April 1, 2019






NA SALEH ALLY
Yanga imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho linalodhaminiwa na Azam Sports, jambo ambalo linaendelea kuifanya Yanga iwe katika moja ya timu zilizofanya vizuri katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara na kombe hilo.


Unaweza kuhoji, kwamba kwa nini nasema Yanga ni moja ya timu ambazo zimefanya vizuri? Huenda ikateleza lakini uhalisia unaonyesha hivi, Yanga ni moja ya timu bora kabisa. Nitakuambia kwa nini.


Hadi sasa ndiyo inayoongoza ligi kwa maana ya kukusanya pointi nyingi zaidi. Kama itakwama hapo mbele litakuwa jambo jingine. 


Kwa upande wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Yanga sasa ni moja ya timu bora nne kwa kuwa imeingia nusu fainali. Huu ndio ubora wao hadi sasa, kama baadaye tutazungumza kulingana na wakati.


Yanga wametinga nusu fainali baada ya ushindi wa mabao 4-3 wa mikwaju ya penalti dhidi ya Alliance ya jijini Mwanza katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo, juzi Jumamosi.

Wakati Yanga inatinga nusu fainali, shujaa wake alikuwa ni kipa Klaus Kindoki ambaye alipangua mkwaju wa mwisho wa penalti na Yanga ikafanikiwa kusonga mbele.


Hakuna ubishi, mchezo huo ulimalizika kwa dakika 90 kuwa sare ya bao 1-1, Alliance wakisawazisha lakini bado ndani ya muda huo, Kindoki raia wa DR Congo alifanya kazi yake vizuri.


Kama unakumbuka, Kindoki ndiye amekuwa kipa ‘kicheko’ kwa watani wa Yanga, kwamba wamempata kipa kutoka nje ya Tanzania lakini anaonekana ni garasa.


Wamekuwa wakifanya utani lakini unaendana sana na uhalisia. Nasema hivyo kwa kuwa Kindoki amekuwa hafanyi vizuri na kiwango chake kimekuwa duni na si msaada kwa Klabu ya Yanga.


Ndio maana unaona, baada ya kuondoka kwa Beno Kakolanya kukawa na hofu kubwa ndani ya Yanga. 


Unaweza kusema, kama Yanga ina kipa kutoka nje, vipi iwe na hofu baada ya kuondoka kwa kipa aliyekuwa siku zote pale. Maana yake yule wa kutoka nje haaminiki na kama ni hivyo basi kazi yake haikuwa na kiwango.


Unaona hofu ilipozwa na kipa kinda, Ramadhani Kabwili ambaye alijitahidi kufanya kazi yake vizuri. Kama unakumbuka, Kabwili alipaswa kuwa kipa namba tatu lakini akageuka kuwa shujaa wa Yanga kwa kuwa kiwango cha Kindoki kilikuwa duni.


Kocha Mwinyi Zahera alijitahidi kumpa nafasi tena na tena lakini Kindoki aliendelea kurudia makosa yaleyale, mwenyewe akarudi nyuma na kumuweka kando huku akimtetea kwa maneno kwamba ni bora.

Watanzania wapenda mpira wangependa maneno yawe vitendo na huenda sasa Kindoki ameanza kutimiza hilo, kwamba vitendo badala ya maneno tu.

Binafsi naona bado Kindoki hajailipa Yanga vizuri kwa mshahara ambao wamekuwa wakimlipa. Bila Shaka utakuwa ni kuanzia dola 1,000 (zaidi ya Sh milioni 2.5) kwenda juu.

Maana kazi yake imekuwa duni, ameendelea kukaa benchi na hakuwa tegemeo licha ya kwamba ni mchezaji wa kimataifa. Sasa anaanza kuonyesha kile alichotakiwa kufanya tangu zamani.

Ndio maana nimewahi mapema kutaka kumkumbusha Kindoki kwamba ameanza kuonyesha kwamba alistahili kusajiliwa na Yanga kutokea nje lakini hajathibitisha.

Amekuwa akipokea mshahara wake bila ya kazi sahihi kwa muda mrefu. Kupatia mara mbili au tatu hauwezi kuwa uthibitisho, hivyo anapaswa kuonyesha kiwango bora ya hicho zaidi na zaidi na kuwa tegemeo na msaada wa juu kwa klabu yake.

Kama haitakuwa hivyo, bado itaonekana si sahihi kwa kuwa atakuwa anaibuka na kupotea kadiri siku zinavyosonga mbele na kwa mchezaji bora, kiwango hakipaswi kuwa sawa na milima, leo juu kesho chini.


Mchezaji wa kimataifa, lazima awe na faida kwa klabu na taifa husika na kama hana, basi haina haja ya kuwa naye na badala yake bora kukuza wazawa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic