September 30, 2018


Gumzo la leo Jumapili kila kona ya Tanzania ni Simba na Yanga. Kila sehemu ni rangi za njano na nyekundu, lakini mwisho wa siku mwamuzi mwanamama, Jonesia Rukyaa ndiye atakayesimama kati kuamua nani ashinde.

Ndiye ambaye dunia nzima itakuwa ikimtazama ingawa si mara yake ya kwanza kuchezesha mechi ya watani wa jadi hii ni ya tatu.

Tunakuchambulia mambo kadhaa ya Jonesia ambaye kutajwa kwake katika mchezo huo kulisababisha gumzo hasa kuhusu kama ataweza kuumudu mchezo huo kwa hali ya ushindani wa sasa? Maswali hayo yanatokana presha ya mchezo huo hasa kipindi hiki ambacho Simba na Yanga zote zina mzuka.

ALIZALIWA MWAKA 1988

Jonesia alizaliwa mwaka 1988 na pia ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera na muda mwingi huwa anakuwa huko hata wakati anatangazwa kuamua mechi ya leo alikuwa mazoezini.

ANAISHI NA BIBI YAKE

Taarifa ambazo gazeti hili linazo ni kuwa Jonesia anaishi pamoja na bibi yake, wazazi wake wapo lakini haishi nao wako kivyao ingawa anawatunza.

NI MFANYABIASHARA

Nje na mchezo wa soka, binti huyo ni mfanyabiashara na biashara zake zipo Kagera. Anajihusisha na maduka, saluni na kilimo.

MTANI JEMBE PIGO LA KWANZA

Mechi yake ya kwanza kubwa kuchezesha tangu alipoanza fani hiyo ilikuwa ni ya Mtani Jembe ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa iliyopigwa Desemba 13, 2014.

Yanga ilifungwa mabao 2-0, mchezo huo ulianza kwa presha kubwa na almanursa umshinde katika dakika za mwanzo lakini baadaye alitulia na kuumudu mpaka mwisho. Mechi ya pili, Yanga akashinda mabao 2-0 kwenye ligi msimu 2015/16.

KIGOGO ALIMTISHIA MAISHA

Mmoja wa vigogo wa Mtibwa aliwahi kumtishia maisha msimu wa 2015/16 baada ya kuchezesha mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Ruvu Shooting, mwaka huo, alidai ameinyonga timu yao. Gazeti hili lilionyeshwa SMS na jina la kigogo huyo, taarifa hizo zilifika TFF lakini suala hilo likamalizwa kishikaji.

ATISHIWA TENA

Msimu huohuo wa 2015/16 baada ya kuchezesha mchezo wa Stand United dhidi ya Azam FC, mwamuzi huyo alitishiwa na kiongozi mmoja kwa madai ya kuipendelea timu moja kati ya hizo.

REKODI YA MWAMUZI MDOGO

Alipochezesha mechi ya Nani Mtani Jembe kipindi kile aliweka rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kuchezesha mechi hiyo ya wapinzani pia kuwa mwamuzi mdogo zaidi kupewa beji ya Fifa nchini aliyoipata wiki kadhaa baadaye.

KOCHA ALIMSIFIA

Katika hali ya kushangaza, wakati makocha wengi wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi kila mechi, Kocha wa Jackson Mayanja aliyekuwa anainoa Coastal Union, alisifia uwezo wa Jonesia pamoja na waamuzi wenzake mara baada ya mchezo dhidi ya Simba ambapo Coastal ilifungwa bao 1-0, Oktoba, 2015. Kipindi hicho wengi walimponda.

FAINALI ZA AFCON

Mwaka jana alichezesha fainali za Afcon kwa wanawake nchini Cameroon na amewahi kuwa mwamuzi bora wa Bara.

BADO YUPOYUPO


Spoti Xtra liliwahi kumuuliza mwamuzi huyo juu ya maisha yake ya ndoa, alijibu kwa ufupi tu kuwa: “Sijaolewa.” Uchunguzi unaonyesha kuwa mpaka sasa bado hajaingia katika ulimwengu huo wa wapendanao uliounganishwa na Mungu.

Kutoka Spoti Xtra

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic