Kuelekea kwenye mchezo wa Ligi kuu utakaochezwa kesho kati ya Yanga na Biashara United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu, ataukosa mchezo huo huku mashine mbili zikiongezwa ndani ya kikosi.
Ajibu amekuwa na mwanzo mzuri kwa sasa kwenye ligi akihusika kwenye mabao 14 kati ya 27 ya kikosi hicho ambacho kimefanikiwa kuweka rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja kati ya 14 waliyocheza.
Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh amesema tayari kikosi kimeanza mazoezi kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Biashara United, wanatambua utakuwa na ushindani na kuwasihi mashabiki wajitokeze kwa wingi.
"Mchezaji wetu Ibrahim Ajibu hatakuwa sehemu ya kikosi kwa kuwa amepatwa na msiba wa ndugu yake hivyo tumempa ruhusa na Mrisho Ngasa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu,".
"Wachezaji wengine ambao tayari wamesharejea kwenye kikosi na wameanza kufanya mazoezi ni pamoja na Papy Tshishimbi, Gadiel Michael ambao walikuwa majeruhi, hivyo tunaamini tutaendelea kufanya vizuri kwenye ligi," alisema.
Biashara United wamecheza michezo 14 kwenye ligi na kushinda mchezo mmoja na wamepoteza michezo 6 na kutoa sare michezo 7 wamejikusanyia pointi 10 wakiwa nafasi ya 20 watamenyana na Yanga ambao wapo nafasi ya kwanza.
0 COMMENTS:
Post a Comment