NA SALEH ALLY
KABLA ya mechi yao jana dhidi ya Ruvu Shooting, Simba walikuwa kileleni na pointi 35 wakifuatiwa na Azam FC halafu mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga ambao walikuwa wameshinda mechi yao ya mwisho kwa mabao 2-0 dhidi ya Lipuli FC mjini Iringa.
Simba ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na mwenendo wake hasa baada ya kushinda mechi nne mfululizo baada ya kuondoka kwa Kocha wake, Joseph Omog ambaye alitupiwa virago.
Omog alitupiwa virago baada ya baada ya Simba kung’olewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho na rasmi kuvuliwa ubingwa ambao yeye aliiwezesha Simba kuubeba kwa mara kwanza baada kuwa imerejeshwa.
Wakati Omog anaondoka, licha ya kwamba Simba inaongoza ligi, bado ushindi wake ulikuwa wa kusuasua ukiambatana na sare mfululizo.
Ilikuwa ni kama mwendo wa panda na kushuka, hali iliyoifanya Simba kutokuwa na uhakika na hasa utaona ilikuwa ikichuana na Yanga na Azam FC kwa tofauti ya mabao na leo ilikuwa Azam FC wako kileleni kesho wenyewe.
Baada ya Simba kushinda mechi nne mfululizo, tayari mambo yakabadilika na pengo la pointi likaanza kujitokeza kufikia hali ilivyo sasa.
Ushindi wa mechi nne mfululizo uliipa Simba pointi 12, lakini timu ikafunga mabao 12 bila ya kufungwa, jambo ambalo liliifanya kutengeneza pengo jingine kubwa la mabao ya kufunga.
Kutokana na mwendo huo, gumzo la ubingwa likaanza na sasa ikawa kuzungumzia Simba itatwaa ubingwa au ndiyo ina nafasi kubwa kati ligi ndiyo ilikuwa imeingia katikati.
Safari ya mechi 15 katika ligi kuu si mchezo, tena huu ni mzunguko wa lala salama ambao kila mmoja anakuwa anapigania “hali yake”. Haliwezi kuwa jambo dogo hata kidogo.
Inawezekana kabisa wachezaji wa Simba wakawa katika nafasi ya kufanya vizuri katika kipindi hiki kutokana na mambo mawili makubwa.
Kuachiwa timu kwa Kocha Msaidizi, Masoud Djuma. Ambaye kwa wachezaji ilikuwa kila mmoja aonyeshe kwamba anastahili kucheza na si kama ilivyokuwa awali kwa Omog ambaye walikuwa wamemzoea.
Kama unakumbuka, Djuma amewaongoza mechi tatu mfululizo wakianza kushinda 2-0 ugenini dhidi ya Ndanda FC, halafu wakaitwanga Singida United mabao 4-0 kama ya kuivurumisha kwao Kagera Sugar kwa mabao 2-0.
Wachezaji walikuwa ni lazima wamuonyeshe Djuma wanastahili kucheza na hakuna zaidi ya kufanya vizuri zaidi. Baada ya mechi tatu, kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anaanza kazi na moja kwa moja wachezaji wanajikuta tena kwenye utawala mpya ambao pia lazima waonyeshe.
Mechi ya kwanza wakashinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji na ya pili chini ya Mfaransa huyo ni jana dhidi ya Ruvu Shooting.
Ukiangalia kinachowainua Simba ni suala la nidhamu na kujituma na wachezaji wanafanya hivyo kwa kuwa wanajua wanaingia kwenye utawala mpya wa kocha ambaye lazima atahitaji mambo hayo.
Hivyo wanayafanyia kazi kwa nidhamu ya juu na juhudi kubwa, ndiyo maana uwezo wao unafanya kazi kwa kiwango cha juu na sahihi kabisa. Hivyo lazima tuone tofauti kutokana na uhalisia.
Simba wanaweza kuwa mabingwa katika mechi 15 zilizobaki kama suala la nidhamu na juhudi sahihi yenye matokeo ya maarifa. Lakini kama watajisahau kama ilivyokuwa awali, basi watajua miujiza ya soka iko wapi.
Wanaodhani Simba tayari ni bingwa wanajidanganya, mpira hauna rafiki asiye na nidhamu au asiye na juhudi na maarifa. Ukiacha hata kama unaujua basi unakushangaza, nidhamu iliyotukuka au sahihi. Simba wakiendelea hivi, mwisho faida itakuwa kubwa kwao, wakijiona wao ndiyo wao, taarifa wataipata.
0 COMMENTS:
Post a Comment