July 6, 2018

Klabu kongwe ya Yanga, kwa sasa inafanya mambo yake kimyakimya na habari mpya ni kwamba uongozi wa timu hiyo umemshusha kocha, Guy Bukasa raia wa DR Congo ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kuwa kocha msaidizi akichukua mikoba ya Shadrack Nsajigwa ambaye aliwekwa pembeni hivi karibuni.

Bukasa ameletwa ikiwa ni kuliongezea nguvu benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mkongo mwingine, Mwinyi Zahera.

Bukasa ametokea katika kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo na alianza kazi jana ikiwa ni muda mfupi kabla ya pambano la Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga itacheza na Gor Mahia ya Kenya, Julai 18, mwaka huu.

Taarifa za uhakika ambazo Championi Ijumaa linazo ni kuwa, kocha huyo tayari ameshaungana na wenzake na amesaini mkataba wa miaka miwili na usajili huo umependekezwa na Zahera ambaye anamjua vizuri baada ya kufanya wote kazi wakiwa kwenye timu ya taifa ya DR Congo.

“Ndiyo ni kweli kwamba pengo la kocha Nsajigwa kwa sasa limeshazibwa baada ya kushushwa kwa kocha mpya kutoka DR Congo, Guy Bukasa ambaye ameshaanza kazi mapema ndani ya timu leo (jana Alhamisi). Yeye amekuja kwa ajili ya kuwa msaidizi na vilevile atasaidiana na Zahera pamoja na Noel Mwandila raia wa Zambia ambaye yeye yupo hapa muda mrefu.

“Yeye (Guy Bukasa) amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kufundisha hapa na atakuwa sehemu ya timu ambayo inajiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Gor Mahia. Ujio wake umependekezwa na kocha Zahera kwa sababu wao wamewahi kufanya kazi wote huko nyuma,” kilisema chanzo hicho.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV