Uwezo wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Mzambia, Clatous Chama umewafurahisha mashabiki wengi wa soka, lakini Jonas Mkude amekiri kwamba mchezaji huyo anajua sana na atakachofanya ni kujenga naye ushirikiano mzuri kwani anaamini hawatazuilika.
Mkude amesisitiza kwamba akisimama na Chama ndio watakuwa viungo bora zaidi nchini. Mzambia huyo alionyesha vitu vyake wakati Simba ikitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Asante Kotoko ya Ghana, Jumatano iliyopita kwenye mechi ya Simba Day.
Ufundi mkubwa wa kupiga pasi, kumiliki mpira, kuanzisha mashambulizi lakini pia kuituliza timu pindi inapokuwa ikishambuliwa, ndiyo sababu kubwa ambayo imemfanya awe gumzo zaidi.
Katika mechi hiyo ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Chama alionekana kushirikiana vilivyo na viungo wenzake Jonas Mkude na James Kotei katika kupanga mashambulizi na kuwatengezea nafasi za kufunga washambuliaji, Mganda, Emmanuel Okwi pamoja na Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Mkude ameliambia Spoti Xtra kuwa; “Chama ni mchezaji mzuri ambaye kila mtu aliona uwezo wake tulipocheza na Asante Kotoko kwa hiyo binafsi sina wasiwasi naye kwani ana kila kitu kinachohusiana na soka.”
“Naamini kama tutacheza kwa pamoja muda mrefu na kuzoeana naamini hakuna timu itakayokuwa na kiungo bora kama sisi, jambo kubwa ni Wanasimba wote kuwa kitu kimoja na kuendelea kutuunga mkono, naamini kwa kufanya hivyo msimu ujao tutafika mbali zaidi.”
Kocha wa Dodoma FC ambaye ana mapenzi na Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema kuwa; “Chama ana vitu vya kipekee na washambuliaji watafunga sana kama siku ile alipiga pasi kama sita za hatari lakini Okwi alishindwa kufunga.”
0 COMMENTS:
Post a Comment