SUALA LA WAAMUZI LIGI DARAJA LA KWANZA NA MDHAMINI YATAFUTIWE UFUMBUZI
MENGI ambayo tunatarajia kuyaona kutoka timu za Ligi Kuu Bara, yanaanzia Ligi Daraja la Kwanza ambapo huko ndipo timu zinatengeneza msingi wa baadaye kuja kupanda daraja na kushiriki ligi kuu.
Tayari tunaendelea kushuhudia namna ambavyo ushindani unavyozidi kukua. Ligi Daraja la Kwanza timu nyingi zimedhamiria kupanda daraja ili kuweza kushiriki ligi kuu msimu ujao.
Kila kitu kinawezekana, kikubwa ni mipango kwa timu kuhakikisha inafikia malengo yake. Ikifanikisha kwa hilo, hakuna kitakachoshindikana.
Mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu wakishirikiana kwa pamoja, wanaweza kuisaidia timu yao kufikia malengo.
Kikubwa ambacho kipo kwa sasa kwenye Ligi Daraja la Kwanza ni mambo ambayo Kamati ya Mashindano, Kamati ya Waamuzi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuyatazama kwa jicho la kipekee na kuondoa dosari zilizopo.
Jambo ambalo limekuwa ni wimbo hasa kwa timu nyingi ni suala la waamuzi kuzibeba baadhi ya timu ambazo zinacheza michezo yao kwenye viwanja vya nyumbani kwa kulazimisha kupata ushindi kwa njia ambazo si halali. Hii haipendezi kwa maendeleo ya soka.
Waamuzi wanapaswa wazingatie sheria 17 za soka katika kuamua mchezo bila kujali ni nani ambaye yupo nyumbani ama kuonyesha dalili ambazo sio nzuri.
Suala la lawama kuzidi kuwa nyingi kwa waamuzi linapaswa liangaliwe na kutafutiwa ufumbuzi haraka kabla halijawa sugu. Ikumbukwe kuwa timu ambazo zinafanikiwa kupanda daraja zinakuja kushiriki ligi kuu ambako ushindani wake unakuwa si wa mdogo.
Hivyo kama itatokea timu inapanda kwa kubebwa itafanya iwe ni daraja la kupitisha ushindi kwa timu nyingine na itakuwa ikifungwa tu mpaka inashuka daraja na kurudi ilipotoka ianze upya.
Ili kuweza kupata timu nzuri na za ushindani kwenye ligi kuu, ni lazima upatikanaji wake uwe halali, tabia ya kupanga matokeo na kubebana hautakiwi, kila mmoja apambane na hali yake kuhakikisha anafanikiwa kushinda.
Wakati hayo yakijitokeza, pia suala la mdhamini bado ni tatizo kwa Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu Bara. Kuna umuhimu kwa wadau mbalimbali kuweza kujitoa kuwekeza udhamini wao kwenye ligi hizo ambazo ni msingi mkubwa wa soka la nchi hii.
Ipo wazi kwa sasa baadhi ya timu zimekuwa zikipata tabu kusafiri kwenda mikoa mingine kucheza mechi zao kutokana na kukosa fedha.
TFF wanapaswa wayape uzito pia mashindano haya kwa kuanzia namna ya kuyatangaza kwa wana jamii na mashabiki ili kuwa karibu na jamii ambayo kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuamua kutoa sapoti.
Kwa kukaa karibu na wadau itasaidia kuweza kuona vipaji ambavyo vipo Ligi Daraja la Kwanza pamoja na kuwavutia wawekezaji kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye mashindano haya ambayo yana msisimko wa pekee.
Kila kitu kinawezekana endapo umakini katika kufuatilia haya masuala utawekwa kwani wengi wanachukulia mashindano haya kama kitu cha mzaha ilihali tunatambua tunataka kuwa na soka la ushindani.
Mwendelezo mzuri wa kuweza kuwekeza Ligi Daraja la Kwanza itasaidia timu kupanda daraja zikiwa zimejiandaa vizuri, zile ambazo zitaleta ushindani na kupata wadhamini wanaweza kupanda na wadhamini mpaka ligi kuu.
Kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza makali ya uendeshaji wa timu kama ambavyo tunashuhudia, baadhi ya timu ligi kuu zinahangaika kutafuta fedha za kuweza kujiendesha kwa kuwa hakuna mdhamini mkuu wa ligi.
Tumeona baadhi ya timu zikishindwa k u m a l i z i a mishahara kwa wachezaji wake hata kwenye ligi kuu na zipo ambazo zimeshindwa kurejea baada ya kuweka kambi mikoani na kuamua kuanza kupitisha bakuli ili ziweze kujitoa katika tatizo hilo.
Sasa hali hii endapo litaendelea kwa muda mrefu mambo yatazidi kuwa magumu kwa baadhi ya timu ambazo hazina hata mdhamni mmoja ligi kuu inaanza kuleta wasiwasi kwa kuwa muendelezo wake utakuwa na matokeo mabaya.
Matokeo ya mwanzo huu hapo baadaye kama mdhamini hatapatikana ni kwamba kuna timu ambazo zitashindwa kusafiri kwa kukosa fedha za kwenda mkoa mwingine, kuna wachezaji wataanza kufanya migomo ya chini kwa chini kushinikiza walipwe mishahara yao.
Ikifika hatua hii ushindani utakuwa kwa timu chache ambazo zinaweza kumudu gharama za uendeshaji hali itakayopoteza mvuto ambao upo kwa sasa kwenye ligi na utafanya ligi kupoteza kabisa mvuto hivyo wadau wa soka muda wa kuokoa soka letu ni sasa.
18 ZA CHINGA ONE, CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment