September 5, 2018


Kufuatia kushindwa kununuliwa kwa makontena 20 yanayotajwa kuwa ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambayo yanapigwa mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mara ya pili, hali hiyo imeibua gumzo baada ya kufananishwa na nyumba za mfanyabiashara, Said Lugumi ambaye naye nyumba zake zinasumbua kwa kutonunuliwa.  

Kati ya nyumba zake tatu zilizokuwa zikipigwa mnada tangu mwaka jana mpaka sasa ni nyumba moja tu iliyopo Mbweni jijini Dar ndiyo iliyopata mteja.

Baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba makontena hayo yamekosa wateja kutokana na kuwa ghali ukilinganisha na mali zilizopo ndani. Mfanyabiashara Athumani Iddi amedai kwamba mali hizo huenda zimekuwa zikikosa wateja kutokana na kuogopwa kwa wanaozimiliki ambao ni Makonda na Lugumi.

Kufuatia hali hiyo mwandishi wetu alizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali Yono, Scholastica Kivela, ambayo imepewa kazi ya kuuza mali hizo ambazo zimekuwa zikisuasua kuuzika. Akizungumza na Uwazi Jumapili iliyopita, Kivela alisema mali hizo zinaendelea kuuzwa ambapo katika mnada uliofanyika Jumamosi iliyopita waliuza vitu vingi vya watu wengine lakini makontena ya Makonda wateja walishindwa kufika bei.

“Katika mnada tuliofanya Jumamosi tuliuza vitu vingi sana yakiwemo magari na vitu vingine vya thamani lakini ukweli hayo makontena ya Makonda bado hayajapata mteja. “Wakati tukiyanadisha wateja walikuwa wakifika bei kwenye shilingi milioni 10 mpaka 15 wakati lengo letu lilikuwa ni kuyauza shilingi milioni 60, hivyo bado hayajapata mteja.”

Akizungumzia kupunguza bei ya makontena hayo ili yapate wateja, Scholastica amesema hilo ni jukumu la Serikali, ikiona hayauziki ni jukumu lake kukaa na kufikiria kupunguza bei. “Kama hayatauzika kwa bei hiyo, hilo ni jukumu la Serikali kukaa na kutafakari kuyapunguza bei maana sisi kazi yetu ni kupiga mnada tu kwa bei elekezi,”alisema.

Kuhusu suala la wateja kuogopa kununua makontena hayo kwa kumuhofia Makonda na zile nyumba za Lugumi nazo kubuma kuuzika alisema; “Kama hao wateja wanaogopa kununua hayo makontena na nyumba za Lugumi kwa kuwahofia wenyewe hayo ni mawazo yao finyu, nawaomba wasiwe na mawazo hayo kwa kuwa mnada huo unafanyika kwa baraka za Serikali, hivyo nawatoa hofu wateja wenye mawazo ya kuhofia kununua mali hizo.

“Waje wanunue na watakuwa salama kabisa na hizo mali zao.” Na kuhusu nyumba za Lugumi alisema zilikuwa tatu moja ipo pale Upanga na nyingine mbili zipo Mbweni, moja imeshapata mteja, tuliiuza kwa zaidi ya shilingi bilioni moja, hivyo tunawakaribisha wateja waje wasiogope kuja kwenye mnada,” alimaliza kusema Scholastica.

Mnada wa Makontena ya Makonda ulifanyika katika bandari kavu ya Malawi Cargo na wanunuzi walitakiwa kuwa na vitambulisho, leseni ya gari na hati ya kusafiria. Makontena hayo yanapigwa mnada baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuagiza yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

 Mbali na Makonda mwenyewe kutoridhia uamuzi huo wa Serikali, tayari Rais Dk. Magufuli amesema sheria za nchi zinasema wazi kuwa ni mtu mmoja tu katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.

Mtu huyo ni waziri wa fedha na mipango. Magorofa ya Lugumi nayo yanauzwa na Kampuni ya Udalali ya Yono baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic