August 12, 2018




NA SALEH ALLY

Pamoja na kwamba ilionekana kama haina uwezo sana, Manchester United imeanza Ligi Kuu England msimu wa 2018/19 kw aushindi.


Pamoja na hivyo, bado imekuwa hivi; Kocha Jose Mourinho anachukuliwa kama kocha mchovu si kama yule anayejulikana na wengi wanaamini hana tena nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England ‘Premier League’. 

Hisia hizi zimekuwa wazi, watu wengi wataalamu wa michezo na hata mashabiki wanaamini hivyo hasa kwa kuwa Manchester United haikuwa na usajili wa mbwembwe sana kama klabu nyingine kubwa.

Ukimya wa Mourinho unaonekana kuwafanya wengi waamini sasa hana tena nafasi ya kufanya vizuri. Inaonekana Pep Guardiola ndiye mwenye nafasi kubwa kwa kuwa msimu uliopita, alitwaa ubingwa kwa jumla ya pointi 100.

Wakati Manchester United ya Mourinho ilimaliza katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 87. Hivyo hakuna wa kumzuia Guardiola na akitokea, basi nafasi kubwa inasukumwa kwa Jurgen Klopp raia wa Ujerumani anayekinoa kikosi cha Liverpool.

Kimjadala Liverpool inaonekana iko fiti au bora zaidi. Hii inamfanya Mourinho atoke katika nafasi ya chaguo la pili kuwa bingwa hadi nafasi ya tatu, tena kama mambo yatamuendea vizuri.

Ukiangalia kiufundi unaona Mourinho bado ni hatari sana kwa makocha wengine na nafasi ya kutwaa ubingwa unaweza kusema ni kati ya makocha watatu wenye nafasi hiyo lakini yeye anakaa katika zile mbili za juu.

Yaani, kama atakwenda kwa uhakika hesabu zake zikikubali, ana nafasi ya kuwa bingwa. Akikosea bado anaonekana ni vigumu kumuondoa nafasi ya pili. Hivyo Manchester City au Liverpool watakuwa na kazi kubwa.

Baada ya kushika nafasi ya pili msimu uliopita, inaonekana wazi Mourinho hawezi kukubali kufanya hivyo tena msimu mpya. Si vibaya kusema msimu huu utakuwa ni mwamuzi wa mwisho kwa maisha ya Mourinho England.

Maana kama atafanya vizuri, basi atakuwa amejihakikishia kukaa na kutaka kuendelea kufanya kazi na Manchester United lakini kama ataboronga, safari itamkuta, iwe kwa kuchagua yeye au waajiri wake.

Mechi 10 za mwanzo zina nafasi kuu ya kujua mwenendo sahihi wa Mourinho ingawa kila mmoja anapaswa kukumbuka karibu kila nchi aliyobeba ubingwa wa ikiwemo England, alianza kwa kuteleza na alipoziba pengo aliloona lina tatizo, ubingwa haukuwa na maswali tena.

Kama ataukosa safari hii, maana yake ile plani yake iliyozoeleka itakuwa imefeli na inawezekana ikawa mwisho kurudi na kusimama vizuri tena kama ambavyo aliwahi kufanya.

Ambacho wengi wanapaswa kukumbuka, Mourinho ni kocha mwenye uwezo na mbinu ya ubebaji makombe kwa kuwa inathibitishwa na zaidi ya makombe 10 aliyowahi kubeba. Kwamba ni kocha anayejua nini afanye kuwa bingwa.

Mechi hizo 10 zinaweza kuwa ndiyo dira ya Mourinho, kwamba amefanya vipi, vizuri au la! Atafungua Ligi Kuu England akiwa nyumbani na Leicester na wiki inayofuata atasafiri kuwavaa Brighton na baadaye atarejea nyumbani kucheza na Tottenham kabla ya kwenda ugenini mechi mbili dhidi ya Burnley na Watford.

Utaona mechi zake tano za mwanzo hazina vigogo isipokuwa Tottenham ambayo ni mechi ya tatu. Kama atafanikiwa kushinda zote tano, atakuwa amepita juu ya timu nne sumbufu na kigogo mmoja. 

Lakini atakuwa amepata nafasi ya kutengeneza ubora kwa kuwa mechi tatu za ugenini atakuwa ameshinda.

Fungu la pili linalotengeneza mechi nyingine tano, litaanza Septemba 22 dhidi ya Wolverhampton, Mourinho akirejea nyumbani tena, halafu atakwenda jijini London kuwavaa West Ham United, atarejea Old Trafford kucheza na Newcastle United kabla ya kurejea tena London kuwavaa Chelsea na Oktoba 27, watamalizana na Everton FC inayodhaminiwa na SportPesa.

Katika fungu la pili unaona hakuna tofauti kubwa kwa kuwa ndani ya timu tano kuna mechi nyingine ya kigogo Chelsea na Man United watakuwa ugenini.

Kama atafanikiwa kutengeneza ushindi kwa asilimia 90 katika mechi hizo za mwanzo za ligi. Maana yake itakuwa vigumu sana kumzuia Mourinho kwa kuwa kikosi kitajenga hali ya kujiamini na yeye atakuwa imara kujenga mwendelezo sahihi.

Ubora wa ulinzi kwa Mourinho ni jambo linalojulikana. Msimu uliopita alishika nafasi ya pili kwa ubora akiwa ameruhusu mabao 28 na Man City waliongoza wakiwa wamefungwa mabao 27.

Kwa kikosi chake alivyokisuka akitumia jumla ya Euro milioni 82.7. Lazima kitakuwa na sababu ya kuwashangaza wengi ambao hawakizungumzii na kama atapatia katika mechi hizo 10 hadi Oktoba 27, kumkamata, itakuwa kazi ngumu sana.


MANCHESTER UNITED 2018/19
AGOSTI 11:  Leicester City (N)
AGOSTI 18: Brighton (U)
AGOSTI 25: Tottenham (N)
SEPTEMBA MOSI: Burnley (U)
SEPTEMBA 15: Watford (U)
SEPTEMBA 22: Wolverhampton (N)
SEPTEMBA 29: West Ham UTD (U)
OKTOBA 6: Newcastle United (N)
OKTOBA 20: Chelsea (U)
OKTOBA 27: Everton (N)


1 COMMENTS:

  1. kati ya timu zinazopewa nafasi ya kushinda ubingwa wa EPL msimu huu ni Man city, Liverpool, Man UTD na totteinham... inakuaje unasema haina uwezo sana? timu ambayo mmeitoa ktk mbio za ubingwa na haina uwezo ni Chelsea na Arsenal kwanini usiziongelee hizo unaitaja Man U? acha ushabiki ongelea mpira!!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic