December 25, 2018



NA SALEH ALLY 

YANGA imekwenda kwa muda mrefu sana bila ya kukaa katika mwongozo ambao ulikuwa sahihi kwa maana ya mwendo wa kiungozi.


Uongozi wa Yanga umeyumba, umekuwa ni ule usiokuwa na mpangilio sahihi kwa kuwa tu viongozi wake kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu hawakuwa katika wakati mzuri.


Kumbuka Mwenyekiti Yusuf Manji, ndiye alianza kuingia katika misukosuko ya kimaisha. Akaamua kuomba kupumzika, hasa baada ya maelezo yake kwamba daktari alimtaka apumzike.

Kaimu wake, alichukua gurudumu, kumbuka baada ya muda fulani, naye aliingia kwenye wakati mgumu hadi baadaye akaamua kutangaza kujiuzulu nafasi yake ambayo ilibaki wazi pamoja na ile ya mwenyekiti.

Mtendaji mkuu wa klabu ni katibu mkuu. Wakati huo alikuwepo gwiji la Yanga, Charles Boniface Mkwasa ambaye bahati mbaya akaugua mwisho akachukua uamuzi wa kupumzika na siku chache baadaye akasafirishwa kwenda India kwa matibabu.

Ukiangalia hadi sasa nafasi za Yanga zimekuwa ni zile ambazo ‘zina makaimu” tu. Si wale waliochaguliwa na unaweza kujiuliza kwa nini Yanga hawajafanya uchaguzi?

Swali hili limezunguka kwa kitambo sasa hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipoamua kutumia kamati yake ya uchaguzi kuitisha na kusimamia uchaguzi huo.

Awali nilikuwa ninajiuliza kwa nini TFF imeamua kulisimamia suala hilo kupitia kamati yake wakati Yanga wanayo ya kwao na wangeweza kufanya wenyewe. Lakini lile swali langu la kwa nini Yanga hawana viongozi waliochaguliwa lilikuwa halijapata jibu.

Baadaye nikaona hakukuwa na tatizo Yanga kufanya uchaguzi kwa kusaidiwa na TFF katika usimamizi lakini lingekuwa jambo jema uchaguzi huo, kamati ya Yanga nayo ishirikishwe.

Wanachama wa Yanga wamekuwa wakilalama kuhusiana na uchaguzi huo na baadhi kuuona kama si sawa kwa kuwa mwenendo wake wa usimamizi hauonyeshi kama ni uchaguzi hasa wa Yanga, hasa kihisia.

Ukiangalia kwa uhalisia, unakuwa uchaguzi sahihi wa Yanga kwa kuwa wagombea na wapiga kura watakuwa wanachama wa Yanga. Hapo kinachokosekana ni uelewa sahihi na wingi wa nguvu.

TFF na hata serikali naona kama inatumia nguvu nyingi sana badala ya mwendo mzuri wa kuelewana na kuelezana ambao siamini kama umeshindikana.

Wanachama wa Yanga wanaweza wakawa hawajaelewa hasa kinachoendelea. Hawana uhakika wa wanachokisikia na inawezekana kuna wale wanaowaaminisha tofauti kwa kuwa tu hawafaidiki na uchaguzi huu.

Hivyo serikali inaweza kupitia katika njia nzuri na kuendelea kufafanua kwa kuwapa elimu na faida za kuhakikisha viongozi wanapatikana.

Wanachama wanaweza kuachana na ile hadithi ya Manji kwanza. Lakini wanaweza pia kuepushwa na maneno wanayojazwa, ila hakuna ubishi lazima waelezwe vizuri, wafafanuliwe na kudadavuliwa vitu baada ya kuambiwa kibabe au kulazimishwa tu.

Ukiwa mkubwa si lazima uzungumze kibabe ndio usikike. Wakati unapozungumza kwa ufafanuzi bora na maelezo ya kutosha inaweza kusaidia. Vizuri kueleweshana maana itawasaidia hata watakaoshinda kwenye uchaguzi kupata ushirikiano.

Nilisikia wako wanaopotosha uchaguzi, binafsi sina uhakika. Lakini kama ni hivyo, siamini wanaopotosha watakuwa wanafanya hivyo kwa maslahi ya Yanga. Inawezekana kabisa ni maslahi ya matumbo yao na ubinafsi wao.

Kama ni hivyo, basi wabadilike na kuisaidia Yanga ambayo imeishi maisha ya kubahatisha kwa muda sasa na chanzo ni hicho, kuyumba kwa uongozi kutokana na watu kujiondoa lakini ile ya ubinafsi ambayo inatokana na wanachama kadhaa kujiangalia wao.

Inawezekana wamekuwa wakifaidika na uchaguzi na huu hauna faida kwao. Basi vizuri wakaangalia faida zaidi za klabu yao, halafu wao watafuatia.






4 COMMENTS:

  1. Serikali wafanye jitihada gani tena kwa yanga? Yanga ameshaonana mara kadhaa na waziri husika kistaraabu kabisa ila hao Yanga kama wamerogwa. Kama tatizo ni Manji basi Manji hayupo vizuri kwa sasa na kunako uhai Manji atakuwepo ila la kufanaya Yanga kwa sasa ni kuchagua viongozi watakaokuwa na zamana ya kuisimamia timu katika kipindi hiki cha mpito ili kujenga misingi ya kuiwezesha timu kutafuta wazamini zaidi au hata kuingia katika mfumo wa hisa.

    ReplyDelete
  2. hawa viongozi waliopitishwa kugombea na TFF KIBABE ndio watakuja kuimaliza YANGA tuombe uhai tu tutakuja kuona siku za mbele na Serikali kama ina nia nzuri na YANGA basi watumie hekima kusimamisha uchaguzi huu wa kibabe

    ReplyDelete
  3. Yanga kuweni wepesi hata kuiga watani zenu
    ....mfano mwezi february ni kumbukumbu ya kuzaliwa klabu ya yanga iteni mechi ya kimataifa ya kirafiki na chezeni mechi ya kimataifa na klabu kongwe moja ya Afrika au Ulaya katika uwanja wa Taifa mjaze uwanja siku hiyo fanyeni umahasishaji nchi nzima na matendo ya fadhila katika jamii waalikeni mabalozi waasisi wa uhuru wa Tanganyika walio hai na wa mapinduzi ya Zanzibar ipigwe dua jangwani....halafu wachezaji watembelee hospitali na kutoa misaada, na pia uwanja wa Taifa kuwe na burudani mbalimbali halafu jioni muujaze uwanja....mtapata fedha nyingi tu

    ReplyDelete
  4. basi acheni Mo aondoke halafu tuone simba wakijikimu kupitia hayo matamasha yao

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic