March 1, 2018






Na Saleh Ally
WIKI iliyopita klabu ya Ruvu Shooting ilifanya hafla yake fupi ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya mambo kadhaa yaliyotangazwa.

Shooting walikuwa wamejipanga na mambo mengi ambayo yalionyesha wazi kwamba wana mipango endelevu na ya muda mrefu.

Klabu hiyo ilitangaza rasmi kuingia katika mfumo wa hisa wakiindoa mikononi mwa jeshi na sasa wamiliki watakuwa ni wale walionunua hisa.

Ingawa jeshi nalo lina hisa zake, lakini watu wengine kama akina Saleh Ally, nao wanaweza kuwa na nafasi ya kumiliki Ruvu Shooting, moja ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Maana yake, Ruvu Shooting wameamua kuingia katika mikono mchanganyiko, yaaniile ya jeshi pamoja na wadau wengine wa soka na kwa kiasi kikubwa itawaongezea idadi ya mashabiki ambao watafuta mawazo ya kuwa ni timu ya jeshi.

Timu nyingi ambazo hujulikana kuwa ni timu za jeshi pekee, wananchi wamekuwa hawapendi kujihusisha nazo kwa kuwa wanaamini kwamba tayari zina wahusika wenyewe.

Hii imekuwa ni athari kubwa kwa timu nyingi ambazo zinamilikiwa na majeshi kuwa na urafiki mdogo na wananchi wa kawaida. Huenda hata Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeona hili jambo. Kwa uamuzi wao, Ruvu Shooting wanaweza wakawa wameukwepa mtego wa Fifa.

Pamoja na kujitangaza kuhusiana na hisa, Ruvu Shooting walitangaza uzinduzi wa jezi zao maalum kwa ajili ya mashabiki wao.

Jambo hili limekuwa zuri zaidi kwa kuwa Ruvu Shooting wameonekana sasa ni timu ambayo iko makini na ina mipango endelevu inayolenga kuifanya timu hiyo kuwa kubwa zaidi na ushindani wake sasa hautakuwa uwanjani pekee badala yake hadi kibiashara.

Mfano wakati wanauza jezi zao, tayari Ruvu Shooting watakuwa wanaua ndege wawili kwa jiwe moja hasa pale unapozungumzia suala la kuingiza faida.

Kwanza ni suala la wao kuingiza faida kutokana na jezi hizo ambazo watakuwa wakiuza kwa mashabiki wao. Tena vizuri zaidi kwa kuwa waliamua kuuza kwa Sh 20,000 kwa kila jezi.


Ingawa ninaweza kuwashauri kwa kuwa ndiyo wanaingia katika biashara hiyo na wao ni wachanga katika biashar hiyo au idadi ya mashabiki waliyonayo, bado wanaweza kupunguza bei zaidi na kuwa hata nusu yake, yaani Sh 10,000 kwa jezi za mashabiki ili wafaidike zaidi na kujikusanyia watu zaidi.

Faida ya pili ni kwa wale wanaouza maziwa ya Cowbell. Kama unakumbuka awali niliwahi kuwapongeza na kueleza kampuni zinazojitokeza kupongeza timu ndogo ambazo si Simba, Yanga au nyingine kama Azam FC na Singida United zinapaswa kupongezwa.

Maziwa ya Cowbell yatafaidika zaidi kila Ruvu Shooting inapouza jezi zake kwa mashabiki lakini Ruvu Shooting nao watafaidika kwa kumfanya mdhamini ajione anatangazika zaidi na hii itazidi kuwavuta ikiwezekana kuwekeza zaidi baada ya kuona wana faida kubwa.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amekuwa rafiki wa karibu kila mtu kutokana na juhudi kubwa ya kuizungumzia na kupamba timu yake.


Kwa hatua wanazochukua sasa huku wakifanya angalau vizuri katika Ligi Kuu Bara itazidi kuipatia Ruvu Shooting heshima ya kuwa timu ambazo hazina maneno pekee badala yake kazi wanaijua na mipango ya maisha yao si ya kuishia kesho, badala yake wanaona mbele.

Timu kama Ruvu Shooting inapofikia kufanya hivyo, inapaswa kuungwa mkono na kupewa moyo kwa kuwa inakuwa inafuta zile hisia za kuamini kila timu inayofanya vema au kuwa na mipango bora lazima iwe Simba au Yanga pekee, jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma mpira wetu.






0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic