Na Saleh Ally
KILA mtu ana haki ya kutoa maoni lakini bado kabla ya kutaka kulizungumzia jambo unaweza ukajifunza ili kupata uhakika wa mambo.
Mazungumzo yamejengwa katika njia nyingi tofauti na unapozungumza ishu inayohusiana na kumlaumu mtu, hii ndiyo inahitaji zaidi kujifunza kabla.
Watalaamu wanasema, kusikiliza ni silaha kubwa kuliko kuzungumza kwa kuwa ukisikiliza, utaweza kuzungumza vizuri hasa katika ujenzi wa hoja kuliko ukiwa unazungumza tu bila ya kuwa msikivu kwanza.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alipanga kikosi chake namba moja katika mechi nzuri na ya kuvutia ya Kombe la Mapinduzi wakati mabingwa hao wa Tanzania Bara walipowavaa KMKM.
Simba ilishinda kwa bao 1-0 katika mechi hiyo hiyo, mfungaji akiwa kinda Rashid Juma. Kikosi cha Simba kilikuwa kile kinachocheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ilikuwa mechi nzuri kwa kuwa ilikuwa na nguvu na ufundi mwingi sana. Mpira uliochezwa ulionekana na kuifanya mechi kuwa moja ya zile bora za michuano hiyo msimu huu.
Pamoja na Simba kushinda, hali imeonekana kuwaudhi mashabiki ambao wanalala kutokana na kuumia kwa kiungo mkabaji Erasto Nyoni.
Nyoni aliumia katika mchezo huo baada ya kugongwa na Hafidh Mohammed “kokoy’ wa KMKM. Sasa atakosa mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa hatua ya Makundi dhidi ya JS Saoura na inawezekana wiki moja zaidi akawa nje ya uwanja akiendelea kupata matibabu ya goti.
Ukiangalia matibabu, atakapopona aanze mazoezi taratibu hadi atakaporejesha fitnesi yake, hakuna ubishi ni wiki mbili hadi tatu. Jambo hili kwa Wanasimba limegeuka kero.
Ajabu zaidi, wamekuwa wakimuangushia mzigo kocha Aussems raia wa Ubelgiji kwamba aliamua kupanga kikosi kamili katika Kombe la Mapinduzi huku akijua mashindano hayo si muhimu.
Mbaya zaidi nimeona hadi wale wengi wanaamini ni watalaamu wakiingia katika mkumbo huo. Inawezekana ni mawazo ya kimhemko au yanayounganisha ushabiki wa mtu fulani.
Kiuhalisia, si sahihi. Aussems hapaswi kulaumiwa na alikuwa sahihi kabisa kumtumia Nyoni na wachezaji wengine wa kikosi cha kwanza katika mechi hiyo.
Suala la kuumia, mtu anaweza kutokewa nalo hata mazoezi, au akiwa anakimbia na kadhalika. Hivyo si ajabu mchezaji kuumia na kuukosa mchezo.
Kikubwa ni kujiuliza, kwa nini Aussems aliamua kuwatumia wachezaji hao zikiwa zimebaki siku tano kabla ya mchezo ambao kwake ni muhimu sana?
Nyoni ni injini ya Simba katika ulinzi. Alikuwa lazima acheze mechi hiyo kama walivyocheza wachezaji wote kwa ajili ya “match fitness”. Hii ni pasha misuli kiushindani kabla ya mechi kubwa na wachezaji wanatakiwa kufanya hivi.
Ndani ya siku tano, wanatakiwa kucheza mechi au mazoezi ya kiushindani sana ili kujitengenezea usahihi wa miili yao kimwili na akili kabla ya mchezo.
Mchezaji kabla ya kuingia lazima apashe misuli na kocha hupasha akili yake kwa maelekezo. Mchezaji pia hawezi kuandaliwa na mechi akifanya mazoezi tu kila siku kwa siku nane tisa.
Lazima awe ana mechi kama hiyo ya KMKM au wacheze kwa wenyewe, “mechi mazoezi” ambayo ukiishuhudia unaweza kudhani wanatoana roho.
Hii ni kutengeneza utayari wa upambanaji katika mechi inayosubiriwa kwa hamu. Hivyo ni lazima kuwe na “match fitness” kabla ya mechi ngumu na muhimu na hasa kwa zile mechi ambzo zina ligi fupi, ambayo ni makundi au ingekuwa ya mtoano.
Nafikiri umewahi kuona mara nyingi kunakuwa na mechi za kirafiki, makocha wanalazimika kufanya hivyo wakati wanaelekea kucheza mechi ngumu ya mashindano hasa katika kipindi ambacho wanaona watakaa sana wakifanya mazoezi bila ya kuwa na mechi.
Hivyo, Aussems alifanya jambo la kitalaamu ambalo linaeleweka. Ndiyo maana hauwezi kuona akiwatumia tena wachezaji wake wa karibu hiyo katika mechi nyingine ya Kombe la Mapinduzi labda hadi baada ya mechi ya Waalgeria hao.
Jambo zuri kama hatuelewi, vema kujifunza. Pia jiulize kama kweli ulikuwa haujui kweli Aussems anaweza kufanya jambo ajishambulie mwenyewe bila sababu ya msingi!
Aidha, kwa mashabiki wajue hivi; hata katika mechi ya mashindano au mazoezini, kuumia ni jambo la kawaida na kutokea kwake ndiyo maisha yenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment