February 19, 2019


BAO la mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere, limezuia shilingi milioni 20 walizoahidiwa kupewa wachezaji wa Yanga kutoka kwa mabosi wao.

Timu hizo, zilivaana wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mchezo uliomalizika kwa Simba kufanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Kagere.

Ushindi huo walioupata Simba umewafanya wafikishe pointi 39 wakiwa chini ya Yanga wenye 58, lakini kama Simba wakishinda viporo vyao vinane vilivyobaki, wataongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, wachezaji hao waliahidiwa fedha hizo kama wangefanikiwa kuifunga Simba katika mchezo huo wa ligi uliojaa upinzani mkubwa.

Mtoa taarifa huyo alisema, wachezaji hao walipewa ahadi hiyo viongozi walipovamia Nafeland Hotel iliyopo Manzese ambako Yanga waliweka kambi ya siku moja kujiandaa na mchezo wa Simba wakitokea Morogoro walipokuwa awali.

Aliongeza kuwa, kipigo hicho walichokipata Yanga, kimewafanya wakose fedha hizo na kusababisha kusikitika na wengine kulia baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa na mwamuizi wa kati, Hance Mabena wa mkoani Tanga.

“Kama unakumbuka baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa na mwamuzi wa kati kuashiria kumalizika kwa pambano hilo, wachezaji wengi walikaa uwanjani na kulia.

“Kilio hicho kilikuwa na maana yake ni kusikitika kuzikosa fedha hizo walizoahidiwa na viongozi hao waliofika kambini kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji siku moja kabla ya mechi.

“Hata hivyo, kocha Zahera (Mwinyi) aliwatuliza wachezaji hao waliokuwa wakilia wakiwa vyumbani na kuwataka kutokatishwa tamaa na badala yake kujiandaa na michezo ijayo ya ligi,” alisema mtoa taarifa huyo.

Beki mkongwe wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani alithibitisha hilo kwa kusema: “Hizi mechi kubwa zinazozikutanisha Simba na Yanga, ahadi nyingi zinatolewa za fedha kutoka kwa viongozi na baadhi ya wanachama.

“Kama mechi hii na Simba tuliahidiwa fedha nyingi ambazo ni siri kama tungefanikiwa kuwafunga wapinzani, lakini bahati haikuwa upande wetu, pia niwapongeze wachezaji wenzangu tumeonyesha kweli tulikuwa tunataka ushindi licha ya kufungwa bao hilo moja lililotokana na kosa dogo.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic