February 22, 2019




Na Saleh Ally
MKONGWE Mrisho Ngassa amesema katika familia yao wamefundishwa mkubwa hakosei, ndiyo maana hawezi kuanza kumkosoa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro hadharani.


Muro ambaye ni mwanamichezo, mchambuzi, shabiki na mwanachama wa Yanga alitoa maoni yake kuhusiana na kikosi cha Yanga.

Wakati akizungumza alieleza namna ambavyo anaamini kikosi hicho kilivyo kuhusiana na mambo kadhaa.

Moja lilikuwa ni kuhusiana na Kocha Mwinyi Zahera ambaye alimuita ni sawa na mhamasishaji tu.

Zahera, raia wa DR Congo, amekuwa kipenzi cha Wanayanga kutokana na juhudi kubwa anazozifanya kuhakikisha kikosi chake kinafanya vema katika michuano mbalimbali inayoshiriki licha ya kuelezwa kwamba kinaandamwa na ukata.

Pamoja na hivyo, Muro alimuona ni mhamasishaji akitumia neno “hawezi kuwa kocha”. Jambo hili lilionekana kuwakwaza sana Wanayanga ambao walimshambulia kwa maneno mengi makali, mitandaoni.

Kama haitoshi, Muro aliweka msumari wake kwa kusema kwamba wachezaji kama Haruna Moshi 'Boban' na Mrisho Ngassa wamechoka na hawakupaswa kuwa Yanga.


Bosi huyo wa Arumeru alionyesha kutofurahishwa na Yanga kuwasajili wakongwe hao akiwaeleza kwamba miili yao imechoka akiamini hawawezi kuwa msaada katika ligi kuu na michuano mingine.


Hakuna ubishi Muro alikuwa akitoa maoni yake kama mwanamichezo lakini alibaki palepale kwenye shida ya "kuhemka" na kusema mambo utafikiri kuna ugomvi.


Alisahau kabisa kwamba Yanga ipo kileleni, hata kama ikitokea jambo gani itabaki kuwa ya pili inayogombea nafasi ya kwanza. Maana yake ni Top of Two. Hii ni moja ya timu bora kabisa za Ligi Kuu Bara kwa msimu huu.


Kama timu inaongoza ligi na wanaotoa mchango ni hao wakongwe, tatizo nini? Zahera ndiye aliyepitisha Boban asajiliwe, lazima anajua anachokihitaji na kocha huyo ni mjuzi kuliko Muro.


Hata kile kitendo cha Muro kusema Zahera ni mhamasishaji si sahihi kwa kuwa kwa taifa kama DR Congo lililopiga hatua kubwa katika soka linamtegemea katika timu ya taifa, vipi aonekane ni kocha wa kubahatisha na kufikia kuwa mhamasishaji!

Muro hakuwa sahihi, huenda alijisahau wakati akitoa maoni akafanya kama alivyozoea zamani bila ya kuangalia sasa yuko upande au nafasi ipi.


Kitu kizuri zaidi ambacho amekifanya Muro ni kuomba radhi jioni ya juzi. Aliwaomba wote aliowakwaza wamuwie radhi. Huu ni uungwana na vema kumsikiliza kwa kuwa amerudi nyuma na kutambua alichokifanya hakikuwa sahihi.


Kabla ya Muro hajaomba radhi, Ngassa alizungumza na kuonyesha ukomavu wa hali ya juu. Kiwango hicho cha ukomavu sikukitegemea kutoka kwake.


Ngassa ametuonyesha kweli sasa ni mkongwe kwa kuwa badala ya kujibu kwa jazba alimuacha Muro awe huru na alichozungumza na yeye akasisitiza kazi yake ni kucheza mpira.


Maneno aliyosema Ngassa ni aghalabu kuyasikia yakitamkwa na wachezaji wengi wa hapa nyumbani Tanzania kwa kuwa wengi wangependa kujibu mapigo kwa maneno ikiwezekana makali zaidi ya yake yaliyowakwaza wao.

Wanadamu tuna tabia ya kujibiana kwa kupeana maumivu. Hili ndilo wengi tungependa litokee kwa yule aliyekuumiza. Lakini Ngassa ameonyesha inawezekana wanamichezo au wanasoka kuwa watu wenye busara ya juu wakati mwingine kuwashinda hata viongozi wa serikali.


Kwa Muro hili litakuwa funzo, kama alivyomueleza Ngassa kuwa ni rafiki yake lakini anamueleza ukweli, basi wakati mwingine vizuri kutafakari kwamba Yanga ya "Kampa Kampa Tena", inaweza kurudishwa na Wanayanga wenyewe kwa kushirikiana na kujua sahihi cha kufanya badala ya kulaumiana na kushambuliana.


Kama kuna tatizo la kifedha, vipi iwe rahisi kupata wachezaji wa bei ya juu. Kama ataelewa, hii pia ni sababu ya Yanga kuwa na watu walio tayari kulipwa kiwango cha kawaida na wakajitolea zaidi.


Acha iwe Ngassa kampa Muro.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic