Nahodha wa klabu ya Simba, John Bocco hana shida na suala la wachezaji wa kigeni kuruhusiwa kuwa 10 katika msimu ujao.
Msimu ujao wa 2018/19, kutakuwa na ongezeko la wachezaji watatu wa kigeni kutoka saba ambao walikuwa msimu uliopita na sasa watakuwa 10 kwenye msimu ujao baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa idhini hiyo hivi karibuni.
Bocco amesema; “Kila mtu ana mtazamo wake juu ya suala hili la wachezaji 10 wengine wanasema litaua soka na wengine wanasema litapandisha, kwangu niungane na wale ambao wanasema suala hilo la kuongezwa kwa wachezaji litasaidia kubusti mpira wetu.”
“Nasema hivyo kwa sababu kutakuwa na vita kwanza ya wachezaji wa kigeni wao kama wao lakini pia kutakuwa na vita nyingine kwetu sisi wazawa na wachezaji wa kigeni. Suala hilo la wachezaji wa kigeni kuwa wengi litasaidia kwetu kupambana vilivyo kuhakikisha tunapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
“Yaani kama Mbongo ataingia ndani ya kikosi cha kwanza cha timu yake basi atakuwa amefanya kazi kubwa sana na hilo litasaidia sana kuongeza kitu kwenye soka letu na kwa hali hiyo itakuwa sasa mtu ana uwezo wa kwenda kupambana kokote pale, niwaambie viongozi tu wasajili wachezaji ambao wataleta kweli changamoto ndani ya timu na siyo waje watu ambao watakuwa na viwango vidogo,” alisema Bocco.








POINTI
ReplyDelete