October 19, 2018


KESHO Jumamosi mapema tu saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika Mashariki, Chelsea itakuwa mwenyeji wa Manchester United ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu England.

 Katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, mwamuzi atakuwa Mike Dean. Wachambuzi wengi wa soka wanautazamia mchezo huo tofauti.

 Wengi wanaona unaweza kuwa wa mwisho kwa Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho. Mourinho amekuwa njia panda na kibarua chake ndani ya kikosi hicho hali ambayo inawafanya wengi waamini kwamba akipoteza mchezo huu atakuwa hatarini zaidi. 

Hivi karibuni taarifa zilivuma kwamba atatimuliwa haraka, lakini akaja kupona baada ya mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Newcastle United kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. 


Katika mchezo huo, mpaka kipindi cha kwanza United walikuwa nyuma kwa mabao 2-0, lakini dakika tisini wakashinda 3-2. Baada ya mchezo huo, kukawa na mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, sasa ligi zinaendelea na kesho ndiyo Mourinho atakuwa na kibarua hicho. 


Beki wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa Kituo cha Sky Sport, Jamie Carragher, amesema: "Ilikuwa vizuri kwao kwenda kwenye mapumziko wakiwa na pointi tatu. Kwa jinsi walivyoibuka na ushindi hakuna ushindi mzuri zaidi kama wa kutokea nyuma.


"Ni mtihani mwingine kwa Mourinho kuhakikisha kwamba anaendelea kusalia kuinoa timu hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa za kutimuliwa kwake, lakini pia hata kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri pia anatakiwa kudhihirisha ubora wake." Huu utakuwa ni mchezo wa 180 kwa timu hizo kukutana katika michuano yote.

 Chelsea imeshinda 54, Man United 77, sare zikiwa 49. Mara ya mwisho kukutana timu hizo, Chelsea iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa Kombe la FA msimu uliopita. Katika Uwanja wa Stanford Bridge, mara ya mwisho Chelsea iliifunga Man United bao 1-0. 


Hiyo ilikuwa msimu uliopita, lakini mara ya mwisho kukutana kwenye ligi, Man United iliibuka na ushindi wa maba 2-1. 


Ikumbukwe kuwa, Chelsea inaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya pili ikijikusanyia pointi 20 sawa na kinara Manchester City na Liverpool inayoshika nafasi ya tatu, huku Man United ikishika nafasi ya nane ikiwa na pointi 13.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic