May 21, 2018





NA SALEH ALLY
NIMESEMA mara nyingi sana kuhusiana na mpira wa Tanzania kujaa unafiki kupindukia.

Watu wengi wanaohusika katika michezo na hasa mpira, si waaminifu, wanaongozwa na unafiki pia ni watu ambao ushabiki ndiyo wanaamini ni mafanikio makubwa katika kupata maendeleo katika michezo.
Nimepinga sana hali hii, lakini naona kuna mlima mkubwa wa aina hii ya watu katika michezo na hasa soka.

Rais Magufuli alizungumza mambo mengi ya msingi, ajabu kabisa baada ya hapo, mashabiki wa soka waliona mjadala mkubwa ni suala la tundu aliposema Kagera waliona tundu. Wakasahau yote ya msingi, sijui katika mpira kuna wasiojua au wajuaji ni wengi kuliko uwezo wao!

Nimevutiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, John Pombe Magufuli, huenda mechi za soka zenye kujaza watu zinahitaji aina yake kama wageni rasmi ili kusaidia kubadili mambo mengi sana.
Angalia, wageni wengi rasmi wanapenda kuremba, kubembeleza na kuhofia kuonekana wabaya. Huenda wangependa kutoa sifa zaidi kwa wahusika ili waweze kushangiliwa uwanjani hapo, lakini Magufuli alituonyesha tofauti kabisa.

Wageni rasmi wengi, hupenda kutoa sifa nyingi hata zisizokuwa na maana lakini kwa Rais Magufuli sote tumeona tofauti na inawezekana kawa mgeni rasmi anayegusa zaidi kuliko wengine waliowahi kutokea.
Kama kuna mwingine aliwahi kutokea basi sikuwahi kumsikia lakini alichokifanya Rais Magufuli, kilikuwa ni zaidi ya darasa na sasa Simba, Yanga na wengine wanapaswa kukifanyia kazi.


Nitawakumbusha baadhi ya mambo ambayo aliyazungumza yaliyojaa ukweli na hayakwepeki na ili kubadilika na kuingia upande wenye tofauti, basi kikubwa itakuwa ni kuyafanyia kazi.

Usindikizaji:
Viongozi, makocha na wachezaji wa Simba na Yanga watakuwa wamelisikia hili suala la Magufuli. Kwamba amechoshwa na usindikizwaji na hili sote tunalijua na tumelijadili mara nyingi tu.

Kawaambia Simba wawe wa kwanza kwenda kubeba ubingwa wa Afrika, lakini Yanga ndiyo wanapaswa kuwa wa kwanza kwa kuwa sasa wanaendelea.

Mnajua kubeba ubingwa wa Afrika nini kinahitajika, Simba na Yanga mnajua kinachotakiwa na maandalizi ya kubeba ubingwa hamna hata kidogo. Sasa basi muanze kufanya mambo sahihi ili kubadili mambo sasa.

Wakachukue kombe:
Kuchukua kombe, tutadanganyana, lakini Rais Magufuli ameonyesha yuko chanya, hivyo Simba na Yanga, waanze kujipanga kuanzia sasa ili wafikie malengo kwa kuwa tunajua bado ana muda wa kuongoza, kabla hajaondoka kufanikisha inawezekana lakini haitakuwa lelemama bila ya uwekezaji, watu sahihi na mipango sahihi.



Mpira mbovu:
Mgeni rasmi gani angeweza kuwaambia Simba mbele ya kadamnasi kama wameonyesha soka lisilo na kiwango cha Afrika? Rais Magufuli amepita katikati bila ya kupoteza muda, kweli kwa kiwango kile, ubingwa wa Afrika itakuwa hadithi ya milele.

Mgeni rasmi kashafanya yake, kawaachia mzigo wa ukweli na sasa ufanyieni kazi.

Yanga nao washinde:
Ujumbe wa Yanga washinde katikati ya kadamnasi ya watu wa Simba, hili ni jambo jingine linaloonyesha mgeni rasmi si mtu wa kuyumba au uoga.

Rushwa na michezo:
Rais Magufuli ameeleza tuhuma za rushwa jambo ambalo katika michezo limekithiri.

Nani mwingine angeweza kusema vile tena Simba kukiwa na tuhuma hizo. Lazima tukubali kubadilika na tusitake kuitafsiri hiyo kauli yake kama sehemu ya kuwa kuna uonevu au vinginevyo.

Kweli kuna hayo matatizo, inawezekana hata viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamekuwa na wakati mgumu kwa kuwa wameamua kupambana kwa juhudi kuu dhidi ya rushwa.

Tuache mambo ya kuzunguka, tuache uongo, tuachane na mambo ya kuamini kuwa katika michezo ni sehemu ya kujichukulia fedha tu huku michezo ikidorora na nchi kuendelea kupata aibu. Badilikeni na mtaona mambo yanakuwa tofauti.

Ingewezekana kila mechi kubwa mgeni rasmi kama Rais Magufuli angekuwa anaalikwa ili kuendelea kutoa darasa kama hilo alilolitoa ambalo litadumu miaka 10 ijayo.

Kumbukeni alichokisema kitaendelea kuwa kumbukumbu na mifano “kumbukwa” kwa kuwa aligusa sehemu husika tena penyewe ndani ya tundu.









1 COMMENTS:

  1. Brother Saleh,tuache siasa na mambo mengine ya mtu chuki zake binafsi lakini Magufuli Kiboko. Ni vigumu kuamini yakwamba ni Mtanzania halisi aliezaliwa na kukulia katika jamii ya kitanzania kwa sababu tatizo letu kubwa watanzania ni kuzungumza ukweli na kuusimamia kwa vitendo. Hali halisi ya kiwango chetu cha michezo Tanzania si kwenye mpira tu bali hata michezo mingine kwa kipindi kirefu sasa ni ya kutia aibu na si jambo la kulimumunyia kauli tena ni la kuliezea ukweli na kwa kiasi fulani hata kutumia neno "kuelezea ukweli" huwa halikizi uzito wa tatizo lilipo kwenye madhaifu yetu kwenye michezo labda neno halisi la kutumia ni 'kukemea' hali yetu duni na dhalili ya ushiriki wetu katika michezo. Wakati mwengine utasikia watanzania tunasingizia hali yetu duni ya michezo hasa mpira wa miguu hutokana na hali yetu duni ya kiuchumi lakini tukikutana na waburundi wanatufunga sasa sina uhakika lakini kati ya Burundi na Tanzania sijui bani ana hali ngumu zaidi ya kiuchumi.Watanzania licha yakuwa wavivu wa kuzungumza ukweli lakini ni wavivu wa akili na kimwili vile vile. Suala la gharama katika michezo sawa hatukatai lakini kama mpira ni pesa peke yake basi Marekani wangebeba kombe la dunia karibu kila mashindano. Lakin tatizo letu sisi Watanzania hatuna hata mchezo mmoja tunaoweza kuleta ushindani wa kweli kwa wapinzani wetu kila siku sisi ni washindikizaji. Kwa hivyo kauli na masisitizo ya muheshimiwa Raisi Magufuli imekuja katika wakati muafaka kabisa au tuseme amechelewa. Ingawa kuna watu lazima hawatawacha mzaha juu ya kauli zake lakini ai jambao la ajabu kwani sisi ni watanzania wengi wetu huona majungu ni tija zaidi kuliko mafanikio.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic