ISHU YA WAMBURA NA KARIA TFF YAWATETEMESHA VIGOGO WAKUBWA
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeingiwa na mchecheto na kushindwa kufafanua ishu ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa shirikisho hilo Michael Wambura ambaye mahakama imeamuru arudi ofisini.
Mahakama Kuu imetengua maamuzi ya Kamati ya Maadili ya kumfungia kifungo cha maisha cha kutojihusisha na soka kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Maadili ya TFF ilitangaza kumfungia Wambura kutokana na kukutwa na makosa matatu, ikiwemo kuchukua fedha za TFF ambazo ni za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
Pili ni kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEMS LIMITED huku akijua malipo hayo siyo halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.
Na Tatu, ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho hilo ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015.
Rais wa TFF, Wallace Karia amesema; “Siwezi kulizungumzia suala la Wambura ambalo lipo katika vyombo vya sheria, msikilizeni na muandike vile anavyosema.” “Lakini itakapofika muda wa sisi kuweza kuzungumza tutazungumza kwa kuvitaarifu vyombo vya habari lakini kwa sasa suala hilo siwezi kulisemea,” alisema Karia.
Aidha kwa upande wa Wambura alipotafutwa kuzungumzia iwapo kuna taarifa yeyote aliyoipata kutoka TFF baada ya kuwasilisha shauri hilo, alisema kuwa; “Mimi nimeshapeleka shauri langu na nimeshazungumza sana kuhusiana na suala hilo kilichobakia ni wao kufanya utekelezaji kwani shauri linatakiwa kujibiwa haraka.
“Kama haitatekelezeka haraka inabidi turudi mahakamani kueleza na itakuwa ni kosa la jinai na shauri linatakiwa kutekelezeka haraka na haijatolewa muda maalumu,” alimaliza. Lakini Kiongozi wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amewataka viongozi wa TFF kulichukulia kwa umakini suala hilo kwani linaweza kuleta shida endapo mabavu yakitumika na Simba na Mtibwa zikafungiwa kushiriki michuano ya kimataifa.
CHANZO: SPOTI XTRA
0 COMMENTS:
Post a Comment