Na Saleh Ally
KUMEKUWA na gumzo kubwa katika michezo kutokana na kauli za viongozi au wanachama maarufu wa klabu ya Simba.
Simba ndiyo inayoonekana kufanya mambo yake kwa mpangilio mzuri kwa kipindihiki hasa kama utafananisha na wakongwe wengine klabu ya Yanga.
Upande wa Yanga, mambo yanakwenda mwendo mbaya na wa uchovu. Migogoro na kutoelewana na inaonekana utulivu inabidi utafutwe.
Simba wanakwenda vizuri, ingawa kuna klabu nyingine zinakwenda vizuri kama Azam FC, Mbeya City. Lakini kikubwa kinaangaliwa ni watani wa jadi, mwendo ukoje. Ukweli upande wa Yanga, mambo si mazuri.
Lakini gumzo la kauli ya kwanza ilitolewa na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah maarufu kama Try Again ambaye alielezea kuhusiana na uamuzi wao kutomchukua Kelvin Yondani kama ilivyokuwa ikielezwa.
Try Again, akaenda mbali zaidi kwa kufafanua kwamba hawakuwa na mpango wa kuchukua mchezaji kutoka Yanga akitoa mfano namna ambavyo walimchukua Haruna Niyonzima na Yanga wakamsajili Ibrahim Ajibu Migomba na mwisho klabu hizo hazikufaidika kutokana na viwango vya wachezaji hao kudorora.
Inajulikana furaha ya mashabiki wa klabu hiyo mbili, kama kuna nyota upande mmoja akasajiliwa upande mwingine, ni furaha kuu kuliko kuangalia timu inahitaji nini.
Kama Try Again ameliona hilo, tena anakiri kupitia makosa ambayo wamepitia. Hapa unagundua kuna mabadiliko makubwa na anakuwa kiongozi anayeonyesha mabadiliko yanahitajika na sasa klabu hizo zinapaswa kufanya mambo kitaalamu badala ya kuangalia ushabiki.
Ushabiki kuingilia mambo ya kitaalamu, imekuwa ni athari kubwa katika klabu hizo na hili limekuwa ni tatizo kubwa. Sasa ni wakati wa kulimaliza hilo.
Lakini unaona, wakati Try Again amezungumza hilo, siku chache baadaye, Mohammed Dewji maarufu kama “Mo Dewji”, ametoa kauli inayoonyesha kuwa ni ya kijasiri.
Kauli yake, Mo Dewji ambaye ni mwanachama maarufu na mwekezaji mtarajiwa wa klabu ya Simba, amesema angependa kuona Yanga imara kwa ajili ya Simba bora.
Mo Dewji anaamini Yanga ikiwa vizuri, itaongeza ushindani kwa Simba na Simba inayopokea ushindani sahihi nayo itakuwa bora zaidi.
Kama haitoshi, Mo Dewji akasisitiza kwamba Yanga ikiwa bora, Simba bora pia inasaidia kupatikana kwa kikosi bora cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Viongozi wengine wangeogopa kusema hili kwa hofu ya kuwadhi mashabiki, kwa hofu ya kuchukiwa na mashabiki. Hii imekuwa ni kawaida na imewapa nguvu mashabiki kuendeleza hisia potofu kwamba ushabiki ni chuki au upande mmoja kufanya vizuri, mwingine unapaswa “majalala” au umechoka hilo mbaya.
Binafsi nimezungumza na kusisitiza sana kwamba kumekuwa na ushabiki wa hisia za kizamani ambao unaingia katika kipindi tofauti na unaonekana umepitwa na wakati lakini wahusika wamekuwa wakilazimisha.
Angalia ule mfumo wa mashabiki wenye rangi nyekundu au njano, kuwapiga wale ambao wanaonekana si mashabiki wa timu yao wanapokuwa uwanjani. Unawapiga wa nini, kwa nini usiwatanie na kama wamekosea pa kukaa wasielekezwe pa kukaa.
Kwa nini mkiwa mashabiki hadi mpigane na kutukanana? Faida yake nini hasa? Rundo la mashabiki ni wale ambao wanashabikia timu kwa sifa. Yaani wangependa kujionyesha mbele ya Yanga au Simba wenzao wao ni mashabiki wenye uchungu kwa kutukana, kuwadhalilisha au kuwalaumu watu. Hii ni tabia mbovu, ushabiki wa kizamani na huenda kupitia kauli za viongozi hao inaweza kusaidia kuwabadilisha wengi kwamba ushabiki si chuki, ugomvi au kuumizana au kuombeana matatizo.
Ushindani bora ni upendo, ushindani bora ni kila upande kuwa imara, hii inasaidia kuzalisha ushindani sahihi.
Binafsi naona kwa kauli hizo mbili, basi kuna nafasi kubwa ya klabu ya Simba kupiga hatua haraka na kuingia kwenye dunia nyingine kabisa.
Kama viongozi wao wa juu watakuwa na mawazo chanya kama hayo. Basi kwa kipindi hiki cha dunia hii inayokwenda haraka, suala la maendeleo kwao litakuwa ni la kugusa tu.
Maana yake watakuwa viongozi wanaoangalia uhalisia, kipi kinachotakiwa kufanyika kwa manufaa ya klabu na si furaha ya muda ya mashabiki au hofu ya kulaumiwa.
Huenda kauli za Try Again na Mo Dewji, zitasaidia kubadili mengi na kuwabadili viongozi wa klabu nyingine na mwisho kuusaidia mpira wa Tanzania ambao umeendelea kudumaa kwa kuwa wakongwe wenyewe nao wamedumaa.
KAULI ZAO.
TRY AGAIN:
“Hatuna mpango wa kumsajili Yondani kwa sababu ni mchezaji tegemeo wa Yanga. Kumsajili Yondani ni kuibomoa Yanga pia kuuboa mpira wa nchi hii.
“Tumepata somo mwaka jana, tulimsajili Haruna Niyonzima na wao wakamsajili Ibrahim Ajibu. Nadhani kila mmoja ni shahidi wa viwango vya wachezaji hao, hawajazisaidia klabu zao.”
MO DEWJI:
“Tunahitaji Yanga imara ambayo inaweza kushindana na Simba.Tunahitaji Yanga imara kwa ajili ya timu bora ya Taifa Stars. Ninawaombea Yanga waweze kupita katika kipindi hiki kigumu kwao, wanapaswa watulie na waungane upya.”
Mimi naona afadhali hata wangemwacha LAUDIT Mavugo na Niyonzima akarejeshwa Yanga hata kwa mkopo. Tangu asajiliwe sioni thamani ya fedha yake.
ReplyDelete