Simba imefanikiwa kufanikiwa kuwaondoa Gendarmarie ya Djibouti na sasa itakutana na Al Masry ya Misri.
Al Masry ndiyo wamekuwa gumzo kwa kuwa kila mmoja anajua Simba wanakutana na timu ngumu hasa.
Lakini kipa namba moja wa Simba , Aishi Manula hana hofu na ameonekana kufurahi kukutana na Al Masry huku akitamka kuwa hao ndiyo ‘saizi’ yao kutokana na ubora wa kikosi chao.
Simba ilifanikiwa kutinga katika hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwaondoa Gendarmarie kwa ushindi wa mabao 5-0 walioupata nyumbani na ugenini.
Timu hiyo, katika uwanja wake wa nyumbani ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana ugenini na kushinda bao 1-0.
Kwa mujibu wa mtandao wa timu hiyo, Manula alisema kuwa kwa upande wao wachezaji wamejiandaa vema na mchezo huo na kikubwa malengo yao ni kuwaondoa kuwaondoa Al Masry katika hatua hiyo ya michuano.
Manula alisema, mechi mbili zilizopita walizocheza na Gendarmarie hazikuwa ngumu kulinganisha na ubora wa kikosi chao ambacho kinaundwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.
“Michezo miwili ya hatua ya awali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmarie haikuwa migumu sana kulinganisha na ubora wa kikosi cha Simba.
“Hazikuwa mechi ngumu sana kulinganisha na ubora tulionao sisi katika kikosi chetu cha Simba chini ya benchi letu la ufundi.
“Ilikuwa ni michezo ya kawaida sana ila nadhani sasa kwenye mchezo unaofuata ndiyo tunaanza mashindano rasmi na tunajiandaa vyema sana kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Al Masry ambao tutaanza nyumbani kwa kucheza mchezo wa kwanza,” alisema Manula.
Simba wanatarajia kucheza mchezo wa kwanza wa hatua ya awali kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Machi 6 kabla ya kurudiana Machi 16, mwaka huko Misri.
0 COMMENTS:
Post a Comment