April 1, 2019







NA SALEH ALLY
Klabu kongwe ya soka nchini Yanga, imepanga kufanya uchaguzi wake wa viongozi mnamo Aprili 28, mwaka huu.


Uamuzi huo umetangazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, George Mkuchika ikiwa ni siku moja tu baada ya wajumbe wawili waliokuwa wamebaki, Hussein Nyika na Samuel Lukumay kujiuzulu.


Kujiuzulu kwa Lukumay na Nyika kumetoa nafasi kwa Yanga kufanya uchaguzi usiokuwa na vipande kwa kuwa utakuwa uchaguzi utakaowajumuisha Wanayanga bila ya kuchagua viongozi kadhaa wa kuchaguliwa kwa ajili ya kujaza nafasi.


Wakati Yanga wakisubiri siku ya uchaguzi, wameunda kamati ya watu saba itakayosimamia kazi za Yanga katika kipindi cha kwenda katika uchaguzi.

Msisitizo wa Mkuchika umekuwa hivi; kamati hiyo si ya kuendesha timu badala yake, inasimamia kazi za Klabu ya Yanga.

Wajumbe saba wa kamati hiyo ni Moses Katabaro, Hussein Ndama, Maulid Kitenge, Said Ntimizi, Said Ntimizi, Nyika na Lukumay.

Uamuzi wa Yanga kutaka kufanya uchaguzi ni mzuri sana na ukiangalia ni kama Lukumay na Nyika wamepata shinikizo “shauri” ili wajiuzulu na kutoa nafasi kwa Yanga kufanya uchaguzi “full”.

Binafsi naona ni enzo sahihi hasa na Yanga wanapaswa kulisimamia vizuri ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika. Nasema wasimamie vizuri kwa kuwa hofu yangu, kusiingie na mambo mengine yanayoweza kuwa chanzo cha uchaguzi huo kutofanyika.


Yanga wamekuwa wanapita milima na mabonde na uchaguzi umekuwa ukipigwa danadana mara kadhaa kutokana na matakwa ya watu mbalimbali ambao huenda kuwepo kwa uongozi uliochaguliwa na wanachama ni sehemu ya kuwabana kufaidika na Yanga.

Uchaguzi wa Yanga umekuwa katika wakati mgumu, lakini wanaoufanya uwe uchaguzi mgumu ni Wanayanga wenyewe na inaonekana kuna ambao wamekuwa wakifaidika na Yanga kutokuwa chini ya uongozi wa kuchaguliwa.


Unaona, Yanga imejiendesha muda mrefu bila ya kuwa na mwenyekiti na makamu wake, hata makatibu wakuu kwa muda wamekuwa ni wale wanaokaimu, jambo ambalo linaifanya Yanga kutotulia katika ngazi ya kiuongozi.


Wakati ndiyo huu na Yanga wanapaswa kuutumia vizuri kuhakikisha lengo la uchaguzi linafikiwa. Ufanyike na kuanzisha njia mpya zenye matakwa sahihi kuifanya Yanga kuwa na watu wanaoiongoza na wanaowajibika kwa wanachama.


Angalia shida za sasa walizonazo Yanga, hakuna anayeweza kuwajibika kwa kuwa si mwenyekiti wala makamu. Kuwa na wanaowajibika ni rahisi kuhoji na kufanikisha hasa katika uendeshaji kwenda katika maendeleo.


Hivyo, kwa wale huenda walikuwa na nia ya kuuzuia tena uchaguzi, safari hii vema wakarudi nyuma ili kuisaidia klabu hiyo kupata viongozi wake ili iweze kujiendesha kwa nia sahihi na kiushindani.


Ukitaka kuonyesha mapenzi kwa kitu fulani, basi wakati mingine usijali zaidi matakwa yako badala yake faida ya kitu hicho. Wanaoweza kuisaidia na kuiokoa Yanga ni Wanayanga wenyewe kama ambavyo pia wanaweza kuiangamiza. 


Msisitizo, Aprili 28 uchaguzi ufanyike kweli na kamati itekeleze majukumu yake kuhakikisha inafikia malengo ya kufanikisha uchaguzi huru na wa haki ili kuirudisha Yanga katika mstari.




1 COMMENTS:

  1. Sawa mwana Yanga jaribu kuwa unahimiza wanachama wenzako wasilete tena fuzjo, umenielwa we saleh

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic