KUMSAJILI OLE MAN UNITED HALIKUWA CHAGUO SAHIHI, VAN GAAL AFUNGUKA
KOCHA wa zamani wa Manchester United, Louis van Gaal, amesema kuwa Manchester United hawakufanya lolote kumtoa kocha Jose Mourinho na kumpa kibarua Ole Gunnar Solskjaer.
Desemba mwaka jana Manchester United walimtupia virago Mourinho na kumpa timu hiyo Solskjaer.
Hata hivyo, Van Gaal ambaye naye aliifundisha Manchester United baada ya kutimuliwa kwa David Moyes ambaye aliingia kwenye timu hiyo kuchukua nafasi ya Alex Ferguson ambaye alistaafu amesema kuwa halikuwa chaguo sahihi.
Van Gaal ambaye hivi karibuni alistaafu kufundisha soka amesema kuwa makocha wote wawili wanalinda sana lango lakini tofauti yao ni kwamba Solskjaer anapata ushindi.
Van Gaal amesema kinachowakomboa United ni kwamba kocha huyo anapata ushindi kwenye michezo yake anayocheza lakini uongozi wa timu hiyo haukufanya chaguo sahihi.
Solskjaer amefanikiwa kupata ushindi wa michezo 14 kati ya 19, ambayo ameiongoza United kama kocha wa mpito.
“Mourinho alibadilisha mfumo wangu na kucheza soka la kushambulia kwa kushtukiza huku akilinda sana lango.
“Tazama sasa United wana kocha wa aina hiyo hiyo anashambulia kwa kushtukiza na kulinda sana lango, faida kubwa ambayo wanakutana nayo United ni kwa kuwa Solskjaer yeye anapata ushindi.
“Tazama jinsi Manchester United inavyocheza sasa siyo kama ambayo ilikuwa ikicheza chini ya Sir Alex Ferguson, inacheza soka la kushambulia kwa kushtukiza na kurudi kulinda lango lao.
“Kama mtu anaupenda mfumo huo sawa, lakini sidhani kama unaweza kuwa bora kuliko wangu wa kushambulia,” alisema Van Gaal .
United kwa sasa wapo pointi mbili nyuma ya timu zinazowania nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England na watakutana na Barcelona kwenye mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.








0 COMMENTS:
Post a Comment