe mechi iliyopita, imewakuza na kuwabadili.
Yanga inapaswa kuwaandaa zaidi wachezaji wake maana mapengo ya wakongwe ni tatizo na lazima wakubali, hawakulitumia sahihi dirisha dogo.
Walipaswa kutokuwa waoga na kutohofia mashabiki, badala yake uamuzi sahihi ukiwemo kuwakata majeruhi wasiopona, Yanga haiwezi kuwasubiri milele kwa kuwa ina malengo yake kama sasa, nafasi muhimu uwanjani, zimebaki jukwaani.








Pengine mambo haya yangeelezwa kabla ya match ingekuwa wakati muafaka.
ReplyDelete