June 3, 2018







NA SALEH ALLY
Najaribu kukumbusha kwa ile stori ya Mtanzania pekee mwenye mafanikio makubwa zaidi katika mchezo wa mpira wa kikapu tokea uhuru wa nchi yetu.


Unamjua, huyu ni Hasheem Thabit Manka. Mtanzania pekee aliyeleta heshima kubwa na kucheza katika Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani maarufu kama NBA.


Hasheem ni mtoto aliyezaliwa jijini Dodoma na kukulia jijini Dar es Salaam ambako aliishi katika kitongoji cha Sinza.
 Kamwe hakuwa staa zaidi ya umaarufu wake kutokana na mwonekano wa umbo lake refu wakati huo akiwa na urefu wa Futi 7.1. Baada ya kuanza kupiga hatua hadi anafikia kucheza NBA alikuwa na urefu wa Futi 7.3 na wakati fulani alikuwa mchezaji mrefu kuliko wengine wote katika NBA.


Wakati akiwa na mafanikio makubwa, kila mmoja alifurahia, mambo yake yalipoanza kuyumba, lawama bila uchunguzi, kumshambulia kwa maneno ya kukatisha tamaa bila ya kujua kilichokuwa kinamkabili hadi kushuka vilitawala.


Hakuna aliyewahi kumhoji au kusikia Hasheem anaelezeaje kuhusiana na alipofikia au alipokuwa. Ajabu, hakuna aliyewahi kumsaidia alipofikia pale angeweza kulaumu wakati alipoyumba.


Suala la Hasheem, lilionyesha tulikosa uungwana, tulijidai tunajua bila ya kuhoji na wakati mwingine niseme tulionyesha husuda na kutokuwa na upendo.


Hili suala limejirudia tena kwa Mtanzania Thomas Ulimwengu. Mmoja wa Watanzania ambao wamepata mafanikio makubwa katika soka katika ukanda wa Afrika.
Ulimwengu ni kati ya Watanzania wawili tu waliowahi kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na hata kucheza Kombe la Dunia la klabu.


Yeye na Mbwana Samatta ndiyo wamefikia hatua hiyo. Lakini tumeona Ulimwengu akiporomoshwa na majeraha mfululizo, hili limekuwa jambo lililomporomosha kwa muda sasa.

Ameonekana ameshindwa kufanya vizuri baada ya kuondoka TP Mazembe na kwenda Sweden katika klabu ya AFC ambayo ilimuuza kutoka Sweden kwenda TP Mazembe. Lakini mambo hayakuwa mazuri na alitumia muda mwingi kujitibu.


Ulimwengu alitibiwa Sweden, Afrika Kusini na baadaye Ubelgiji, ikionekana rafiki yake Samatta aliingia katika juhudi kuhakikisha anamuona anapona kwa kuwa alitambua anatakiwa kusaidiwa au kuungwa mkono.


Sisi hatukufanya lolote kumuonyesha Ulimwengu tu pamoja naye. Hatukuonyesha kukerwa na kuyumba kwake na ikiwezekana kama hatuna uwezo wa kumsaidia lolote, basi hata kumuunga mkono kwa maneno mazuri ya kutia moyo wakati akipambana kurejea.


Hakika Ulimwengu amepambana sana kurejea hadi kufikia kusajiliwa tena na klabu kubwa Afrika ya Al Hilal ya nchini Sudan.



Ukiangalia, historia yake ya kuzaliwa Dodoma na kukulia Dar es Salaam inataka kufanana na ile ya Hasheem. Lakini inafanana zaidi kwamba wakati wakipambana kukua, hawakuwa na msaada wetu.


Tulisherekea mafanikio yao wakati wa furaha na walipoingia matatizoni, tukasubiri wageuke na kuwachoma visu mgongoni tukionyesha husuda na unafiki wa wazi bila ya woga tena tukishindwa hata kukumbuka namna walivyotupa sifa na heshima kutokana na kazi zao nzuri.


Ndugu zangu, tuache unafiki, tubadilike na tukubali sisi sote ni wakosefu na tunaweza kurekebishana kwa kuambiana ukweli lakini vema kupeana moyo wakati mgumu na kukumbushana kwamba inawezekana kuvivuka vipindi hivyo.

Kusema maneno ya kufikirika, kushambulia tu bila ya kuwa na uhakika kwa kuwa tuna vidole vinavyoweza kuandika na macho yanayoweza kuona kinachoandikwa, si jambo sahihi.


Jiulize mara ngapi umekosea na ilikuwaje, lakini jiulize unayemlaumu kwa kukosea, uliwahi kumsaidia ili aepuke makosa au atoke katika makosa baada ya kukosea.
Kauli ya Watanzania hatupendani bado hatuwezi kuifuta sasa kutokana na matendo yetu kujaa unafiki, uzandiki na tabia ya husuda.


Tuwapende watu wetu, tuwapende na kuwaunga mkono vijana wetu waliofanya juhudi kufikia juu tukawasikia au kuwaona wakiwa hapo. Siku wakikwama jambo basi wasigeuke ubao wa darts au nyavu za goli kushambuliwa bila ya sababu za msingi badala ya kushauriwa, kupewa moyo na kuungwa mkono ili waamke tena.



Jiulize, wakirejea tena tutaanza kuwashangilia tena? Kama itakuwa hivyo si jambo baya kwa kuwa tutakuwa tunawaunga mkono. Lakini jiulize, utajisikiaje kama kurejea kwao hakutakuwa na msaada wako hata kidogo kama mzalendo?

2 COMMENTS:

  1. Bro rudia kusoma kicha kuna typing error Tukubali nasiyo Tulubali

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic