March 25, 2019


DAR ES SALAAM: KWA mara nyingine, maandalizi ya ndoa ya staa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mchumba’ke, Francis Siza ‘Majizo’, imevurugwa, Risasi Jumamosi limedokezwa.

ITAFUNGWA LINI?

Katikati ya shauku ya kutaka kujua ndoa ya Lulu na Majizo itafungwa lini baada ya mrembo huyo kuvishwa pete ya uchumba, kumekuwa na tetesi nyingi zenye kuleta mvurugano wa kuharibu jambo hilo la heri.

Kwenye kutaka kuvuruga mambo, hivi karibuni wabaya wa Lulu walisambaza habari mbaya zikimhusisha mwigizaji wa filamu za Kibongo, Rose Alphonce ‘Muna Love’ kuwa ndiye chanzo cha chokochoko hizo za kuvuruga ndoa ya Lulu. Ifahamike kwamba Lulu na Muna, mbali na kuwa waigizaji, pia ni marafiki wa karibu tangu kitambo kiasi cha watu kudhani ni ndugu.

USHIRIKINA WATAJWA

Madai ya wafitini wa ndoa ya Lulu yalimtuhumu Muna kuwa ndiye aliyesambaza habari kuwa Lulu ana tabia za kishirikina hivyo hata mchumba wake huyo alimrudisha kwake kwa njia ya ndumba baada ya kutaka kumwacha. Kufuatia madai hayo, gazeti hili lilizungumza na Muna ambaye alifunguka kuwa maneno hayo hayana ukweli wowote.

Muna alipingana vikali na madai kwamba baada ya kuokoka aliamua kusema ukweli wa maovu yote aliyokuwa akiyafanya huko nyuma akiwa na Lulu. Muna alikanusha madai kuwa alimfuata Majizo na kumweleza siri za Lulu kwamba ana tabia za kishirikina za kwenda kwa waganga na hata uhusiano wao ni kwa sababu za kishirikina.

Kwa mujibu wa madai hayo ya wabaya wa Lulu, baada ya Majizo kujihakikishia kwamba vitu hivyo ni vya kizushi na kichonganishi, alipuuza na kuendeleza mahaba na mkewe huyo mtarajiwa. Lakini madai yanaendelea kusema kuwa, familia yake haikukubaliana na mawazo ya ndugu yao huyo, huku wakisogeza mbele tarehe ya kufunga ndoa.

MAJIZO ASIMUOE LULU?

Kuna madai kuwa, ndugu wengine walitaka asimuoe Lulu kabisa na ikiwezekana amuoe zilipendwa wake, Hamisa Mobetto, jambo ambalo mwanaume huyo hayupo tayari kulifanya.

Muna aliendelea kusema kuwa alishtushwa na madai hayo na kusema kwamba yeye hajui chochote kinachoendelea hivyo anashangaa kuambiwa hivyo na kusababisha mvurugano wa maandalizi ya ndoa ya Lulu na Majizo.

“Jamani mimi sifahamu chochote kuhusu suala hilo, ndiyo kwanza ninawasikia mnaniambia, sielewi chochote kinachoendelea huko mitandaoni, niko bize na watoto, ila Mungu wangu awabariki wote wasionitakia mema,” alisema Muna.

LULU AMWACHIA MUNGU

Hata hivyo, Risasi Jumamosi lilizungumza na Lulu ambaye alifunguka kwa kifupi kuwa siyo kila kitu kinahitaji maelezo hivyo anawaacha wanaoamini hayo mambo waendelee kuamini.

Lulu aliongeza kuwa, kuna mambo mengi yanazungumzwa, lakini yeye alishaamua kumwachia Mungu ndiye anajua ukweli wote. “Binafsi naamini katika mawazo na mitazamo huru, kuanzia kwangu na kwa watu walionizunguka na jamii nzima kwa jumla. “Unajua siyo kila kitu kitahitaji kujieleza, acha kila mtu aamini kile anachoamua kuamini,” alisema Lulu.

KUTOKA KWA MHARIRI

Taarifa za Lulu kufunga ndoa na Majizo zilianza kuzagaa tangu mwaka juzi, hata hivyo mpaka sasa hawajakamilisha tendo hilo takatifu. Ingawa maelezo yasiyo ya shaka yanasema kuwa Majizo amedhamiria kwa dhati kumuoa Lulu, tunawashauri wawili hao kupuuza kila aina ya uchonganishi ili waweze kufanikisha jambo hilo jema kwani wafitini hawakosekani.

Waswahili wanasema, “mti wenye matunda, hupopolewa mawe” hivyo wazibe masikio yao na watazame mapenzi yao ya dhati yaliyopo mioyoni mwao, wasonge mbele. Ndoa ni baraka. Tunawatakia kila la heri katika hatua hiyo muhimu kwenye maisha ya binadamu ulimwenguni.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic