June 10, 2018


Na George Mganga

Mechi ya fainali ya SportPesa Super Cup imemalizika kwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Kenya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Gor Mahia walitawala zaidi mchezo wakiwa na kikosi chao kamili huku Simba wakipata wakati mgumu kutengeneza nafasi za kufunga.

Gor Mahia wamejipatia mabao yao kupitia kwa Mshambuliaji wao hatari, Medy Kagere aliyefunga la kwanza katika dakika ya 6 tu ya mchezo na kufanya kipindi cha kwanza kiende kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza tena kwa Gor Mahia kuzidi kulisakama lango la Simba wakionesha njaa ya kupata goli jingine ambapo mnamo dakika ya 54, Tuyisenga alifunga bao la pili kwa kumalizia mpira wa krosi uliopigwa kutoka kulia mwa Uwanja na kumuacha Kipa Aishi Manula akiwa hana cha kufanya.

Mpaka Mwamuzi wa mchezo anapuliza kipyenga cha kumaliza mchezo, Gor Mahia 2, Simba SC 0.

Ushindi huo unawafanya Gor Mahia kuwa mabingwa wa Kombe la SportPesa Super Cup kwa mara ya pili mfululizo na kujipatia tiketi ya safari kuelekea England kukipiga na Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Ikumbukwe mwaka jana Gor Mahia waliweza kutwaa ubingwa huo katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya kuwafunga wapinzani wao wa Kenya, AFC Leopards kwa jumla ya mabao 3-0.


3 COMMENTS:

  1. Timu bora iliyojiandaa vizuri ndiyo imeshinda. Hongera wachezaji wa Simba mmecheza vizuri mmejitahidi lakini ni dhahiri hakikuwa kikosi bora cha kushinda kikombe. Tatizo letu hatutaki kujikosoa wenyewe tunasema yeyote anaweza kuchezea Simba

    ReplyDelete
  2. Hakuna kitu hapa bongo fani yetu ni umachinga tu.sijui lini tutakua sawa sometimes Una tamani kuhama nchi.

    ReplyDelete
  3. Kwa jinsi Simba ilivyokwenda kwenye haya mashindano ni dhahiri ni wao wenyewe ndio walioizima ndoto ya kwenda kucheza na Everton. Yaani vile vile kibongobongo kimzaha mzaha hakukua na sababu ya simba kuvunja kambi baada ya ligi kuu na kuwaruhusu wachezaji kutawanyika kabla ya kwenda kenya kama kweli walikuwa wapo serious na safari ya Everton lakini sisi kama Watanzania kila siku tuna madhaifu ya ajabu kabisa na matamanio hewa.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV