May 24, 2018




Na Saleh Ally
SIMBA imefanikiwa kurudisha  heshima ya kubeba ubingwa wa Tanzania Bara baada ya kuukosa kwa misimu mitano mfululizo.

Jambo ambalo lilikuwa ni kama kidonda ndani ya mioyo ya Wanasimba. Wamekuwa wakijaribu kukitibu bila ya mafanikio hata punde.

Utaona, msimu uliopita, Simba ilifanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho. Unaweza kusema ulikuwa ni msimu wa mafanikio makubwa kwa kuwa hata katika Ligi Kuu Bara walishika nafasi ya pili, Yanga wakabeba ubingwa wakiwazidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa pekee.

Pamoja na hayo, Simba hawakuonyesha kukitibu kidonda ambacho kiliwasumbua kwa muda mrefu. Ilionekana wazi, maumivu yao yalikuwa sehemu nyingine na pale walipopata ahueni maana walitaka kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara.

Ilionekana moja kwa moja, bila ya ubingwa wa Tanzania Bara, maumivu ya kidonda cha Simba yangeendelea kuwa makali tena na tena.

Msimu huu Simba imefanikiwa kuponya kidonda cha miaka nenda rudi kilichowasumbua Wanasimba. Imebeba ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza baada ya misimu hiyo mitano ya maumivu.


Simba imechukua ubingwa takribani mwaka mmoja baada ya viongozi wake wakuu wawili wa juu kuingia mahabusu wakiwa na tuhuma za utakatishaji wa fedha za klabu hiyo.


Rais wa klabu, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ambao nafasi zao kwa sasa kaimu na ni Salim Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna ambao hakika wanastahili pongezi kwa kazi waliyofanya kupambana hadi mwisho baada ya kukabidhiwa jukumu la kupambana na kuponya kidonda cha Wanasimba wenzao.


Wamefanikiwa, lakini hakuna ubishi kama walianza kufanya vema basi walipita kwa kuendeleza au kubadili yale ambayo wamekuwa wakiyafanya akina Aveva na wengine.


Nimeona viongozi hao pamoja na kufanya vizuri wameshindwa kuwa jasiri, kuonyesha kwamba wanatambua kuna mchango wa akina Aveva na Kaburu ndani yake.

Lakini hata katika shukurani ambazo zimekuwa zikitolewa, hatujasikia shukurani zilizopolekwa kwa wale ambao walikuwa wakiipigania klabu na timu yake kama Zacharia Hans Poppe ambaye anatakiwa kuunganishwa katika kesi ya akina Aveva na Kaburu.

Hans Poppe amekuwa akisema yuko nchini India akipata matibabu ya mguu na atarejea Tanzania baada ya matibabu hayo.

Ninachokiona, viongozi wa Simba wamekuwa waoga hata kuwataja wenzao. Wamekuwa wanahofia hata kufungua midomo yao kuyataja majina jambo ambalo ambalo si sahihi hata kidogo kwa mtu imara ambaye anatambua kilicho sahihi.

Nisingependa kuchimba sana na mwisho kuingilia uhuru wa mahakama. Lakini ninawakumbusha kwamba Aveva na Kaburu ni watuhumiwa tu, bado hawajapatikana na hatia.

Kusema mazuri waliyofanya, kuwashukuru kwa michango yao wakati wakiwa na klabu si jambo baya wala haitakuwa kuvunja sheria.


Waliitumikia Simba kwa nguvu zao zote, bado hatujaambiwa wamekosea, hivyo msifumbe midomo hata kusema hatua waliyoifikisha Simba kufikia hatua ya kuponya kidonda hicho.


Walishiriki kwenye usajili, walishiriki katika maandalizi na wanastahili haya matunda.


Sina hofu na suala la medali kama ambavyo inazungumziwa mitandaoni. Lakini ninaamini siku wakitoka rais na makamu wake, watatakiwa kuwakabidhi medali zao za ubingwa kwa kuwa wakati timu inachukua ubingwa wao ndiyo viongozi wakuu.

Tujifunze jambo la kusema yaliyo sahihi bila ya woga, tujifunze kukubali au kukubaliana na mazuri yaliyofanywa na wenzetu.


Nilisikia mtu mmoja akilalamika kwamba Kaburu hakuisaidia Simba. Inawezekana alikuwa na makosa yake nakubaliana naye, lakini tukubali lazima kuna mazuri aliyowahi kuifanyia Simba.

Upendo umekuwa ni nguzo ya ujenzi pale mambo yalipoyumba. Hivyo ni jambo zuri sana kama watu wanaweza kuwajali wenzao walio kwenye shida badala ya kuona kama kuwataja ni sawa na kuonekana kama wao.


Mmeshindwa kuwataja siku ya sherehe za ubingwa na kuonyesha mnathamini mchango wao. Lakini mmeshindwa basi hata kuwazungumzia katika mabadiliko ya Simba kwa kuwa kumbukeni wakati yanaanza, Aveva ndiye alikuwa kiongozi wa juu, pamoja na Kaburu na mara kadhaa tulielezwa walikutana na Mohamed Dewji kusikiliza nia yake ya kutaka kuwekeza.


Walianzisha, kama yanaonekana ni mafanikio, basi wakumbukeni na muonyesha mnathamini.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic