Na George Mganga
DAR ES SALAAM, Kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' leo kinacheza na Uganda 'The Cranes' katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za AFCON ambazo zitafanyika nchini Misri mwaka huu.
Stars inakipiga na Uganda majira ya saa moja za usiku ikiwa na kumbukumbu ya kwenda suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Nambole Stadium huko Kampala, Uganda.
Kuelekea mechi ya leo, tayari Uganda imeshafuzu AFCON na leo inacheza kwa ajili ya kukamilisha ratiba pekee huku Stars ikisaka matokeo ili kupata nafasi hiyo adhimu.
Mbali na Stars kusaka ushindi, watanzania kwa ujumla wanaombea mechi ya Cape Verde na Lesotho iweze kumalizika kwa sare au Lesotho ifungwe na Cape Verde ili Tanzania iandike historia kwa mara nyingine.
Kuiombea Lesotho imalize mechi yake na Cape Verde kwa sare itaisaidia Stars kufuzu endapo itapata matokeo dhidi ya Uganda leo kwani Lesotho naye akishinda kitakachoangaliwa HEAD to HEAD kwa timu mbili.
Msimamo kundi L upoje
Msimamo unaonesha katika kundi L, Uganda imeshika nafasi ya kwanza ikiwa na alama 13 huku Stars ikishika namba mbili na alama tano sawa na Lesotho iliyo ya tatu, wakati Cape Verde ikishika nafasi ya nne ikiwa mkiani na alama zake nne.
Kocha Amunike anasemaje
Kocha Mkuu wa Stars, Mnigeria, Emmanuel Amunike, amesema wao wameshajiandaa kuelekea mechi na Uganda na wako tayari kuandika historia mpya.
Amunike ameeleza kuwa wapo tayari kwa mchezo wa leo ili kuhakikisha Stars inafuzu kutinga AFCON huko Misri.
"Tumeshajiandaa na tupo tayari kwa mchezo dhidi ya Uganda.
"Kila mchezaji yuko fiti na tunaamini tutafanya vizuri ili kupeperusha bendera ya Tanzania.
"Mechi itakuwa ngumu kutokana na historia ya mechi za Uganda na Tanzania zilivyo lakini tutapambana."
Mara ya mwisho Stars kufuzu kwenda AFCON ilikuwa ni mwaka 1980 sawa na miaka 39 iliyopita mpaka sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment