June 18, 2018



NA SALEH ALLY
SASA umebaki chini ya nusu mwaka kuingia mwaka 2019. Kama Mungu atajaalia uzima kwetu sote, wala haitakuwa muda mrefu tutabadili namba ya mwisho kutoka nane kwenda tisa.

Maana yake tutasema ni mwaka 2019. Wakati unapoingia mwaka mwingine, lazima ujitafakari upya na kupiga hesabu ya ulikopita, zaidi ya siku ulifanya jambo lipi?

Katika maisha kuna kitu tunaita hatua, hatua inaenda na mabadiliko ya mambo, kutoka hatua moja kwenda nyingine. Unapiga hatua kwa kuwa unafanya mambo huku ukibadilisha baadhi.

Unalazimika kufanya hivyo kulingana na wakati, kitu kilichofanyika mwaka 1947 kikafanikiwa, hakiwezi kuwa na nafasi mwaka 2018, labda kiongezewe mambo au vitu na ndiyo tunaita mabadiliko.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), ndiyo kongwe zaidi kwa mabaraza yote barani Afrika, ukiachana na uhalisia wa historia linatambuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Lakini Cecafa ndiyo duni zaidi kimaendeleo, mambo yake mengi yanaenda kwa kusuasua na hakika wahusika wamebaki kuwa walewale na sasa ni viongozi wa kudumu.

Utaona, kipindi hiki chini ya Katibu wake Mkuu, Nicholas Musonye mambo yanazidi kuwa mabaya, mashindano wanayoandaa yanazidi kuporomoka kila kukicha.

Angalia ubora wa zawadi, mfano katika mashindano ya Kagame, imeendelea kubaki dola 30,000 (zaidi ya Sh mil 68) kwa bingwa hadi leo. Ni zaidi ya miaka kumi zawadi hiyo inaendelea kubaki ileile sambamba na zile za washindi wa pili na tatu.

Mashindano hayo yanaongoza kwa kuacha madeni kwa shirikisho husika linalokuwa linaandaa na hii inatoa majibu kwamba yamepunguza mvuto maana gharama za uendeshaji zinakuwa juu kuliko kile kinachopatikana.

Kinachopatikana kinakuwa chini kutokana na kuingiza kidogo hali inayosababishwa na mvuto pungufu wa michuano hiyo. Nani anafanya juhudi kurekebisha hayo?

Jibu hakuna, badala yake Musonye amekuwa akifanya mambo kwa kulazimisha, hali inayojenga adui karibu kila nchi sasa na baadaye mambo yanakwenda kuwa mabaya zaidi.

Musonye, amekuwa na mafanikio katika mashindano hayo kwa kipindi hicho cha chini ya miaka 10 iliyopita. Sasa yanandelea kuwa na zawadi ileile, mfumo uleule wakati klabu zinakwenda zinafunguka macho, sasa zinapiga hatua na kutaka kujiendesha kibiashara zaidi.

Tukubaliane, miaka ya nyuma Cecafa imekuwa ikifaidika zaidi hata kuliko hizo klabu. Sasa klabu nazo zimefungua macho zinataka kufaidika zaidi. Si jambo baya kwa kuwa lazima zijiendeshe kibiashara au kwa faida.

Musonye alitakiwa kubuni njia zaidi, kuyaboresha mashindano hayo na kuyafanya bora na yenye mvuto zaidi na ikiwezekana kuongeza wadhamini zaidi na baada ya hapo mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Kama wadhamini wangeingiza fedha zaidi, klabu zikapata fedha nyingi za maandalizi, fedha kwa wanaoingia mtoano, zawadi za kutosha, zawadi kubwa au nono kwa wafungaji bora, kipa bora, kiungo bora, mchezaji bora na kadhalika, nani angekataa?

Lakini sasa hakuna ubunifu na badala yake, Musonye ameamua kuwa mbabe, anataka kulazimisha mambo na kufanya yaende kwa kubahatisha au anavyotaka yeye.

Musonye amechoka, ni mtu mwenye mawazo yaleyale. Nimekuwa nikisisitiza, Cecafa si mali ya mtu mmoja na wakati umefika anapaswa kuwapisha wengine wanaoweza kuwekeza akili zao na kufanya mambo tofauti.
Aache vitisho, aache kuamini watu bado wamelala na kutaka kufanya mambo ya miaka 10 iliyopita kama mapya mwaka huu au kuelekea ujao. Aondoke aende zake na kuwapa nafasi wengine.


Cecafa kikongwe kisicho na mafanikio, hakijui uchakavu wa sura yake kwa kuwa kinaamini bado kina muonekano wa miaka 10 iliyopita.

2 COMMENTS:

  1. Namshangaa sana huyu Musonye na mambo anayofanya.Mashindano ya CECAFA yanaingilia kalenda za vyama vya soka/FIFA.Mfano Tanzania imemaliza ligi na baadhi ya timu zikaenda kushiriki mashindano ya wadhamini Sport pesa.Zinarejea makwao zikijitayarisha kucheza CECAFA.Zikimaliza mashindano ya CECAFA, then msimu wa ligi kwa Tanzania ligi unaanza August.
    Wachezaji wanapaswa kupumzika kwa maana ya kuwa na likizo kama wafanyakazi au wanafunzi wanapofunga shule.Hapa na mie nawaunga mkono YANGA kwa asilimia mia kujitoa na kuangalia mustakabali wa timu yao na mashindano yaliyo muhimu mbele yao.Kupeleka timu ili kushindania dola elfu 30 wakati mchezaji unamsajili dola elfu 40 haingii akilini.Nawaunga mkono SIMBA ambayo nayo imeamua kupumzisha baadhi ya wachezaji wake kutoshiriki mashindano ya CECAFA.GOR MAHIA itapeleka timu B na kesho tutawasikia RAYON nayo inapeleka timu B.Mambo yakienda hivyo kwa hakika TFF inaingizwa mkenge na itabaki kulia maumivu ya madeni.Viongozi wa TFF msitegemee kuvuna viingilio kutoka kwa mashabiki kwenda uwanjani kwani wengi wao watakuwa busy kwenye luninga na world cup na hata WC ikiisha bado mashabiki watakuwa wameshachoka kuhangaika na mashindano ya CECAFA.

    ReplyDelete
  2. Kwanini CECAFA, TFF na vilabu vinavyoshiriki timu visikubaliane kuingiza vikosi vya pili (B Teams) kama nia ni kuwapumzisha wachezaji wa A Teams lakini michuano ya Kagame Cup iendelee kuwepo kwani inatoa nafasi nyingine kwa timu zetu na wachezaji wake kujenga uwezo zaidi. Mara nyingi tunasema timu zetu zinahitaji michuano mengi zaidi kujenga uwezo bora zaidi na kiwango cvha kimataifa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic